2018-04-27 14:47:00

Kristo Yesu anaendelea kuwaombea waja wake hata huko mbinguni!


Mama Kanisa anafundisha kwamba wanaokufa katika neema na urafiki na Mwenyezi Mungu, na waliotakaswa kikamilifu wanaishi kwa daima pamoja na Kristo Yesu. Hawa wanafanana na Mwenyezi Mungu daima, kwa sababu wanamwona “kama alivyo,” uso kwa uso. Ukamilifu wa maisha haya pamoja na Utatu Mtakatifu; ushirika wa uzima na mapendo pamoja na Fumbo la Utatu Mtakatifu, Bikira Maria na Malaika na wenye heri wote, huitwa mbingu. Mbingu ndiyo hatima ya mwisho ya mwanadamu na utimilifu wa matarajio yake ya ndani, furaha ya hali ya juu na ukamilifu wake. Kwa njia ya Fumbo la Pasaka, Kristo Yesu, amewafungulia waja wake mbingu!

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Ijumaa tarehe 27 Aprili 2018, amedadavua kwa kina mapana “dhana ya mbingu” kama mahali pa kukutana na Kristo Yesu, ili kufurahia maisha ya uzima wa milele. Waamini wamo kwenye uhakika wa safari ya kwenda mbinguni. Somo la kwanza kutoka katika Kitabu cha Matendo ya Mitume 13:26-33: linaloonesha utimilifu wa Fumbo la Pasaka yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo kutoka kwa wafu na kwamba, Mitume ni mashuhuda wa Kristo Mfufuka. Hii ni changamoto kubwa kwa waamini kuendelea kutembea katika ahadi ya Mungu, kwa kutambua kwamba, wao ni taifa teule, licha ya kukosa uaminifu mbele ya Mwenyezi Mungu, lakini Yeye alibaki daima mwaminifu kwa ahadi zake.

Baba Mtakatifu anawakumbusha waamini wote kwamba, wako njiani kuelekea mbingun, mahali ambapo wanatarajia kukutana na Kristo Yesu katika maisha uzima wa milele. Huko mbinguni, Yesu anaendelea kufanya kazi kwa ajili ya waja wake pamoja na kuwaombea mbele ya Baba yake wa mbinguni. Yesu ni njia, ukweli na uzima na hakuna awezaye kwenda kwa Baba yake pasi kupitia kwake na kwamba, nyumbani kwa Baba yake kuna makao mengi! Kumbe, Yesu anaendelea kusali na kuwaombea waja wake, kama alivyo mhakikishia Mtume Petro, Siku ile iliyotangulia kuteswa kwake. Kristo Yesu yuko mbinguni akiwaandalia makao, jambo ambalo linawapatia imani wafuasi wake, Yesu, Kuhani mkuu anaendelea kuwaombea waja wake hadi mwisho wa nyakati. Mwishoni mwa mahubiri yake, Baba Mtakatifu anawaalika wafuasi wa Kristo kuendelea kuwa na mang’amuzi haya katika maisha yao, kwa kutambua kwamba, Kristo anasali na kuwaombea daima mbele ya Baba yake wa mbinguni!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 
All the contents on this site are copyrighted ©.