2018-04-28 07:48:00

Yesu ni Mzabibu wa kweli unaoshuhudiwa katika umoja na upendo!


Utangulizi: “Mimi ndimi mzabibu wa kweli na Baba yangu ndiye mkulima... akaaye ndani yangu nami ndani yake huyo huzaa sana”- karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika tafakari ya Neno la Mungu katika dominika ya tano ya Pasaka. Kristo anayejitambulisha leo kuwa ndiye mzabibu wa kweli anatualika tuwe na umoja naye kama matawi yalivyo kwa mzabibu. Ni mwaliko wa kutafakari juu ya umoja: umoja katika Kristo, umoja katika Kanisa, umoja katika taasisi na umoja katika jamii kwa ujumla.

Masomo kwa ufupi: Somo la Kwanza (Mdo. 9:26-31) linamwelezea Saulo ambaye hapo awali alikuwa mtesi na muuaji wa wakristo na sasa ameongoka. Anaenda Yerusalemu ili ajiunge na Mitume kutangaza Injili ya Kristo. Awali mitume wanasita kumpokea. Wanakuwa na wasiwasi kama ameongoka kweli au ana hila ya kuingia ili awaangamize kwa kirahisi. Kisha kukubaliwa na kuwa mmoja wao, Biblia inatumia maneno “akawa pamoja nao akiingia na kutoka”, akaanza kuhubiri Injili na matokeo yake Kanisa likapata kipindi cha amani; likakua na likaendelea kuongezeka.

Somo hili linakazia bado juu ya neema ya wongofu inayoweza kumbadili mwanadamu kutoka hali ya uasi, ubaridi wa kiimani na hata uadui na kanisa hadi kuwa shahidi wa injili ya Kristo. Kanisa, kama ilivyokuwa jumuiya ya mitume kwa Saulo, liko daima mikono wazi kuwapokea wanawe wapotevu wanaoguswa na kuiitikia neema ya wongofu na kwa namna ya pekee, kanisa na jumuiya nzima ya waamini linaalikwa kusali na kuomba neema hii ya wongofu katika maeneo ambapo linateseka mojakwamoja kimfumo na katika hali ambapo linazuiwa kutekeleza utume wake kama lilivyokabidhiwa na Kristo mwenyewe.

Somo la Pili (1Yoh. 3:18-24) mtume Yohane anazungumza juu ya upendo wa kindugu na namna mkristo anavyoalikwa kuuishi upendo huo katika jumuiya. Anaasa kuwa upendo si maneno bali upendo ni matendo “tusipende kwa neno wala kwa ulimi bali wa tendo na kweli”. Anaendelea kufafanua kuwa upendo huu unapaswa kujengwa kutoka moyo uliotulizwa mbele ya Mungu. Kwa Mtume Yohane, Mungu ni Upendo. Na hivyo upendo kati ya mwanadamu na mwanadamu unapaswa kuwa ni ule unaotoka katika chemchemi hiyo ya upendo wa Mungu. Nje ya hapo utakuwa ni upendo wa maneno tu au kama anavyouita, upendo wa ulimi. Ni moyo uliotulizwa mbele ya Mungu ulio na dhamiri hai, dhamiri  inayotajwa kuwa “ni taa ya Bwana inayopeleleza yote yaliyomo ndani ya mtu  (Rej. Mith. 20:27). Ndiyo inayokuwa kipimo na dira katika maisha ya mwanadamu.

Injili (Yoh.15:1-8): Katika injili ya leo, Yesu, ili kutoa fundisho lingine kubwa, anajifananisha na alama ambayo ina nafasi katika hadhira ya kiyahudi. Alama hiyo ni Mzabibu. wayahudi walikuwa wakulima wa mizabibu lakini pia waliupa mzabibu alama mbalimbali katika imani na katika uhusiano wao na Mungu. Mzabibu ulifananishwa na hekima (Rej. Sir. 24:17), shamba la mzabibu katika Isa. 5:1-7 liliashiria nyumba ya Israeli, yaani waana wa Mungu na katika Yer. 2:21 na Eze. 19:10-14 mzabibu unatumika kama alama ya kuelezea mahusiano kati ya Mungu na waisraeli ambapo mwenyezi Mungu ameuhudumia lakini si mara zote mzabibu huo umetoa matunda tarajiwa.

Yesu anatumia alama ya mzabibu sio kwa kutaka kujieleza kuwa ndiye Israeli ya kweli bali kutaka kukazia uhusiano wake na Mungu Baba na pia uhusiano wake na wafuasi wake. Anasema yeye ndiye mzabibu wa kweli na Baba ndiye mkulima. Baba ndiye chanzo, ndiye asili na ndiye mkuu na Yesu anaukiri ukuu huo. Yeye mwenyewe anabaki ameungana na Baba na kama mzabibu unavyomtegemea mkulima ndivyo na utume wake katika yote aliyokuja kuyafanya duniani yanavyomtegemea Baba na yanavyopata asili kutoka kwa Baba. Kutoka katika muungano huu na Baba, Yesu anatoa fundisho lingine kuwa wafuasi wake nao wanapaswa kuungana naye kama matawi ya mzabibu yanavyoungana na mzabibu kwa ustawi wao na kwa kuzaa matunda. Kumbe Yesu ndiye Mzabibu wa kweli kwa sababu ameungana kabisa na Baba. Vivyo hivyo wafuasi wake wanakuwa wafuasi kweli kwa namna wanavyoungana naye, ndio kuliweka ndani yao Neno lake.

Tafakari fupi: Maandiko Matakatifu katika dominika hii yanatualika kutafakari juu ya umoja katika wafuasi wa Kristo: umoja na Mungu na umoja kati ya wafuasi wao kwa wao. Katika hatua ya kwanza kama wafuasi tunaalikwa kutambua kuwa uhai wetu, uhai wa imani yetu na mantiki ya sisi kuwa wafuasi wa Kristo ni kuungana na Kristo. Nje ya muungano huo sisi sio kitu na yote yanayoendelea nje ya muungano huo ni bure. Muugano huu ni muhimu kiasi ambacho nje yake hatuwezi kufanya chochote. Mtakatifu Thoma wa Akwino anasema - Yesu hakutuambia kuwa “pasipo mimi mtaweza kufanya kidogo au pasipo mimi hamtapata matunda mengi” bali anasema waziwazi “pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lolote”. Ni mwaliko wa kuyaangalia maisha yetu kama wafuasi, si katika matokeo ya kile tunachofanya bali katika chimbuko la kile tunachofanya. Katika utume ambao Mungu amempa kila mmoja wetu kadiri ya wito wake na kadiri ya hali ya maisha aliyoitikia, na hata katika utume wa kanisa kwa ujumla tunaalikwa pia kulitazama hili. Kwamba utume wetu usukumwe kwanza na chimbuko thabiti ambalo ni Kristo na matakwa yake badala ya kuvutwa na matokeo ya kile kinachofanyika kadiri ya mwono wa wapokeaji au watazamaji.

Umoja na Kristo ni mwaliko pia wa kuishi umoja wa kindugu. Tunapoyafumbua macho na kuangalia jamii tuliyomo, tunaona waziwazi kuwa umoja unakuwa ni changamoto. Tunakabiliwa na changamoto hii ya umoja katika familia zetu, katika taasisi zetu na katika jamii kwa ujumla. Na hata tunapoiangalia nchi yetu katika ujumla wake, tunakiri kuwa msingi huu wa umoja unatikiswa na unatikisika. Ni nini chanzo au vyanzo? Ni wapi tulipokosea? Tutaendelea hivi hadi lini? Na ni nini au ni wapi yalipo matumaini yetu?  Hekima ya kawaida hutukumbusha kuwa ili kuvuka kizingiti na kuendelea ni muhimu kuangalia pale unapojikwaa. Ni muhimu kurudi pale tulipokosea, pale tulipokiuka misingi inayolinda na kutunza umoja na kwa unyenyekevu kurudi katika misingi hiyo.

Somo la pili linatualika tuuangalie upendo kama msingi muhimu ya kukuza umoja kati ya waamini. Mtume Yohane anatofautisha upendo wa neno au wa ulimi na upendo wa tendo na kweli. Na ni kama anaweka mbele yetu kioo cha upendo katika kutazama changamoto ya umoja katika jamii zetu na kutaka tujihukumu wenyewe juu ya upendo tulionao kama ni ule wa maneno na ulimi hali mioyo yetu ikiwa mbali na yale tusemayo mbele ya watu au ni upendo wa kweli unaomaanisha kile maneno yetu yasemayo. Kristo mzabibu wa kweli aliyeungana kabisa na Baba aliye Mkulima na kutualika nasi tuungane naye awe nguvu na msaada wetu, tunapojitahidi kuishi tukiwa tumeungana naye na tukiwa tumeungana na wenzetu kwa upendo wa kindugu.

Padre William Bahitwa.

VATICAN NEWS.
All the contents on this site are copyrighted ©.