2018-04-30 07:31:00

Papa Francisko asema huduma kwa maskini ni ushuhuda wa imani tendaji


Chama cha Uhamsho wa Kikatoliki, RnS, ni chombo madhubuti cha majadiliano ya kiekumene, yanayoliwezesha Kanisa Katoliki kutembea bega kwa bega na waamini wa Makanisa mengine ya Kikristo; katika utekelezaji wa uekumene wa sala na huduma makini kwa maskini, na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kazi ya Roho Mtakatifu ni kuwafundisha na kuwaongoza waamini katika umoja na unaofumbatwa kwenye utofauti. Roho Mtakatifu ni chemchemi ya uekumene wa sala, huduma, maisha ya kiroho sanjari na uekumene wa damu!

Baba Mtakatifu Francisko daima anawahimizwa wakristo kufanya hija ya pamoja itakayowawezesha wote siku moja kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu! Anawataka kuendelea kuwa waaminifu kwa amri ya Kristo Yesu kwa waja wake, ili wote wawe wamoja kama anavyokaza kusema katika ile Sala ya Kikuhani, maarufu kama “Sala ya Yesu” inayopatikana kwenye Injili ya Yohane sura ya 17.  Yesu mwenyewe ndiye anayeomba umoja kwa Baba yake wa mbinguni kwa ajili ya wafuasi wake, ili kweli ulimwengu uweze kumwamini Kristo aliyetumwa na Baba wa milele! Kanisa lina matumaini makubwa ya uaminifu wao kwa Neno la Mungu, majitoleo katika huduma makini kwa maskini pamoja na ushuhuda wa maisha yaliyopyaishwa kwa karama na mapaji ya Roho Mtakatifu.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Dr. Salvatore Martinez, Rais wa Chama cha Uhamsho wa Kikatoliki nchini Italia, anawahimiza wanachama kujikita zaidi katika huduma ya upendo kwa maskini na wanaoteseka kama ushuhuda wa imani tendaji! Kuanzia tarehe 28 Aprili hadi tarehe 1 Mei 2018, vikundi na jumuiya za Chama cha Uhamsho wa Kikatoliki nchini Italia zinakutana huko Pesaro, ili kusali, kutafakari na kumshukuru Mungu kwa huruma na upendo wake wa daima. Mwaka huu, wanaongozwa na sehemu ya Injili ya Luka juu ya mfano wa Msamaria mwema aliyemwonea huruma yule mtu aliyeangukia kati ya wanyang’anyi.

Hata leo hii Yesu anawaambia wafuasi wake “Enenda zako, nawe ukafanye vivyo hivyo”. Changamoto ya huduma makini kwa Mungu na jirani ndiyo inayofanyiwa kazi na wajumbe wa Chama cha Uhamsho wa Kikatoliki nchini Italia kwa wakati huu. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake anakaza kusema, waamini wote wanahamasishwa na Kristo Yesu kujizatiti katika njia ya huduma kwa Mungu na jirani kama alivyofanya yule Msamaria mwema. Huu ni mwaliko wa kupenda kama Kristo Yesu alivyowapenda wafuasi wake, kiasi hata cha kuwa ni chemchemi ya huruma na mapendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Kumbe, ni wajibu wa waamini kuwa kweli ni mashuhuda, vyombo na manabii wa huruma na upendo wa Mungu kwa watu wa nyakati hizi, tayari kuwaganga na kuwafunga jeraha zao kwani huruma si jambo la nadharia, linaloelea kwenye ombwe, bali ni imani katika matendo, inayowawezesha watu mbali mbali kuona mwanga na nguvu ya Injili ya Kristo inayookoa na kuponya! Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kanisa linahitaji kuona ushuhuda huu ukimwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu na kwamba, kwa njia ya zawadi na karama za Roho Mtakatifu, waamini waweze kung’amua wito na utume wao unaofumbatwa katika huduma makini. Mwishoni mwa ujumbe wake, Baba Mtakatifu anapenda kuwaweka wanachama wote wa Chama cha Uhamsho wa Kikatoliki nchini Italia chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Kanisa. Anawaomba hata wao kumsindikiza katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa njia ya sala na sadaka zao.

Kwa upande wake Dr. Salvatore Martinez, Rais wa Chama cha Uhamsho wa Kikatoliki nchini Italia, RnS, anapenda kukazia zaidi umuhimu wa huduma kwa Mungu na jirani kama sehemu ya mchakato wa mwendelezo wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya Chama cha Uhamsho wa Kikatoliki Duniani, iliyoadhimishwa kunako mwaka 2017 kwa ushiriki mkamilifu wa Baba Mtakatifu Francisko pamoja na wajumbe wa Makanisa kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Wakati ule, Baba Mtakatifu aliwataka wanachama kusonge mbele kwa ari na moyo mkuu, kwa kumshukuru Mungu kwa wema, huruma, upendo na karama nyingi alizowakirimia katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, tayari kujifunga kibwebwe kwa imani na matumaini, ili kuweza kukabiliana na changamoto mamboleo.

Wanachama wanakumbumbushwa kwamba, wanaweza kuyafanya yote haya kwa neema na nguvu ya Roho Mtakatifu inayotenda kazi ndani mwao. Katika miaka ya hivi karibuni, wameweza kutafakari kwa kina na mapana karama na umisionari wa Chama cha Uhamasho wa Kikatoliki. Kuanzia sasa wanataka kuimarisha dhana ya ushuhuda wa utakatifu wa maisha ya kijumuiya, changamoto inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume “Gaudete et exsultate” yaani “Furahini na kushangilia, wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo” (Mt. 5:12). Huu ni mwaliko wa kumwachia nafasi Roho Mtakatifu ili aweze kuwapyaisha, tayari kushiriki kikamilifu katika utume wa Kristo Yesu hapa duniani.

Karama na utume wa Kanisa vinamwilishwa kwa namna ya pekee katika maisha ya kijumuiya, kwa njia ya huduma makini kwa maskini ambao kimsingi ni amana, utajiri na walengwa wakuu wa Habari Njema ya Wokovu. Mkutano huu ni nafasi muhimu sana ya kushiriki maisha na utume wa Kanisa kama Sakramenti ya Wokovu, kama ilivyokuwa kwa Yesu Msamaria mwema, watu waweze kuona mahangaiko ya jirani zao, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwahudumia kama alivyofanya yule Msamaria mwema. Dr. Salvatore Martinez anasema vikundi na jumuiya za Chama cha Uhamsho wa Kikatoliki nchini Italia zinapaswa kujizatiti zaidi katika toba na wongofu wa ndani, uponyaji, kuwekwa huru, msaada, ujenzi wa udugu, umoja, upendo na mshikamano ili kuanza kuchakarika katika hija ya maisha mapya!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.








All the contents on this site are copyrighted ©.