2018-04-26 15:01:00

Kanisa linajengwa kwa Ekaristi na upendo unaomwilishwa katika huduma


Siku ile iliyotangulia kuteswa kwake, Kristo Yesu aliweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Daraja Takatifu pamoja na kuwaosha wanafunzi wake miguu, kielelezo cha upendo unaomwilishwa katika huduma makini kwa watu wa Mungu. Kristo Yesu, akawaachia Mitume wake mfano wa kuigwa, kwani kazi iliyokuwa inafanywa enzi hizo na watumwa ameitekeleza kwa kuwaosha miguu! Kumbe, upendo, huduma na utume ni mambo makuu matatu yanayotegemeana na kukamilishana katika maisha na utume wa Kanisa. Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 26 Aprili 2018 wakati wa mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican.

Kristo Yesu kabla ya kuingia katika mateso yake aliwausia mitume wake mambo msingi ya kuzingatia katika maisha na utume wa Kanisa: Yesu aliwapatia Fumbo la Ekaristi Takatifu yaani: Mwili na Damu yake Azizi viwe ni chakula chao cha kiroho. Kristo Yesu kwa kuwaosha miguu mitume wake alikazia amri ya upendo unaomwilishwa katika huduma kama mambo msingi yanayolijenga na kuliimarisha Kanisa. Kumbe, waamini wanapaswa kuhakikisha kwamba, wanakuwa waaminifu katika kutekeleza maagizo haya ya Kristo katika maisha yao. Yesu aliwapatia mitume wake Amri ya upendo kwa Mungu na jirani, lakini upendo huo unapaswa kufafana na upendo ambao ameutoa kwa ajili yao, yaani upendo usiokuwa na mipaka, upendo unaoweza kujisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Bila upendo, Kanisa kama taasisi haina mvuto wala mashiko, kumbe, Kristo Yesu anawafundisha mitume wake jinsi ya kupenda kama yeye anavyopenda bila ya kujibakiza hata kidogo. Ni upendo unaomwilishwa katika huduma; kwa kuoshana wao kwa wao kama alivyofanya yeye mwenyewe.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, huu ni upendo unaofumbatwa katika ukweli na unyenyekevu wa hali ya juu. Yesu: Bwana na Mwalimu amewaachia urithi wa uwepo wake endelevu katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu inayopaswa kuwa ni chemchemi ya upendo unaomwilishwa katika huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii! Kwa kuzingatia mambo haya, Kanisa litaendelea kua aminifu kwa Kristo Yesu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Yesu aliwafahamu mitume wake, na hata yule ambaye angemsaliti, mwaliko kwa kila mwamini katika undani na ukimya wa maisha yake, kumpatia nafasi Kristo Yesu, ili aweze kumwangalia kwa jicho la huruma na mapendo! Pale ambapo wamemsaliti, wajute dhambi zao kwa kujionea aibu! Kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Petro, waamini wawe na ujasiri wa kumwambia Kristo kwamba, yeye anafahamu yote, kwamba, wanampenda! Waamini washuhudie upendo unaomwilishwa katika huduma hadi dakika yao ya mwisho katika maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.