2018-04-30 07:54:00

Sinodi ya Maaskofu wa Amazonia 2019 ni mbinu mkakati wa uchungaji


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume huko Amerika ya Kusini hivi karibuni anasikitika kusema kwamba, ukoloni mamboleo unaojikita katika nguvu ya kiuchumi: kwa uchimbaji wa mafuta na gesi asilia; kilimo cha mashamba makubwa ili kukidhi mahitaji ya mali ghafi ya viwanda; ni mambo yanayotishia usalama, maisha, ustawi na maendeleo ya Amazonia. Baba Mtakatifu anawataka Maaskofu kuwa karibu zaidi na wakleri wao; kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya Kiinjili ili kupambana na saratani ya rushwa, ufisadi na kumong'onyoka kwa haki msingi, utu na heshima ya binadamu na kwamba, Maaskofu wathamini majadiliano katika ukweli na uwazi.

Haya ni mambo msingi kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu iliyoitishwa na Baba Mtakatifu Francisko. Lengo ni kuibua mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji zitakazokidhi mahitaji ya uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili; utamadunisho kwa kuhakikisha kwamba, tunu msingi za kiinjili zinamwilishwa katika tamaduni, mila na desturi za watu wa Amazonia pamoja na kuzisafisha zile zinazosigana na kupingana na Habari Njema ya Wokovu! Ni Sinodi itakayojikita katika mchakato wa kukuza na kudumisha haki msingi za binadamu kama njia ya kuenzi utu na heshima ya binadamu!

Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu katika mahojiano maalum na Gazeti la L’Osservatore Romano anasema kwamba, tayari mchaka mchaka wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu wa Amazonia umeanza na unaendelea kushika kasi tangu wakati wa hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko huko Amerika ya Kusini. Mtandao wa Kanisa Amerika ya Kusini, REPAM, ulioanzishwa kunako mwaka 2014 unaendelea kusimamia sera na mikakati ya maendeleo endelevu kwenye Ukanda wa Amazonia. Mtandao huu ni matokeo ya Mkutano mkuu wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini na Caribbean, uliofanyika huko Aparecida kunako mwaka 2007.

Mtandao huu, tayari umekwisha fundishwa kuhusu mchakato wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu na tayari wameanza kuchapa kazi, tema zinazotarajiwa kujadiliwa na Maaskofu pamoja na kuanza mchakato wa Hati ya Maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu wa Amazonia. Hapa kutakuwa na ushirikiano wa karibu sana kati ya wajumbe wa mtandao huu pamoja na Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu. Kipaumbele cha kwanza kinachotolewa na Mama Kanisa ni uinjilishaji na utamadunisho; ekolojia na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; haki msingi za binadamu na huduma ya maendeleo endelevu kwa makabila 240, hii ni changamoto changamani ambayo Kanisa linataka kuivalia njuga kwa kuibua mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji kwa ajili ya Ukanda wa Amazonia anasema Kardinali Lorenzo Baldisseri.

Kanisa katika maisha na utume wake kwenye Ukanda wa Amazonia, limejikita katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili; limeendelea kuinjilisha na kutamadunisha Injili, ili iweze kupenya katika: mila, desturi, tamaduni na maisha ya watu. Katika mchakato wa uinjilishaji, kuna mahali ambapo Kanisa liliteleza katika sera na mikakati yake, ndiyo maana Sinodi ya Maaskofu wa Amazonia inapania pamoja na mambo mengine: kuangalia matatizo, changamoto na fursa zilizopo ili kuweza kupyaisha mchakato wa uinjilishaji kwa kusoma alama za nyakati, ili hatimaye, Kanisa liweze kuwa na chapa ya familia ya Mungu kutoka Ukanda wa Amazonia kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko.

Lengo ni kuhakikisha kwamba, tunu msingi za maisha ya watu wa Amazonia zinazofumbatwa katika mila, desturi na tamaduni zao, zinaheshimiwa na kuthaminiwa kama daraja maalum la uinjilishaji unaofumbatwa katika utamadunisho. Mama Kanisa anataka kuimarisha sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa kusoma alama za nyakati, ili kweli mchakato wa maboresho uweze kuleta ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kalenda ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Amazonia imeanza rasmi mwezi Aprili kwa kikao cha Sekretarieti kuu ya Sinodi ambacho kimeongozwa na Baba Mtakatifu Francisko pamoja na kutoa muswada wa mapendekezo ya hati ya maandalizi ya Sinodi ya Maaskofu wa Ukanda wa Amazonia.

Hati ya Maandalizi baada ya maboresho itatumwa kwenye Mabaraza ya Maaskofu, Taasisi na kwa wadau mbali mbali, mwezi Juni, 2018 kwa kuzingatia ushauri utakaokuwa umetolewa na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kipaumbele cha kwanza ni kwa watu mahalia wa Ukanda wa Amazonia, wanao endelea kupokwa ardhi, rasilimali, utajiri, amana na tunu msingi za maisha kutokana na ukoloni mamboleo. Mila na desturi zao zinapaswa kuheshimiwa, kutunzwa na kuendelezwa anasema Baba Mtakatifu Francisko. Ukanda wa Amazonia unaonekana kuwa kama ni “kichwa cha mwendawazimu” kwani atu mbali mbali wanataka kukimbilia huko ili kujichotea utajiri na rasilimali za dunia kwa mafao yao binafsi. Haya ni matokeo ya rushwa na ufisadi unaopekenyua umoja, mshikamano na mafungamano ya kijamii huko Amerika ya Kusini. Kardinali Lorenzo Baldisseri anakaza kusema, uinjilishaji wa kina unakwenda sanjari na sera na mikakati ya maendeleo endelevu ya binadamu. Kanisa linataka kuimarisha mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote kwa kuijengea familia ya Mungu uwezo wa kupambana na hali yake!

Kuna haja ya kuwa na mipango miji makini, ili kuratibu idadi ya watu wanaohamia katika eneo hili ili kujitafutia fursa za ajira. Unyonyaji, ubaguzi na uvunjwaji wa haki msingi za binadamu ni kati ya changamoto kubwa zinazopaswa kuvaliwa njuga na Mababa wa Sinodi ya Maaskofu wa Amazonia. Kanisa badala ya kujikita katika mbinu yakuona, kuamua na kutenda; sasa mchakato huu unapaswa kutekelezwa kwa kutumia “miwani ya imani” na ili kuweza kupata ufanisi mkubwa, kuna haja ya toba na wongofu wa shughuli za kichungaji kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili”.  Kanisa daima linapaswa kusoma alama za nyakati kama alivyoshuhudia Mtakatifu Turibius wa Magroveyo wakati wa maadhimisho ya Mtaguso wa III wa Lima, ili kweli Kanisa liendelee kuwa ni sauti ya kinabii kwa watu wasiokuwa na sauti; watu ambao utu na heshima yao vinawekwa reheani! Viongozi wa Kanisa wanapaswa kuwa kati pamoja na watu katika utekelezaji wa sera na mikakati ya shughuli za kichungaji. Wajenge utamaduni wa kusikiliza kwa maskini na hatimaye, kujibu kilio cha maskini na wanyonge katika jamii. Ukanda wa Amazonia unahitaji viongozi watakaokuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake.

Kardinali Lorenzo Baldisseri anakaza kusema, maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Amazonia yatafanyika mjini Roma kunako mwaka 2019 kwa kulihusisha na kulishirikisha Kanisa zima, chini ya uwepo na ushiriki mkamilifu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kuna matumaini makubwa yatakayoibuliwa na Mababa wa Sinodi ya Maaskofu wa Amazonia kwa kuangalia medani mbali mbali za maisha na utume wa Kanisa kwa ajili ya mustakabali wa Ukanda wa Amazonia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 








All the contents on this site are copyrighted ©.