2018-05-08 06:30:00

Wananchi wa Perù simameni kidete kupinga utamaduni wa kifo!


Baraza la Maaskofu Katoliki Perù, CEP, linayashutumu Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yanayopokea fedha nyingi na hivyo kujijenga kiuchumi kwa ajili ya kupandikiza utamaduni wa kifo kwa kukumbatia sera za utoaji mimba nchini humo. Zawadi ya maisha inalindwa kikatiba, lakini kutokana na uchu wa mali na fedha, NGO hizi zimekuwa ni mahali pa kupandikiza utamaduni wa kifo. Jitihada zote hizi zinakwenda kinyume wanasema Maaskofu wa Perù na sera za kupambana na uhalifu, mauaji, utekaji nyara na ubakaji wa wanawake na wasichana bila kusahau mauaji ya wanawake majumbani mwao!

Maaskofu wanasikitika kuona rasilimali fedha ambayo ingeweza kutumika kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi, inatumbukizwa katika sera za utoaji mimba. Baraza la Maaskofu Katoliki Perù limeyasema haya katika maandamano makubwa ya kutetea uhai dhidi ya kifo yaliyofanyika nchini humo, Jumamosi, tarehe 5 Mei 2018 kwa kusindikizwa pia na ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anayeitaka familia ya Mungu nchini Perù kusimama kidete: kulinda, kutetea na kudumisha uhai wa binadamu, tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake, hadi mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu.

Uhai ni haki msingi ya binadamu na kwamba, hakuna mtu mwenye uwezo wa kumwondolea mtu uhai wake. Wananchi wa Perù wanahamasishwa kusimama kidete kutetea Katiba ya Nchi na Injili ya Uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Wananchi wasikubali watu wachache kuwapoka matumaini katika maisha yao na kwamba, huu ni wakati wa kuunganisha nguvu zao ili kutetea Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Kwa pamoja, washikamane katika kulinda utu na heshima ya binadamu, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi ili kudumisha amani na utulivu!

Na Padre Richard. A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.