2018-04-28 14:55:00

Mtakatifu Yohane Paulo II: Urithi, amana na utume wake!


Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican ulikuwa ni dira na mwongozo wa maisha na utume wa Mtakatifu Yohane Paulo II kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, daima binadamu na mahitaji yake msingi, ndicho alichopenda kuona kwamba, kinavaliwa njuga na Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo! Hiki ndicho kiini cha ujumbe ulioandikwa hivi karibuni na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa washiriki wa mkutano wa kimataifa ulioandaliwa Chuo Kikuu cha Kipapa cha Mtakatifu Thoma wa Akwino, kilichoko mjini Roma kwa kushirikiana na Ubalozi wa Poland mjini Vatican, kama kumbu kumbu endelevu ya miaka 40 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican ni neema kubwa sana ambayo Mwenyezi Mungu amelijalia Kanisa lake. Neema hii ikamwilishwa katika maisha na utume wa Kanisa kwa njia ya Mtakatifu Yohane Paulo II aliyetangaza na kushuhudia amana na utajiri wa Mafundisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican katika maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo. Binadamu na mahitaji yake msingi, alipewa kipaumbele cha pekee kabisa katika maisha na utume wa Kanisa.

Mtakatifu Yohane Paulo II aliweza kufanya hija za kitume 104 nje ya Italia. Akabarikiwa kufanya hija za kichungaji 142 nchini Italia, daima maneno yake yaliambatana na vitendo; akagusa na kufariji mamilioni ya watu duniani, huku akitangaza na kushuhudia uhuru wa kidini na uhuru wa kuabudu kama kiini cha haki msingi za binadamu! Matokeo yake ni kuanguka kwa Ukuta wa Berlin kunako mwaka 1989. Kanisa likatoka kidedea na kusimama kifua mbele ili kupinga sera za kibaguzi zilizoigawa dunia, kati ya Kaskazini na Kusini: likaimarisha tunu msingi za maisha ya Kikristo, kwa kujikita katika haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi kama kanuni msingi za Mafundisho Jamii ya Kanisa.

Mtakatifu Yohane Paulo II kwa kufuata dira na mwongozo wa Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, akaimarisha mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene; kiasi hata cha kujiweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Ni kiongozi aliyetambua na kuthamini sana mchango wa wanawake katika ustawi na maendeleo ya jamii na Kanisa katika ujumla wake, mambo yanayojionesha hata katika Nyaraka zake za kichungaji “Muliris dignitatem” yaani “Utu wa mwanamke”. Alikazia sana umuhimu wa utakatifu wa maisha ya Kikristo kama kielelezo cha uaminifu kwa Kristo na Kanisa lake, kiasi cha kuthubutu kuwatangaza watakatifu wapya 482 na wenyeheri 1319, mwaliko na changamoto ya kumfuasa Kristo Yesu kama chemchemi ya utakatifu na utimilifu wa maisha ya Kikristo.

Mtakatifu Yohane Pualo II, alikuwa na karama ya pekee katika maisha na utume wa Kanisa kwa vijana, kwani hawa kwake walikuwa ni jeuri na matumaini ya Kanisa na jamii katika ujumla wake, utume ambao unaendelea kutekelezwa na Mama Kanisa hata nyakati hizi. Katika maisha na utume wake, aligusa medani mbali mbali za maisha ya binadamu; akaimarisha mafundisho msingi ya Kanisa yanayofumbatwa katika huruma ya Mungu, Roho Mtakatifu, Uhusiano kati ya imani na akili; Ari na mwamko wa kimisionari ndani ya Kanisa.

Mtakatifu Yohane Paulo II, hata dakika zake za mwisho katika udhaifu wa mwili na magonjwa, akaendelea kuwa ni shuhuda, nabii na chombo cha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Akafanikiwa kuonesha ukuu, utakatifu, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kardinali Pietro Parolin anahitimisha ujumbe wake kwa washiriki wa mkutano huu wa kimataifa juu ya kumbu kumbu endelevu ya miaka 40 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki kwa kumshukuru Balozi Janusz Kotansk, waandaaji pamoja na washiriki wote kwa kumuenzi kwa dhati kabisa Mtakatifu Yohane Paulo II, kama kioo cha utekelezaji wa Mafundisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican katika maisha na utume wa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.