2018-04-27 14:29:00

Dumisheni maisha ya kidugu na mwelekeo wa kijumuiya katika utume


Maadhimisho ya mkutano mkuu wa thelathini na mbili wa Shirika la Mtakatifu Gabrieli na familia ya Wamisionari wa Montforti ni fursa makini ya kumbu kumbu, kushukuru pamoja na kufanya rejea tena kwa mambo msingi ya maisha na utume wa Shirika. Huu ni muda muafaka wa kutafakari maisha ya Kijumuiya na changamoto zake, tayari kujenga utamaduni wa upendo duniani! Huu ni muhtasari wa mawazo makuu yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 27 Aprili 2018 alipokutana na kuzungumza na Wanashirika la Mtakatifu Gabrieli pamoja na familia ya Wamisionari wa Montforti wakati huu wanapoadhimisha mkutano wao mkuu wa Shirika unaoongozwa na kauli mbiu “Maisha ya kidugu na mwelekeo wa kijumuiya katika utume wa Wamisionari wa Montforti.”

Padre Gabriel Deshayes alilipatia Shirika dira na mwelekeo mpya kwa kujikita katika msingi wa Neno la Mungu linalopaswa kusomwa, kutafakariwa na hatimaye, kumwilishwa katika maisha. Hekima inayofumbatwa katika maisha ya Kikristo ni mwanga angavu uliomwongoza Mtakatifu Luigi Maria katika maisha na utume wake, kwa kuwaalika waamini kumsikiliza Mwenyezi Mungu na kujiweka chini ya ulinzi na tunza yake. Kwa kuzingatia na kuweka katika maisha ushauri wote huu, aliwasaidia watu kupambanua changamoto mbali mbali za maisha.

Baba Mtakatifu anasema, kauli mbiu “Maisha ya kidugu na mwelekeo wa kijumuiya katika utume wa Wamisionari wa Montforti” inalenga kuwajengea uwezo wanashirika kupambana na athari za ubinafsi, utandawazi usiokuwa na mashiko wala mvuto; ukosefu wa ufanisi pamoja na kukazia mambo yanayoonekana kwa nje peke yake. Wamisionari hawa wawashe moto wa Roho Mtakatifu na hekima ya Kikristo kama sehemu ya utajiri unaomiminika kutoka katika mafundisho ya Mtakatifu Luigi Maria, anayewafundisha namna ya kuwa na kuishi kikamilifu wito wao kama walimu, ili kuthamini maisha kama zawadi ya pekee kutoka kwa Mwenyezi Mungu ili hatimaye kukua na kufikia ukamilifu katika upendo.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, mambo haya yanamwilishwa kila siku katika sala, unyenyekevu kwa Roho Mtakatifu, uaminifu kwa Sheria kanuni za Shirika na upendo unaofanyiwa kazi, kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria! Baba Mtakatifu anawahamasisha wanashirika hawa kufuata nyayo za Bikira Maria pamoja na kudumisha maisha ya kidugu kama yanavyosimuliwa na kushuhudiwa kwenye Kitabu cha Matendo ya Mitume kwani yanamvuto na mguso mkubwa kwa watu wanaowazunguka. Wanashirika wakubali tofauti zao msingi, misimamo na mawazo yao pamoja na kuhakikisha kwamba, kinzani na migogoro ya maisha ya kijumuiya inatatuliwa kwa kuzingatia upendo na unyenyekevu.

Udugu uwahamasishe kujisahau wenyewe na hivyo kujiachilia mikononi mwa Roho Mtakatifu, ili kuimarisha maisha ya kijumuiya katika furaha na amani ya ndani, kwa kuwajali na kuwashughulikia jirani kwa upendo mkamilifu; daima majadiliano katika ukweli na uwazi yakipewa kipaumbele cha pekee ili kujenga umoja katika tofauti msingi. Umaskini wa maisha ya kiroho unawatumbukiza watawa wengi katika majonzi na masikitiko makubwa kiasi hata cha kupoteza maana ya maisha.

Ili kuvuka hali kama hizi, Baba Mtakatifu anawataka watawa kujenga jumuiya zinazosimikwa katika ukarimu ili kushuhudia ile furaha ya kuishi pamoja kama ndugu, ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa vijana wa kizazi kipya, wanaotaka kumfuata nyayo za Kristo Yesu katika maisha ya kipadre na kitawa. Watawa wajenge utamaduni wa kusikiliza kwa makini bila ya kuwa na maamuzi mbele; vijana watambuliwe na kuthaminiwa, ili waweze kushirikisha karama zao kwa ajili ya mafao ya wengi. Utamaduni wa upendo ni jibu muafaka katika ulimwengu wa utandawazi, kwa kuendelea kuwa mashuhuda wa utume katika sekta ya elimu, kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu ni hekima ya Mungu iliyomwilishwa, changamoto na mwaliko wa kujenga na kudumisha upendo na mshikamano na watu kutoka katika tamaduni na marika mbali mbali ya maisha.

Changamoto ya kutangaza, kushuhudia imani pamoja na maisha ya kijumuiya inaweza kukabiliwa kwa njia ya kipaji cha ubunifu kinachomwilishwa katika elimu makini, daima kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wao kikiwa ni maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hawa ni watu wanaopaswa kujengewa uwezo ili waweze kupambana na hali pamoja na mazingira yao. Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza na hatimaye anawataka kwenda mbali zaidi huku wakiwa na imani na ari mpya zaidi ya kimisionari inayorutubishwa kwa Fumbo la Pasaka. Mwishoni, amewaweka watawa wote hawa chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Kikao cha Hekima na hatimaye, kuwapatia baraka zake za kitume.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.