2018-04-27 15:49:00

Kumbukeni kwamba, Mimi ni Mzabibu nanyi ni matawi!


Upo mfano mmoja wa tai ambao nadhani ingefaa kutumika kama tafakari yetu Jumapili hii ya tano ya Kipindi cha Pasaka Kijana mmoja mhindi mwekundu huko Amerika ya Kaskazini – aliokota kwa bahati yai la tai na wazo alilolipata ni kuliatamisha kwa kuku. Yai likaanguliwa pamoja na kuku wengine na kukua na kuku wengine kama kawaida. Huyu tai aliishi maisha yake yote akidhani kuwa ni kuku na aliishi na kufanya yote sawasawa na kuku wa kawaida. Hata hakuweza kutumia mabaya yake yenye nguvu kuruka juu na mbali.

Sote twajua kuwa katika ulimwengu wa ndege, tai ndiye ndege mfalme. Miaka ikapita na tai huyu akaendelea kuzeeka. Siku moja akaona juu tena mbali ndege mzuri ajabu. Akasema, oh! ndege mzuri ajabu. Yule kuku akamwambia yule ni tai, mfalme wa ndege wote. Lakini kuku akamwambia inatosha usiwaze kuhusu hilo zaidi ya dakika mbili. Kweli hazikupita zaidi ya dakika mbili yule tai akafa kwa mshtuko. Pengine mfano huu utatusaidia kuingia katika tafakari yetu ya leo. Sisi ni matawi lakini matawi yahitaji mti, tena mti wenye mizizi na uhai barabara. Kwa kawaida matawi ni taswira halisi ya asilia ya mti husika, ya kiini cha mti. Katika maisha yetu yahitajika kubaki salama na vizuri katika mikono salama na tena kwa uaminifu mkubwa.

Mfano wa mzabibu kwa Waisraeli unaeleweka vizuri zaidi kwa sababu pia ni mojawapo ya mazao yao ya kudumu. Katika Agano la Kale – Zab. 80,8 – tunasoma, ulileta mzabibu toka Misri, ukawafukuza mataifa ukaupanda. Katika Isa. 5,7 – tunasoma, kwa maana shamba la mizabibu la Bwana wa majeshi ndilo nyumba ya Israeli, na watu wa Yuda ni mche wake wa kupendeza, akatumaini kuona hukumu ya haki, na kumbe aliona dhuluma, alitumaini kuona haki, na kumbe alisikia kilio. Katika Hosea 10,1 – tunasoma, Israeli ni mzabibu utoao matunda yake, kwa kadiri ya wingi wa matunda yake, kwa kadiri iyo hiyo ameongeza madhabahu zake, kwa kadiri ya wema wa nchi yake, kwa kadiri iyo hiyo wamefanya nguzo nzuri.  

Waisraeli walikuwa hata na sura ya tawi la mzabibu katika sarafu zao wakati wa utawala wa Makabayo. Kwa hiyo Yesu anapongea na kusema mimi ni mzabibu anaeleweka vizuri sana kwao. Mshikamano wa mti wa mzabibu ni kielelezo cha umoja na uhai. Cha pekee sana katika mfano huu wa leo ni kuwa Yesu anataka kuwatoa watu kutoka katika mtazamo ulioelekezwa kwa vitu na kuelekea kwa mtu, yaani Yesu Kristo mwenyewe. Tena anasema mimi ni mzabibu wa kweli.

Yule tai aliyeishi kama kuku na kufa kama kuku alipata mwanzo mbaya. Kwanza baada ya kutagwa aliachwa na ni kwa bahati tu aliokotwa na kuatamishwa kwa kuku. Alibaki kuwa tai lakini alipandikizwa kwenye mazingira yasiyokuwa yake au yasiyo sahihi. Badala ya kuishi kama tai akaishi kama kuku ingawa alikufa kama tai. Hakuishi uhalisia wake wa ndege tai. Mfano huu pengine utusaidie kuangalia jinsi tunavyouishi ukweli wetu katika maisha yetu - imani yetu inavyotufundisha na kututaka tuwe. Matengano yetu kama wanadamu hayana tena maana. Mtazamo wetu uwe wa umoja, watoto wa baba mmoja na mama mmoja – kielelezo sasa ni Kristo. Ni mwito unaotuita tutoke katika vifungo vya ubinafsi wa aina yo yote kifamilia, kiukoo, kijiji, kikabila, kitaifa na kuwa wamoja. Mti na shina ni mamoja. Hata katika maisha ya kawaida tunaalikwa kujua vizuri tushikamane na nani. Tukae na nani. Tufanye nini ili tukamilishe maisha yetu.

Katika somo I mstari wa mwisho – tema ya umoja iko wazi. Tema inaongelewa vizuri sana na Luka juu ya Paulo. Paulo alipoingia Yerusalemu aliogopwa na wote kwani walimjua kama mtesaji. Luka anasema wazi kuwa walishindwa kumkubali kama mtume na mfuasi wa Kristo. Twajiuliza – hivi lile kanisa changa lingemkataa kata kata ingekuwaje leo? Alipokelewa tu kwa sababu ilikuwepo jumuiya ya kanisa dogo. Jumuiya ya waamini. Simulizi la Barnaba pia linasaidia kutoa wasiwasi waliokuwa nao – Barnaba anaeleza barabara kile kilichotokea. Watu wakampokea. Bila wasiwasi Paulo anaanza kuhubiri habari ya Kristo. Ndiyo maana Luka anahitimisha akitaja amani na kukua. Wanapokutana pamoja, amani hupatikana na hukua na kukomaa pamoja.

Katika Agano la Kale taifa la Mungu linafananishwa mara nyingi na shamba la mizabibu. Katika Yer. 2:21 – tunasoma hivi – nami nalikuwa nimekupanda, mzabibu mwema sana, mbegu nzuri kabisa, umegeukaje, basi, kuwa mche usiofaa wa mzabibu mwitu machoni pangu? Hakika mzabibu huu ulipoteza dira na kusahau mshikano na haja na lazima ya kubaki pamoja na Bwana wake.

Katika somo la Injili tumesikia fundisho juu ya mzabibu. Katika maandiko matakatifu tunapata maandiko haya katika Injili tatu za kwanza Yesu akitumia kielelezo hicho kwa kuueleza Ufalme wa Mbinguni – Mt. 20:1-8; 21:28-31,33-44. Yesu anatumia uzao wa mzabibu kwa ajili ya Ekaristi Takatifu ya Agano Jipya – Mt. 26:29. Hapo Yesu anajiita mzabibu wa kweli, uzao wake utakuwa Taifa jipya teule, wala halitadanganya matumaini ya Mungu – Yoh. 15;1-17. Taifa jipya hilo litaishi katika uzima wa imani na mapendo kwa sababu wanaishi katika Kristo.

Ndugu zangu, watu wanapokutana pamoja, hutokea jambo. Hii ni kanuni mojawapo kuu ya sosholojia. Hata katika tasaufi – spirituality. Ni katika umoja, makuzi yanatokea, uhai hupatikana. Ukiota peke yako hubaki ndoto, jumuiya ikiota pamoja ukweli hutokea. Umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu. Umoja katika jumuiya huzaa matunda. Katika Agano Jipya – Mdo ya Mitume – msisitizo huu uko wazi zaidi kuliko katika sehemu nyingine yo yote ya Maandiko Matakatifu. Umoja huu unaelezwa na falsafa ya moyo mmoja na roho moja – Mdo. 4,32. Matokeo yake ni kuongezeka kwa jamii, kukua – Mdo. 2,42. Makutano yao, yanazaa jumuiya inayoongezeka.

Sifa za makuzi haya zinaonekana wazi pia katika sehemu nyingine za maandiko Matakatifu: Yoh. 14:23 – Yesu akajibu akamwambia, mtu akinipenda, atalishika neno langu na baba yangu atampenda, nasi tutakuja kwake, na kufanya makao kwake. Palipo na upendo na mapendo mimi nipo kati yao. Hitaji mojawapo la kikundi cho chote chenye mshikamano ni upendo. Yoh. 17: 21 – wote wawe na umoja, kama wewe, baba ulivyo ndani yangu nami ndani yako, hao nao wawe ndani yetu, ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma. Mfano mzuri wa kuigwa wa umoja ni utatu mtakatifu. Mtakatifu Yohani wa Msalaba anasema – Roho iliyoungana na Mungu, huogopwa na shetani kama vile angekuwa Mungu mwenyewe.

Katika Injili – umoja huu na kukua huko kunaelezwa katika mzabibu na matawi. Ili sisi tuwe na umoja kati yetu ni lazima tubaki na Kristo. Kinyume chake umoja wetu hautadumu. Tukiwa ndani yake, tupo pia pamoja. Sisi pamoja, ndani yake, tutazaa matunda. Kitokeacho wakristo wakiwa na umoja kiko wazi somo la pili – upendo, ukweli na amani hutokea.

Kadiri ya Yohane, Mungu huhusiana nasi kwa njia ya mapendo. Mapendo hayo ya kimungu huonekana wazi kwetu tukipendana sisi kwa sisi. Wakristo wakikaa pamoja, mapendo hutawala na uhai wa kimungu hupatikana. Yohani anaendelea kusema – ukweli huweka wazi Neno la Mungu ambalo hufanya kazi ndani yetu. Ukweli huwepo tukiungama Neno la Mungu. Ukweli ni kielelezo cha umoja wetu katika Kristo. Kadiri ya Yohane pia, amani ni tunda la ushindi wa Kristo dhidi ya ulimwengu. Huondoa tabaka kati yetu na Baba, huondoa matengano na mifarakano katika jumuiya. Ni ujumla wa uwepo wetu binafsi na jumuiya katika Kristo. Wakristo wakikaa pamoja – Kristo yupo kati yao. Katika mwaliko wa Neno la Mungu siku ya leo tunaalikwa kutambua hilo. Kutambua kuwa Yesu ndiye mzabibu wa kweli. Uhai wa kweli na uzima upo ndani yake.

Kutambua sifa mbalimbali zinazoleta uhai huo na umoja huo katika Kristo. Upendo, ukweli na amani. Katika somo Yesu anatumia mfano wa mzabibu kwa kueleza kwamba Waisraeli wasio waaminifu hawastahili kuhusiana na mzabibu wa Mungu; watu wengine wataaminishwa shamba hilo la mizabibu, nao ni watu wa mataifa, yaani wapagani – Mt. 21:33-44, ikiwa walioaminishwa watapoteza ufahamu huo. Habari juu ya vibarua wa shamba wasio waaminifu – Yesu anatumia kielelezo cha shamba la mizabibu kuelezea ufalme wa Mungu – Mt. 20,1-8.

Ndugu yangu mpendwa, Je, wewe na mimi ni matawi mema katika mti wa uhai yaani Yesu Kristo? Je wewe na mimi ni tawi linalozaa au hapana? Kama mkristo wewe ni tawi lenye uhai? Uwepo wako katika familia, jumuiya, parokia ukoje? Ni kupe?  Yesu anajiita mzabibu wa kweli, uzao wake utakuwa Taifa jipya teule, wala halitadanganya matumaini ya Mungu – Yoh. 15;1-17. Taifa jipya hilo litaishi katika uzima wa imani na mapendo kwa sababu wanaishi katika Kristo. Bila shaka hii ndiyo namna ya kuishi Injili leo hii – kuwa taifa jipya, lenye imani na mapendo kwa sababu linaishi katika Kristo.

Tumsifu Yesu Kristo.

Padre Reginald Mrosso, C.PP.S.

 
All the contents on this site are copyrighted ©.