2018-04-26 16:12:00

Papa kukutana na wahanga wa nyanyaso za kijinsia kutoka Chile


Dr. Greg Burke, Msemaji mkuu wa Vatican, akijibu maswali ya waandishi wa habari mjini Vatican amesikika akisema kwamba, Baba Mtakatifu Francisko wakati wowote kuanzia sasa anatarajiwa kukutana na kuzungumza na waathirika wa nyanyaso za kijinsia kutoka nchini Chile. Hawa ni Juan Carlos Cruz, James Hamilton na Jose Andrès Murillo. Baba Mtakatifu amewshukuru watu hawa kwa kukubali mwaliko wake na kwamba, anatanguliza tangu sasa shukrani zake za dhati kabisa. Mkutano huu utakuwa ni wa faragha unaofumbatwa katika udugu na kwamba, Baba Mtakatifu mwenyewe anataka kuomba msamaha; kushiriki katika mateso na mahangaiko yao pamoja na kuona aibu kwa yale yaliyowasibu maishani mwao.

Baba Mtakatifu anataka kuwasikiliza kwa dhati kabisa kutoka moyoni mwake, ili ushauri watakaompatia uweze kusaidia kuzika kashfa za nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa. Kila mtu atakutana na Baba Mtakatifu kwa faragha na anawaomba waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya Kanisa nchini Chile ambalo kwa sasa linapitia katika kipindi kigumu sana cha historia ya maisha na utume wake. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, ataweza kukutana na waathirika hawa katika hali ya amani na utulivu wa ndani; kwa kuaminiana na kuthaminiana kama mambo msingi yanayopania kuganga na kutibu nyanyaso hizi kutoka katika dhamiri za watu, ikizingatiwa kwamba, ni vitendo ambavyo vimetekelezwa ndani ya Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 








All the contents on this site are copyrighted ©.