2018-04-27 15:06:00

Mwenyeheri Hanna Chrzanowska, mwamini mlei na muuguzi


Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wa Kitume “Gaudete et exsultate” yaani “Furahini na kushangilia, wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo” (Mt. 5:12) anasema, utakatifu ni hija ya mapambano dhidi ya dhambi kwa kuendelea kupyaisha ile neema ya utakaso ambayo waamini wameipokea katika Sakramenti ya Ubatizo! Utakatifu unawawezesha waamini kuguswa na mahangaiko ya jirani zao, kwa kutambua na kuthamini utu na heshima yao kama watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Waamini wanaitwa kuwa watakatifu kwa sababu Mwenyezi Mungu ni Mtakatifu na ni kiini na utimilifu wa utakatifu wenyewe. Utakatifu ni changamoto inayopaswa kupaliliwa kila kukicha na kamwe haitoshi kuwa Mkristo na mwamini kuanza kubweteka, bali daima ajitahidi kushiriki katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika haki, amani, upendo na mshikamano unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu! Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanapozungumzia kuhusu Fumbo la Kanisa wanakazia umuhimu wa waamini kushiriki kikamilifu katika Sakramenti za Kanisa. Wanasema waamini kwa kuimarika na misaada mingi ya wokovu namna hii na ya ajabu, waamini wote wa kila hali na hadhi wanaitwa na Kristo Yesu kila mmoja kwa njia yake, kwenye ukamilifu wa utakatifu kama Mwenyezi Mungu alivyo mtakatifu!

Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu, Jumamosi, tarehe 28 Aprili 2018 kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, anamtangaza Mtumishi wa Mungu Hanna Chrzanowska kuwa Mwenyeheri, kwenye Madhabahu ya Huruma ya Mungu, Jimbo kuu la Cracovia, nchini Poland. Mwenyeheri Hanna Chrzanowska alizaliwa tarehe 7 Oktoba 1902, akabahatika kupata masomo yake kutoka Chuo kikuu cha Jagiellonica, kilichoko nchini Poland. Ni muasisi wa Jarida la Wauguzi wa Poland” aliyeweka msingi wa Chama cha Kitume cha Wauguzi Wakatoliki nchini Poland, wanaoendelea kusimama kidete kulinda, kutetea, kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Alifariki dunia tarehe 29 Aprili 1973 huko Cracovia, huku akiwa anaimba utenzi wa Bikira Maria “Magnificat.”

Mwenyeheri Hanna Chrzanowska ni mwamini mlei, aliyechuchumilia utakatifu wa maisha kama sehemu ya amana na urithi kutoka kwa wazazi wake. Alibahatika kufundwa katika tunu msingi za maisha ya kiutu, kiroho na kimaadili; daima akaonesha heshima kwa watu wote, lakini zaidi kwa wagonjwa na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii, kiasi hata cha kuamua kusomea uuguzi ili aweze kuwa kweli msamaria mwema, akiwasaidia watu kuonja mateso yanayookoa kutoka katika Fumbo la Msalaba. Ni mwamini mlei aliyekuwa na Ibada kwa Bikira Maria Mfariji wa wagonjwa, akawaonesha watu mwanga wa maisha hata katika giza la mahangaiko na mateso yao. Ni mwamini ambaye katika umri wa miaka thelathini ya maisha yake, alikwisha palilia utakatifu wa maisha kwa njia ya sala, akajiaminisha kwenye karama ya Mtakatifu Benedikto, Abate ili kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya Sala ya Kanisa aliyojitahidi kuimwilisha kwa njia ya huduma kwa wagonjwa.

Mwenyeheri Hanna Chrzanowska aliguswa kwa namna ya pekee kabisa na Fumbo la Bikira Maria kumtembelea Elizabeth! Hapa Bikira Maria, alikuwa ni kielelezo cha Injili inayomwilishwa katika huduma kwa wahitaji zaidi. Hata wakati wa utawala wa Kikomunisti, Mwenyeheri Hanna alishuhudia imani yake kwa ari na moyo mkuu, akajinyenyekesha kama Msamaria mwema kuwaganga wagonjwa na maskini kwa mafuta ya faraja na divai ya matumaini iliyokuwa inabubujika kutoka kwa Kristo Yesu, Uso wa huruma ya Baba wa milele! Mwenyeheri Hanna Chrzanowska ni mfano bora wa kuigwa hata leo kwani bado kuna umati mkubwa wa wakimbizi na wahamiaji; wagonjwa, maskini na wazee; watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi wanaohitaji kuonjeshwa huruma na upendo kutoka kwa Wasamaria wema, vyombo, mashuhuda na manabii wa huruma ya Mungu kwa watu wa nyakati hizi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.