2018-04-26 15:19:00

Umuhimu wa Sakramenti ya Upatanisho katika maisha ya vijana!


Sakramenti ya Upatanisho ni muhimu sana katika safari ya maisha ya kiroho sanjari na mang’amuzi ya miito miongoni mwa vijana Wakristo. Ni katika Sakramenti ya Upatanisho, Mahakama ya huruma ya Mungu, mwamini anaonja huruma, upendo na msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu; ni mahali ambapo mwamini kutoka katika undani wake, anaguswa na kupyaishwa, huku akitiwa shime ya kusonga mbele katika hija ya maisha ya toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha. Hii ni Sakramenti inayopania kujenga na kudumisha mahusiano ya ndani kabisa na Mwenyezi Mungu.

  

Tema ya “Upatanisho” mintarafu mahusiano ya vijana katika nyanja mbali mbali za maisha ni muhimu sana wakati huu, Mama Kanisa anapojiandaa kwa ajili ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana yanayoongozwa na kauli mbiu “Vijana, imani na mang’amuzi ya miito.” Hii ni nafasi ya kudadavua hali ya kijamii na kitamaduni ambamo wanaishi vijana wa kizazi kipya, kwa kuangalia: vishawishi vya maisha ya ujana, changamoto na vikwazo wanavyopaswa kuviepuka katika maisha ya kiroho na kimwili; tayari kupokea kwa imani na matumaini changamoto za maisha ili kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, Bwana na Mwalimu katika uhalisia wa maisha yao!

Monsinyo Krzysztof Jòzef Nykiel hakimu wa Idara ya Toba ya Kitume anasema, Kanisa kama Mama na Mwalimu, anataka kuwasaidia vijana kusikiliza kwa makini kile ambacho Mama Kanisa anataka kuwafundisha, kung’amua na hatimaye, kumwilisha ushauri huu kama sehemu ya upya wa maisha yao katika miito yao mbali mbali. Mapadre waungamishaji ni waalimu na walezi wanaosaidia kufunda dhamiri nyofu, ili kuwa na mwelekeo chanya katika maisha, kwa kuonja: huruma, upendo na msamaha wa dhambi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, tayari kupiga moyo konde na kuanza kumfuasa Kristo Yesu, hatua kwa hatua katika maisha!

Mama Kanisa anapenda kuwachangamotisha vijana kujitosa kimasomaso ili kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Watoa mada wanaangalia changamoto za shughuli za kichungaji zinazoweza kuwakwamisha vijana kukimbilia kiti cha huruma ya Mungu katika maisha yao! Toba na wongofu wa ndani ni muhimu sana katika kuambata neema na baraka za Mwenyezi Mungu katika maisha. Vijana wanapaswa kutambua kwamba, dhambi ipo na ni kikwazo kikubwa katika kujenga mahusiano mema na Mwenyezi Mungu pamoja na jirani.

Sakramenti ya Upatanisho ni muhimu sana katika ukuaji na ukomavu wa maisha ya mtu kiroho. Vijana wanapaswa kujenga ndani mwao utamaduni wa kuchunguza dhamiri zao mbele ya Mwenyezi Mungu, kwa kuangalia ukweli, tayari kuanza safari ya ukomavu wa maisha ya kiroho. Baba Mtakatifu Francisko akiwa na umri wa miaka kumi na saba, alionja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yake kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho na huo ukawa ni mwanzo wa wito na maisha yake ya kitawa. Baba Mtakatifu katika Wosia wake wa kitume “Gaudete et exsultate” yaani “Furahini na kushangalia, wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo anasema, Wakristo wote wanahamasishwa kuwa watakatifu na wakamilifu kama Baba yao wa mbinguni alivyo mkamilifu. Kila mtu anaitwa kuwa mtakatifu kadiri ya maisha na wito wake. Waamini kwa njia ya maisha na ushuhuda wao, wasaidie kuyatakatifuza malimwengu kwa kuwa kweli ni chumvi ya dunia na mwanga mataifa.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, huruma ya Mungu ni kiini cha Injili na ni njia muafaka ya uinjilishaji mpya unaojikita katika mchakato wa ushuhuda wenye mvuto na mashiko, kielelezo cha imani tendaji! Umefika wakati kwa waamini kujenga utamaaduni wa kuchunguza dhamiri zao, ili kuangalia ikiwa kama maisha yao yanaendana na utu wema sanjari na kweli za Kiinjili zinazotangazwa na kushuhudiwa na Mama Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume “Misericordia et misera” yaani “Huruma na haki” anasema, huruma ya Mungu inapaswa kuendelezwa katika medani mbali mbali za maisha ya watu kama utimilifu wa huruma, upendo na msamaha wa Mungu unaobubujika kutoka katika Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo kutoka kwa wafu! Huruma ya Mungu inajionesha katika maadhimisho ya Sakramenti mbali mbali za Kanisa, lakini kwa namna ya pekee kabisa, Sakrameti ya Ekaristi Takatifu, Upatanisho na Mpako wa Wagonjwa.

Huruma ya Mungu inaendelea kujifunua katika historia na maisha ya watu kwa njia ya Neno la Mungu, ikikumbukwa kwamba,  Biblia ni muhtasari wa ufunuo wa huruma ya Mungu kwa binadamu! Baba Mtakatifu anawataka Mapadre kuhakikisha kwamba, wanaandaa mahubiri yao vyema na kuendelea kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu inayojikita katika: ukarimu, ushuhuda wa maisha, msukumo wa kichungaji, uwazi na utayari wa kutoa huduma ya huruma ya Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho. Vijana wa kizazi kipya wanahamasishwa na Kanisa ambaye ni Mama na Mwalimu kukimbilia huruma ya Mungu katika maisha yao, ili waweze kupambanua vyema wito wao ndani ya Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.