2018-05-07 14:08:00

Papa Francisko: Wazee na wagonjwa wanalitegemeza Kanisa kwa sala


Baba Mtakatifu Francisko akiwa kwenye Parokia ya “SS. Sacramento” iliyoko kwenye kitongoji cha Tor dè Schiavi, nje kidogo ya Jimbo kuu la Roma, Jumapili, tarehe 6 Mei 2018 amepata fursa ya kuwatembelea na kuzungumza na wagonjwa pamoja na wazee Parokiani hapo, ambao wengi wao wanaishi katika upweke, lakini wanayo bahati ya kupatiwa huduma ya maisha ya kiroho pamoja na kuwashirikisha katika vyama vya kitume, ili kuwawezesha kuendelea kutoa mchango wao katika maisha na utume wa Kanisa.

Baba Mtakatifu katika salam zake amewaambia wazee na wagonjwa kwamba, sala na sadaka yao ni muhimu sana kwani zinalitegemeza Kanisa, changamoto na mwaliko kwa wazee kuhakikisha kwamba, wanakuwa karibu na vijana ili kuwarithisha tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni. Waendeleze majadiliano na watoto wadogo pamoja na vijana kwani katika maisha yao, wamebahatika kuwa na kumbu kumbu, ujuzi, maarifa na imani, wanayopaswa kuwarithisha vijana wa kizazi kipya na kamwe wasijisikie kuwa ni watu waliopitwa na wakati.

Baba Mtakatifu anawataka wazee kujifunza kutoka kwa wazee wenzao katika Maandiko Matakatifu waliojizatiti katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema hata katika uzee wao, jambo la msingi ni kumwachia nafasi Roho Mtakatifu ili aweze kutenda kazi ndani mwao! Wazee watambue kwamba, wao ni mzizi wa maisha ya jumuiya, kumbe, ni wajibu wao kurithisha uzoefu na kumbu kumbu za maisha. Wazee wawasaidie watoto kung’amua maana ya maisha, tunu za maisha ya Kikristo na kiutu na kwamba, uzoefu wao, tayari ni shahada tosha kabisa katika maisha. Wazee na wagonjwa waendelee kusali kwa ajili ya kuliombea Kanisa, watoto na vijana; waendelee kuwa karibu na Kanisa na waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake, hadi dakika ya mwisho wa maisha yao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 








All the contents on this site are copyrighted ©.