2018-04-27 07:08:00

Viongozi wa Makanisa kukutana ili kusali na kutafakari huko Bari!


Makanisa ya Kikristo yameamua kujikita zaidi katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika umoja unaoonekana, ushuhuda wenye mvuto na mashiko katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu sanjari na kukabiliana na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu mamboleo! Baba Mtakatifu Francisko anasema, huu ndio uekumene wa damu, maisha ya kiroho, sala na huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii! Lengo kuu ni kuwawezesha Wakristo wote kuwa wamoja kama jibu msingi la Sala ya Kristo pamoja na kusaidia kukoleza mchakato wa amani ing’aayo kutoka katika Uso wa Mungu.

Wakristo wanapaswa kuwa ni mashuhuda, vyombo na manabii wa amani duniani. Migawanyiko miongoni mwa Wakristo ni kikwazo kikubwa katika ushuhuda wa pamoja miongoni mwa Wakristo! Changamoto kubwa iliyoko mbele ya Wakristo katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo ni kuchuchumilia mambo msingi yanayowaunganisha Wakristo kuliko yale yanayoendelea kuwagawa na kuwasambaratisha, anasema Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume, “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili”. Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, amekuwa akitoa kipaumbele cha pekee katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene miongoni mwa wafuasi wa Kristo Yesu! Dr. Greg Burke, Msemaji mkuu wa Vatican anasema, Baba Mtakatifu Francisko tarehe 7 Julai 2018 atatembelea Kanisa kuu la Mtakatifu Nicholaus wa Bari, ili kusali na kutafakari juu ya mateso na mahangaiko ya Wakristo huko Mashariki ya Kati. Hawa ni waamini wanaolazimika kuyakimbia makazi na nchi yao kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.

Baba Mtakatifu ameonesha pia nia ya kuwaalika pia viongozi wakuu wa Makanisa na Jumuiya za Kikristo kuungana pamoja naye katika tukio hili muhimu! Anawaomba Wakristo sehemu mbali mbali za dunia, kushiriki katika maandalizi haya kwa njia ya sala na sadaka zao! Jumuiya ya Mtakatifu Egidio yenye makao yake makuu mjini Roma, imepokea mwaliko huu kwa imani na matumaini kama kielelezo cha ushuhuda wa mshikamano na Wakristo huko Mashariki ya Kati, wanaoendelea kuteseka kutokana na vita, kinzani mbali mbali za kijamii, kisiasa na kidini!

Hivi karibuni, Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo alisikika akisema, watakatifu na wafiadini ni vielelezo na mifano bora ya kuigwa katika maisha na maombezi yao. Wanaonesha dira na mwongozo wa kufuata katika maisha kama wafuasi wa Kristo Yesu. Kwa mifano na maombezi yao, wanawasaidia waamini katika mchakato wa kuwa watakatifu, kama kielelezo cha kutangaza na kushuhudia: ukuu, uweza na utakatifu wa Mungu. Kwa kuwaheshimu watakatifu, waamini wanamtukuza na kumwabudu Mwenyezi Mungu katika utakatifu wake, ambao umemwezesha kuwatembelea na kuwatakatifuza waja wake. Kimsingi, watakatifu ni mng’ao wa utukufu wa Mungu.

Ibada ya kuheshimu masalia ya Mtakatifu Nicholaus wa Bari  yanayohifadhiwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Nicholaus wa Bari, Jimbo kuu la Bari-Bintonto, Italia, inayotekelezwa na Wakristo ambao bado wamegawanyika ni changamoto ya kumwomba asaidie kuganga na kuponya kashfa ya utengano kati ya Wakristo wa Makanisa ya Mashariki na Magharibi. Kwa waamini wa Makanisa haya mawili kuendelea kuonesha Ibada kwa watakatifu hawa ni kielelezo cha utashi wa watu wa Mungu kutaka kuungana tena ili kukuza na kudumisha umoja, ushuhuda na huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.