2018-04-27 07:33:00

Papa Francisko apitisha Katiba Mpya ya Utume wa Sala duniani


Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kushiriki kikamilifu katika Mtandao wa Utume wa Sala, ili kuliwezesha Kanisa kukabiliana na changamoto mbali mbali za maisha na utume wake, daima likisoma alama za nyakati na kujibu kilio cha watu wa Mungu mintarafu mwanga na kweli za Kiinjili. Baba Mtakatifu tarehe 27 Machi 2018 ameidhinisha Katiba Mpya ya Mtandao wa Utume wa Sala kama sehemu ya utume wa Kipapa na makao yake makuu yatakuwa kwenye Sekretarieti kuu ya Vatican.

Taarifa hii imetolewa kwa barua iliyoandikwa tarehe 10 Aprili 2018 na Askofu Mkuu Giovanni Angelo Becciu, Katibu mkuu msaidizi wa Vatican kwenda kwa Shirika la Wayesuit ambalo kadiri ya mapokeo limekuwa likiratibu “Utume wa Sala” kwa kuandaa na kusambaza nia za Baba Mtakatifu kwa kila mwezi. Taarifa hii inahitimisha mchakato mzima wa mapitio na marekebisho yaliyoanza kufanyiwa kazi baada ya Baba Mtakatifu Francisko kumteua Mheshimiwa Frederic Fornos kuwa Mkurugenzi wa Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa. Utume wa Sala umeenea katika nchi 98 duniani na unashirikiana kwa karibu sana na Chama cha Kitume cha Vijana wa Ekaristi. Mtandao wa Utume wa Sala pamoja na mambo mengine unajihusisha kikamilifu katika kuandaa picha za video zinazosindikiza nia za Baba Mtakatifu kwa kila mwezi (www.ilvideodelpapa.org) pamoja na Jukwaa la Sala kwa ajili ya utume wa Kanisa (www.clicktopray.org).

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.