2018-04-28 15:17:00

Papa Francisko: Wakristo dumisheni ushirikiano na mshikamano


Mkutano wa Jukwaa la Tatu la Wakristo Duniani kuanzia tarehe 24-27 Aprili 2018, imekuwa ni fursa ya kutafakari na kujadili masuala mbali mbali yanayogusa maendeleo ya mtu mzima: kiroho na kimwili katika mwanga wa Injili ya Kristo! Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa wajumbe wa mkutano huu amekazia kwa namna ya pekee kabisa umuhimu wa kukuza na kudumisha mshikamano na ushirikiano kati ya watu wa Mataifa kama sehemu ya mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu! Wakristo wakiwa wameungana na kushikamana barabara wanaweza kukabiliana kwa dhati kabisa na changamoto mamboleo, huku wakiendelea kujikita katika mchakato wa mageuzi na upyaisho!

Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo kwa baraka zake, ambazo zimewawezesha Wakristo kutoka katika Makanisa na Jumuiya mbali mbali za Kikristo kukutana kama ndugu, kama sehemu ya utekelezaji wa ile sala ya Kristo Kuhani mkuu, “ili wote wawe wamoja, ili dunia iweze kuamini”. Baba Mtakatifu ameombea mafanikio kwa ajili ya mkutano huu, ili kweli uweze kuwa ni jukwaa la kushirikishana tunu bora za maisha ya kiroho na kiimani kutoka kwa waamini na viongozi wa Kanisa; kwa kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu wamoja katika Kristo Yesu. Baba Mtakatifu anaendelea kukaza kwa kusema, familia ya binadamu ina kiu kubwa sana ya kuona kwamba, mshikamano na ushirikiano huu unajengeka na kudumishwa, ili kuhamasisha mchakato wa kuheshimiana, kuthaminiana; kusameheana, tayari kuunganisha nguvu ili kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu katika hatua na mazingira mbali mbali ya maisha yake!

Askofu Brian Ferrel, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo katika hotuba yake elekezi, amekazia umuhimu wa kukuza na kudumisha majadiliano ya kiekuemene miongoni mwa Wakristo wa Makanisa na Madhehebu mbali mbali, ili kujenga na kudumisha uekumene wa huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwa kutambua kwamba, umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu. Kanisa Katoliki linapaswa kuheshimu na kuthamini changamoto mpya zinazotolesa na Makanisa ya Kipentekoste katika mwanga wa karama, badala ya kuendelea kukazia zaidi na zaidi: Mapokeo ya Kanisa, Sheria Kanuni za Kanisa!

Kumbe, kanuni maadili na utu wema mintarafu mwanga wa Injili ni mambo yanayopaswa kuvaliwa njuga na Wakristo wote. Hii ni changamoto kwa viongozi na waamini wa Makanisa ya Kikristo kuhakikisha kwamba, wanajifunza zaidi taalimungu ili kufahamu Maandiko Matakatifu yanayopaswa kuwa ni dira na mwongozo wa maisha ya Wakristo. Kutofahamu vyema Maandiko Matakatifu ni hatari kwani kunaweza kuibua waamini wenye misimamo mikali ya kidini na kiimani. Makanisa na Jumuiya za Kikristo ziepuke tabia ya wongofu wa shuruti unaojikita katika imani ya miujiza, mafanikio ya chapu chapu bila kutokwa jasho. Kimsinhi, Wakristo wote wamepokea Ubatizo mmoja kwa maondoleo ya dhambi na maisha ya uzima wa milele. Umefika wakati kwa Makanisa na Jumuiya ya Kikristo kuendelea kujizatiti kikamilifu katika misingi na kweli za Kiinjili mintarafu mwanga na maongozi ya Roho Mtakatifu.

Daima, Wakristo wakumbuke kwamba, wanayo imani na ubatizo mmoja. Kumbe, Wakristo washirikishane karama, uzoefu na mang’amuzi yao ya maisha ili kukuza na kudumisha utamaduni wa: Kusoma na kutafakari Maandiko Matakatifu; Kusali na kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa mahalia; mambo ambayo yanaweza kufanywa kwa pamoja na Wakristo sehemu mbali mbali za dunia. Askofu Brian Ferrel, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo anasema, maadhimisho ya mkutano huu yataweza kuzaa matunda yanayokusudiwa, ikiwa kama Wakristo katika maisha yao, watathubutu kujenga mshikamano na kukuza ushirikiano katika huduma, kama kielelezo cha ushuhuda wa mambo msingi yanayowaunganisha kama Wakristo, ili taratibu kuanza kuondokana na yale yanayowafifisha, kuwagawa na hatimaye, kuwasambaratisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.
All the contents on this site are copyrighted ©.