2018-05-09 09:59:00

Mafrateri wawili kutoka Tanzania wapewa Daraja ya Ushemasi, Roma


Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanafundisha kwamba, Mashemasi hushiriki kwa namna ya pekee utume na neema ya Kristo. Sakramenti ya Daraja huwapa chapa isiyoweza kufutwa na hufananishwa na Kristo, aliyejifanya “Shemasi”, yaani mtumishi wa wote. Mashemasi kimsingi ni wasaidizi wakuu wa Askofu na Padre katika maadhimisho ya Mafumbo ya Mungu, hasa Fumbo la Ekaristi Takatifu. Wao hugawa Komunyo Takatifu, husimamia na kubariki Ndoa; hutangaza na kuhubiri; huongoza mazishi na kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma mbali mbali za upendo. Mei mosi mwaka 2018, ilikuwa siku ya furaha kwa jumuiya ya Seminari ya Bikira Maria, Kikao cha Hekima (Collegio Ecclesiastico Internazionale Sedes Sapientiae), hapa mjini Roma kwa kuwa waseminari wake saba kutoka sehemu mbalimbali ulimwenguni waliijongea Altare ya Bwana kwa kupewa daraja ya Ushemasi, kati yao, wawili wanatoka Tanzania.

Mwadhama Giuseppe Kardinali Versaldi, Rais wa Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki, Mei Mosi, 2018 aliongoza Ibada ya Misa Takatifu na kutoa Daraja ya Ushemasi kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Apollinari, hapa mjini Roma.  Ibada hii imehudhuriwa pia  na Askofu Mkuu Paul Ruzoka, wa Jimbo Kuu Katoliki la Tabora, Tanzania. Mashemasi hao saba wanatoka katika nchi zifuatazo: China (1), Japan (1), Ufilipini (1), India (1), Afrika Kusini (1) na Tanzania (2). Wazazi, ndugu, jamaa, marafiki na wafadhili wa mashemasi hao waliudhuria na kushiriki kikamilifu katika sherehe hiyo, jambo lililofanya siku hiyo kufana kisawasawa.  Akihubiri katika misa hiyo Kardinali Versaldi amewaasa mashemasi hao kufuata mfano wa Yesu Kristo aliyekuja kutumikia na wala si kutumikiwa. Tena aliwakumbusha kulingana na Injili ya siku hiyo kuwa si wao waliomchagua Yesu, bali ni Yesu aliyewachagua wao, hivyo wajikabidhi mikononi mwa Kristo ili waweze kuzaa matunda katika utume na maisha yao. Pia aliwahasa kufuata mfano wa Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi, aliyekuwa mchapakazi na mlinzi wa Familia Takatifu.

Furaha ya Jumuiya ya Seminari ya Bikira Maria, Kikao cha Hekima zilipambwa zaidi na shangwe za jumuiya ya watanzania wanaosoma na kuishi Roma. Miongoni mwao wakiwemo waseminari, ambao wengi wao walikuwa ni wanadarasa katika hatua mbalimbali za malezi ya seminari wa mashemasi wawili kutoka nchini Tanzania.  Wakizungumza kwa nyakati tofauti mashemasi hao wamewashukuru watu wote waliowasaidia kufikia hatua hiyo ya kuijongea Altare ya Bwana. Wanaomba sala za waamini wote ili waweze kuendelea kutimiza mapenzi ya Mungu; nao wanaahidi kuwaombea watu wote na wanaahidi pia kutenda kazi kwa ari na moyo mkuu.

Tukiendelea kuwaombea mashemasi hao wapya, tufahamu kwa ufupi wasifu wa wawili wao ambao ni mheshimiwa Shemasi Jerome Gerald Mkindi wa Jimbo Katoliki la Same, Tanzania na mheshimiwa Shemasi Christian Mpalasinge Kapaya wa Jimbo kuu Katoliki Tabora, Tanzania. Shemasi Jerome Gerald Mkindi ni mzaliwa wa Jimbo Katoliki la Same, parokia ya Manoro, kigango cha Kwizu. Shemasi Mkindi alizaliwa Machi, 07, 1990 huko Kwizu, mkoani Kilimanjaro, Tanzania. Alipata elimu ya msingi katika shule ya Msingi Kwizu, mwaka 1997 na kuhitimu elimu hiyo mwaka 2003. Mwaka 2004 aliudhuria masomo ya awali kabla ya sekondari (pre-form one) huko Dido Vocation Training Center. Alipata elimu ya sekondari katika seminari ndogo ya Chanjale ya Jimbo la Same, mwaka 2005 na kuhitimu kidato cha nne mwaka 2008. Mwaka 2009 hadi 2011 alipata elimu ya kidato cha tano na sita katika seminari hiyo hiyo ya Chanjale.

Shemasi Jerome Gerald Mkindi alijiunga rasmi na malezi ya Upadre na kuanza malezi katika kituo cha kulea miito cha Jimbo la Same (Dido Vocation Training Centre) mwaka 2011. Mwaka huo huo alianza masomo ya Falsafa katika Seminari kuu ya Mtakatifu Anthoni wa Padua, Ntungamo iliyoko Bukoba, Tanzania na kuhitimu diploma katika falsafa mwaka 2014. Baada ya hapo alijiunga na Chuo Kikuu cha Kipapa cha Msalaba Mtakatifu (Pontificia Università della Santa Croce) kilichopo Roma kwa masomo ya Taali Mungu mwaka 2014 na kuhitimu kwa kupata shahada katika taalimungu mwaka 2017.

Kwa upande wake, Shemasi Christian Mpalasinge Kapaya ni mwanajimbo wa Tabora, kutoka Parokia ya Familia Takatifu-Ipuli, Kigango cha Bikira Maria Mpalizwa mbinguni-Ifucha. Shemasi Kapaya alizaliwa Aprili 25, 1990, jijini Dar es Salaam. Alipata elimu ya msingi katika shule ya msingi Ifucha iliyoko Manispaa ya Tabora, kuanzia mwaka 1997 mpaka 2003. Kisha akapata elimu ya sekondari katika Seminari ndogo ya Mtakatifu Charles Borromeo, maarufu kwa jina la Itaga, ya Jimbo kuu la Tabora; kuanzia mwaka 2004 mpaka mwaka 2007 alipohitimu kidato cha nne. Alijiunga na shule ya sekondari ya Pugu iliyoko jijini Dar es Salaam mwaka 2008 hadi 2010 kwa masomo ya kidato cha tano na cha sita.

Baada ya majiundo ya awali, Shemasi Kapaya alijiunga rasmi na malezi ya upadre katika Jimbo kuu la Tabora: Mnamo mwezi Machi 2011 mpaka Septemba kisha mwaka huo huo alijiunga katika nyumba ya malezi ya upadre ya Jimbo kuu la Tabora.   Mwezi Oktoba, 2011 alianza masomo ya Falsafa katika Seminari kuu ya Mtakatifu Anthoni wa Padua-Ntungamo iliyoko Bukoba-Tanzania na kuhitimu diploma katika falsafa Juni 2014. Baada ya hapo alijiunga na Chuo Kikuu cha Kipapa cha Msalaba Mtakatifu (Pontificia Università della Santa Croce) kilichopo Roma kwa masomo ya Tauhidi oktoba 2014 na kuhitimu kwa kupata shahada katika masomo ya kitaalimungu, Juni 2017. Mara baada ya kuhitimu masomo ya Taalimungu kwa sasa mashemasi hawa Kapaya na Mkindi wanendelea na masomo ya Falsafa katika ngazi ya shahada ya uzamili katika Chuo kikuu cha Kipapa cha Msalaba Mtakatifu (Pontificia Università della Santa Croce), hapa Roma.  Tuzidi kuwaombea hawa mashemasi wetu neema mbalimbali wanazozihiataji  katika utume wao.

Na Frt. Joachim Makaya.

Seminari ya Bikira Maria, Kikao cha Hekima, Roma.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.