2018-04-26 15:56:00

Baraza la Makardinali Washauri lahitimisha mkutano wake wa XXIV


Baraza la Makardinali Washauri lililoanza kikao chake cha XXIV, tangu tarehe 23-25 Aprili 208 chini ya uongozi wa Baba Mtakatifu Francisko limepitia muswada wa Katiba ya kitume ya Sekretarieti kuu ya Vatican. Wajumbe wameomba muda zaidi wa kuendelea kuyadadavua yale yaliyomo kwenye muswada huu, ili hatimaye, uweze kuwasilishwa kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa mapitio zaidi na hatimaye, kuweza kuidhimishwa kwa ajili ya kuanza kutumika.

Haya yamesemwa na Dr. Greg Burke, Msemaji mkuu wa Vatican, Jumatano, tarehe 25 Aprili 2018 alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari walioko mjini Vatican. Makardinali wote washauri wamehudhuria mkutano huu, akiwemo pia Kardinali George Pell. Kwa upande wake, Kardinali Reinhard Marx, alishindwa kuhudhuria kikao cha Jumatatu kutokana na sababu zilizokuwa nje ya uwezo wake. Wajumbe wamejadili na kupembua kwa kina na mapana tema mbali mbali ambazo tayari zimekwisha jadiliwa kwenye mikutano iliyopita. Kwa wakati huu, wajumbe wamekazia umuhimu wa Sekretarieti kuu ya Vatican kwa ajili ya huduma kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro na Makanisa mahalia; tabia na sifa za shughuli za kichungaji zinazotekelezwa na Sekretarieti kuu ya Vatican; Taasisi; Dhamana na Wajibu wa Idara ya Diplomasia ya Vatican; Kutangaza Injili, Ari na mwamko wa kimisionari kama mambo msingi yanayo pambanua shughuli na utume unaotekelezwa na Sekretarieti kuu ya Vatican.

Kwa upande wake, Kardinali Sean Patrick O’Malley, amewashirikisha Makardinali sera na mikakati inayotekelezwa na Tume ya Kipapa kwa ajili ya kulinda watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia sehemu mbali mbali za dunia. Tume hii, imesikiliza shuhuda za nyanyaso za kijinsia kutoka Brazil, Ethiopia, Australia na Italia na kwamba, utume huu tete na nyeti katika maisha na utume wa Kanisa unatekelezwa kwa nidhamu ya hali ya juu, weledi, uadilifu na uwajibikaji. Tume itaendelea kuwasikiliza waathirika wa nyanyaso za kijinsia, ili kuweza kupata mang’amuzi mapana zaidi. Baraza la Makardinali Washauri limepata pia nafasi ya kumsikiliza Monsinyo Lucio Adrian Ruiz, Katibu mkuu wa Sekretarieti ya Mawasilaino ya Vatican, kuhusu hatua ambayo imefikiwa hadi wakati huu kama sehemu ya utekelezaji wa mageuzi makubwa katika vyombo vya mawasiliano ya jamii vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican. Baraza la Makardinali Washauri, litakutana tena kuanzia tarehe 11 hadi tarehe 13 Juni 2018 hapa mjini Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 

 
All the contents on this site are copyrighted ©.