2018-04-30 08:15:00

Maandalizi ya Sinodi ya Vijana yanazidi kupamba moto Barani Afrika


Baba Mtakatifu Francisko ameitisha Sinodi ya maaskofu kwa ajili ya vijana, itakayofanyika mjini Vatican mnamo mwezi Oktoba 2018, ikiongozwa na kauli mbiu, Vijana, imani na mang’amuzi ya miito. Katika maandalizi ya Sinodi hiyo, Vatican iliandaa tovuti kwa ajili ya kutoa maoni ambamo vijana duniani kote, wamekuwa na fursa na uhuru huo wa kujaza fomu za maswali zilizoandaliwa na kuwekwa katika tovuti hiyo. Bara la Afrika kama mabara mengine, nalo linajiandaa katika ushiriki mzuri wa Sinodi hiyo ya vijana ili iweze kuzaa matunda kwa vijana wa Afrika pia.

Padre Donald Zagore, mmoja wa Jumuiya ya Kazi za Kitume ya Wamisionari wa Afrika, na anayefanya utume wake nchini Togo anasema, changamoto kwa Kanisa barani Afrika ni kuwapokea vijana wa kizazi kipya kwa mikono miwili, likizingatia maswali, dukuduku, hofu na mahangaiko yote waliyo nayo vijana kwa nia ya kuwaelimisha vema katika kufanya mang’amuzi sahihi ya miito anayowaitia Mungu na kuishi kila siku kadiri ya mapenzi yake. Sinodi ya vijana, ni fursa ya pekee sana sio kwa vijana tu, bali kwa Kanisa zima kujipyaisha, yaani kujibebisha fulani hivi. Kujibebisha huku kunapata chimbuko lake ndani ya Kristo anayesema “Nawaambia kweli, mtu yeyote asiyeupokea Ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hataingia humo” (Rej., Marko 10:13). Ni tumaini kubwa la bara la Afrika kwamba, sinodi ya vijana itakuwa kwa hakika msaada mkubwa katika kukabiliana na changamoto nyingi zinazolikabili Kanisa barani humo.

Itakumbukwa kwamba, Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini, hivi karibuni limeadhimisha utangulizi wa Siku ya Vijana Duniani iliyowakutanisha vijana pamoja na wazee wa Kanisa. Kardinali Wilfrid Fox Napier OFM, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Durban, Afrika ya Kusini, alimshukuru Mwenyezi Mungu kwa mafanikio makubwa  yaliyopatikana katika maadhimisho hayo yaliyofanyika Mwezi Desemba 2017. Hii ni changamoto kwa Mababa wa Kanisa kuwasikiliza kwa makini vijana wa kizazi kipya wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, anataka kuwasikiliza vijana moja kwa moja, wakichonga naye mubashara pasi na vizuizi wala vikwazo.

Jambo la msingi anasema Kardinali Napier ni kusikiliza na kujibu matamanio halali ya vijana yanayobubujika kutoka katika sakafu ya maisha na nyoyo zao. Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini, tayari limekwisha jibu maswali dodoso kuhusu maadhimisho ya Sinodi na tayari yamekwisha kutumwa kwenye Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu kwa utekelezaji zaidi. Maoni yaliyotolewa na vijana wakati wa maadhimisho ya utangulizi wa Siku ya Vijana Duniani huko Durban, Afrika ya Kusini, yatawasilishwa na ujumbe wa Afrika ya Kusini wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa vijana, mwezi Oktoba, 2018. Kanisa linatambua kwamba, vijana ni jeuri na matumaini ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake. Kumbe wanahitaji malezi na majiundo makini, ili kuweza kuzingatia mambo msingi katika maisha yao, tayari kufanya maamuzi magumu pamoja na kutoa sadaka kwa mambo mpito katika maisha!

Nalo Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika Ujumbe wa Kwaresima kwa mwaka 2018, linaialika familia ya Mungu nchini Tanzania kuepuka tabia ya kijana Kaini ya kutojali ndugu yake Abeli hata kufikia kujibu kwa kejeli “Sijui, kwani Mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?” (Rej., Mwanzo 4:9): Atajiju na zaidi sana “apambane na hali yake”. Katika kuepuka tabia kama hiyo ya kutokujali, ni muhimu Kanisa la Tanzania katika ujana wake kimisionari, kujikita zaidi katika Uinjilishaji wa kina, kwa kufanya toba na wongofu wa ndani, kisha kujielekeza kwa nguvu na ari mpya katika kujali wengine katika mahangaiko yao kwenye Nyanja zote za kisiasa, kiuchumi na kijamii, mintarafu kujali uhai na malezi mazuri ya watoto na vijana.

Na Padre Celestine Nyanda

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.