2018-04-26 15:00:00

Papa Francisko akutana na Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria


Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria, kuanzia tarehe 24-30 Aprili 2018 linafanya hija ya kitume mjini Vatican kwa kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko pamoja na waandamizi wake. Hii ni hija ambayo kadiri ya sheria kanuni za Kanisa hufanyika walau kila baada ya miaka mitano! Kanisa Katoliki nchini Nigeria linaundwa na Majimbo makuu 9 na chini yake kuna majimbo 45. Ni Kanisa ambalo bado ni changa, lakini linakabiliwa na changamoto, matatizo na fursa katika maisha na utume wake wa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! 

Uongozi mbaya, rushwa na ufisadi wa mali ya umma; ukabila, udini na misimamo mikali ya kiimani ni kati ya mambo yanayoendelea kusababisha vita, kinzani na mipasuko ya kijamii na kidini sehemu mbali mbali za Bara la Afrika, lakini Nigeria kwa namna ya pekee kabisa! Wanaigeria ni watu wa dini na kwamba, imani ni sehemu muhimu sana ya utambulisho na maisha yao. Sehemu kubwa ya wananchi wa Nigeria ni waamini wa dini ya Kiislam na Kikristo.

Takwimu zinaonesha kwamba, kuna Wakristo milioni 70 na kati yao Wakatoliki ni waamini milioni 26. Kwa bahati mbaya, ukabila na udini usiokuwa na mashiko ni kati ya mambo yanayowatafuna na kuwanyong’onesha sana wananchi wa Nigeria. Inasikitisha sana kuona kwamba, udini na ukabila umetumiwa sana kuwagawa wananchi wa Nigeria hata katika masuala ya kiuchumi, kisiasa na kijamii. Kikundi cha kigaidi cha Boko Haramu katika miaka ya hivi karibuni kimekuwa ni chanzo kikuu cha maafa na mauaji ya watu wasiokuwa na hatia. Kimesababisha uharibifu mkubwa wa miundo mbinu ya shule, huduma ya afya na barabara.

Takwimu zinaonesha kwamba, tangu mwaka 2006 hadi wakati huu, wakristo waliouwawa kutokana na misimamo mikali ya kidini nchini Nigeria ni zaidi ya waamini 13, 000. Watu milioni 1.5 wamelazimika kuyakimbia makazi yao kwa kuhofia usalama wa maisha na mali zao. Kikundi cha Boko Haramu kimekuwa pia kikiendesha vitendo vya kigaidi nchini Chad, Cameroon na Niger. Wanawake na wasichana wamekuwa wakitekwa nyara na kubakwa! Watoto na vijana wamekuwa wakibebeshwa mabomu ya kujitoa mhanga, hali ambayo imepandikiza utamaduni wa kifo. Jitihada za Serikali ya Rais Muhammad Buhari aliyeingia madarakani kunako mwaka 2015 kutaka kurejesha: usalama wa raia na mali zao; amani na utulivu, hadi sasa zimegonga mwamba nchini Nigeria.

Mgogoro wa ardhi kati ya jamii ya wakulima na wafugaji, athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na athari za mtikisiko wa uchumi kitaifa na kimataifa ni mambo ambayo yanaendelea kuchangia hali ngumu ya maisha ya wananchi wa Nigeria. Kinzani za kidini kati ya Wakristo na Waislam huko Jos pamoja na utekwaji nyara wa wanafunzi wa shule ya Chibok ni kati ya matukio ambayo yametikisa Jumuiya ya Kimataifa. Wanafunzi 82 waliachiliwa huru, lakini hadi sasa hatima ya wanafunzi wengine 113 haijulikani. Katika shida, mahangaiko na changamoto zinazoikabili familia ya Mungu nchini Nigeria, Baba Mtakatifu Francisko amekuwa daima akiikumbuka na kuisindikiza. Baba Mtakatifu kunako mwaka 2015 aliwaandikia barua Maaskofu wa Nigeria, akiwashukuru na kuwatia moyo kwani licha ya matatizo na changamoto mbali mbali walizo nazo nchini humo, lakini bado Kanisa limekuwa ni chombo na shuhuda wa ukarimu, huruma na msamaha, tunu msingi katika maisha na utambulisho wa Kanisa.

Kanisa Katoliki nchini Nigeria, limeendelea kujikita katika mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene katika ukweli na uwazi; ili kulinda na kudumisha: utu, heshima, haki msingi za binadamu; ustawi, mafao na maendeleo ya wengi. Kanisa bado liko mstari wa mbele katika kuhimiza umuhimu wa upatanisho unaofumbatwa katika; majadiliano na msamaha ili kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa. Majadiliano ya kidini na kiekumene yanafumbatwa kwa namna ya pekee katika huduma makini kwa waathirika wa vitendo vya kigaidi nchini Nigeria sanjari na ujenzi wa nyumba za ibada, ili kweli dini ziweze kusaidia kuponya madonda ya chuki, utengano na uhasama unaobubujika kutokana na misimamo mikali ya kidini na kiimani!

Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria linakaza kusema, licha ya changamoto na matatizo yote haya, lakini bado kuna miito mingi ya maisha ya kipadre na kitawa. Wakristo wengi wanashiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Changamoto kubwa kwa wakati huu ni utamaduni wa kifo unaoendelea kupandikizwa nchini Nigeria kwa kukumbatia sera za utoaji wa mimba pamoja na vitendo vya kigaidi ambavyo vimepeleka familia nyingi zikijikuta zikiwa na watoto yatima, wajane na watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi.

Sera za usawa wa kijinsia na uzazi salama ni hatari sana kwa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya, biashara ya binadamu na utumwa mamboleo ni kati ya mambo yanayochafua utu na heshima ya binadamu; umoja, mshikamano na mafungamano ya kijamii. Maaskofu nchini Nigeria wanaitaka familia ya Mungu nchini humo, kujenga na kudumisha Injili ya familia inayofumbatwa katika Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.

Kanisa kwa kushirikiana na Serikali pamoja na wadau mbali mbali wa maendeleo endelevu ya binadamu, limekuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya umaskini wa hali na kipato; dhidi ya mmong’onyoko wa tunu msingi za kiroho, kanuni maadili na utu wema. Maaskofu wanasema, sera makini na endelevu katika masuala ya kiuchumi ni muhimu sana katika mapambano dhidi ya ukosefu wa fursa za kazi na ajira miongoni mwa vijana wa kizazi kipya! Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria linasema limefadhaishwa sana na matukio yaliyojitokeza Jimbo Katoliki la Ahiara ambako tangu mwaka 2012, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI alipomteua Askofu Peter Okpaleke, hakufanikiwa kukanyaga mguu ndani ya Jimbo lake! Baada ya vuta nikuvute, tarehe 19 Februari 2018, Baba Mtakatifu Francisko akaridhia Askofu Peter Okpaleke ang’atuke madarakani kwa ajili ya ustawi, mafao na maendeleo ya familia ya Mungu Jimbo Katoliki la Ahiara. Ni tukio ambalo bado linahitaji toba na wongofu wa ndani, ili kuanza kuandika historia ya nidhamu, utii na maendeleo ya watu wa Mungu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 
All the contents on this site are copyrighted ©.