2018-04-28 14:15:00

Mpango mkakati wa maboresho ya afya ya umma unapaswa kuwa shirikishi


Baraza la Kipapa la Utamaduni kwa kushirikiana kwa karibu sana na Mfuko wa “Unite To Cure”, pamoja na wadau wengine, kuanzia tarehe 26-28 Aprili 2018, kwa pamoja wameadhimisha mkutano wa nne kimataifa mjini Vatican, uliojikita katika mchakato wa maendeleo ya sayansi na teknolojia inayopania kuboresha afya ya binadamu; kuzuia na kuponya magonjwa; kulinda na kudumisha mazingira bora kwa kuzingatia tamaduni, tunu msingi za maisha ya kiroho na athari zake katika jamii husika! Kauli mbiu ya mkutano huu imekuwa ni “Mpango mkakati wa maboresho ya huduma ya afya duniani”. Hili ni jukwaa la sayansi na teknolojia kwa ajili ya maboresho ya huduma ya afya  ambalo limewashirikisha wadau mbali mbali, kama vile: wataalam wa afya, watunga sera na mikakati ya huduma ya afya pamoja na ushuhuda kutoka kwa wagonjwa wenyewe, ili kwa pamoja waweze kuibua mbinu mkakati utakaosaidia mchakato wa maboresho ya afya duniani. Lengo ni kulinda na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake alipokutana na washiriki wa mkutano huu wa kimataifa, Jumamosi, tarehe 28 Aprili 2018 amesema, tema zilizodadavuliwa na wajumbe zimeweka msingi wa tafakari za kinadharia ambazo zinaonesha dira na njia inayopaswa kufuatwa na wadau mbali mbali, kwani ubinadamu ni mahali muafaka pa kuwakutanisha watu. Katika shida, mahangaiko na magonjwa ya mwanadamu ni vyema kujenga muafaka kati ya watu na taasisi, hata ikiwezekana kuvuka vikwazo vya maamuzi mbele ili hatimaye, kuweza kuunganisha nguvu kwa ajili ya kumsaidia mgonjwa.

Baba Mtakatifu katika hotuba yake amekazia mambo manne: Kukinga, Kurekebisha, Kutibu na Kujiandaa kwa siku za usoni. Baba Mtakatifu anakaza kusema, magonja na shida nyingi zinazomwandama mwanadamu zingeweza kuepukika, ikiwa kama watu wangekuwa na mfumo na utaratibu mzuri wa maisha na tamaduni wanamoishi. Kumbe, kinga ingelenga zaidi kukuza na kudumisha utu wa binadamu pamoja na mazingira anamoishi kwa kuweka uwiano mzuri wa elimu, mazoezi ya viungo, lishe pamoja na utunzaji bora wa mazingira, bila kusahau kutekeleza kwa dhati “sheria kanuni za afya bora” ambazo zinapata chimbuko lake katika maisha ya kiroho, tafiti na chunguzi za magonjwa. Mambo yote haya yangeweza kumsaidia mwanadamu kuishi vizuri zaidi.

Hii inatokana na ukweli kwamba, kuna magonjwa ambayo yanasababishwa na mazingira pamoja na tamaduni mamboleo; baadhi yao ni ulevi, uvutaji wa sigara, uchafuzi wa hewa, maji na ardhi. Magonjwa mengi ya Saratani yangeweza kuepukika ukubwani, ikiwa kama kungekuwepo na sera na mikakati ya kukinga, dhamana na wajibu unaopaswa kutekelezwa na wote! Kumbe, kuna haja ya kujenga na kudumisha utamaduni wa kinga kama hatua ya kwanza ya kudumisha afya bora! Baba Mtakatifu anapongeza juhudi na jitihada ambazo hadi sasa zimefikiwa katika maendeleo ya sayansi ya tiba ya mwanadamu, hasa kwa kuzingatia magonjwa hadimu, chanjo pamoja na magonjwa yanayoshambulia seli za binadamu. Sayansi imeweza kukinga na kurekebisha seli zinazoshambulia magonjwa haya. Ili kupata ufanisi mkubwa zaidi kuna haja ya kuendelea kuwekeza katika tafiti, jambo muhimu sana katika maendeleo ya sayansi na utu wa binadamu.

Sayansi na mazingira yanategemeana na kukamilishana na kwamba, maendeleo ya sayansi na teknolojia yanasaidia kwa kiasi kikubwa maboresho ya afya kiasi hata cha kubadili vinasaba vya watu. Pamoja na maendeleo yote haya ya sayansi na teknolojia, Mama Kanisa anapenda kukazia utu, sheria na kanuni maadili; kwa kutambua uwezo na mapungufu ya sayansi na kwamba, kipimo cha maendeleo ni ustawi, mafao ya wengi na kwa ajili ya mtu mzima: kiroho na kimwili!

Baba Mtakatifu anaendelea kudadavua kwa kusema kwamba ili kuandaa kesho iliyo bora zaidi, kuna haja ya kuhakikisha ustawi wa binadamu unaoweza kuathiriwa kutokana na nguvu kubwa ya maendeleo ya sayansi na teknolojia. Hapa kuna haja ya kusimama kidete dhidi ya utamaduni wa kifo, kwa kulinda na kutunza mazingira, kwa kutoa kipaumbele kwa mahitaji ya watu, lakini zaidi maskini na wale wanaoishi katika mazingira magumu na tete kiasi hata cha kuhatarisha afya zao bila hata kuwa na uhakika wa tiba bora zaidi. Baba Mtakatifu anakaza kusema, ili kuweza kujiandaa vyema kwa siku za usoni kuna haja kwa wataalam na taasisi mbali mbali kushirikiana kwa karibu zaidi, ili kubadilishana uzoefu, ujuzi na mang’amuzi na pili ni kuhakikisha kwamba, hata maendeleo ya sayansi na teknolojia, yanatoa kipaumbele cha kwanza kwa wagonjwa na maskini. Mchakato huu uwashirikishe: wanasayansi na waganga; wagonjwa na familia zao; wasomi na wana maadili; viongozi wa kidini na wanaharakati; viongozi wa serikali na wafanyabiashara; ili yote yawe ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.