2018-04-25 15:42:00

Vijana washirikishwe katika mchakato wa majadiliano ya kidini


Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa kitume “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili” anakazia sana mchakato wa majadiliano ya kidini kama sehemu ya mchango wa Kanisa katika kukuza na kudumisha amani, ustawi, mafao na maendeleo ya wengi na kwamba, Kanisa linatumwa kutangaza na kushuhudia Injili ya amani! Majadiliano ya kidini yanapania pamoja na mambo mengine kuendeleza uhuru wa kuabudu, tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu pamoja na huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Kamwe dini hazipaswi kuwa ni chanzo cha: vita, kinzani na mipasuko ya kijamii, bali daraja inayowasaidia waamini wa dini mbali mbali kujenga: mshikamano wa umoja na udugu ili kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu! Hii ni dhamana inayopaswa kuvaliwa njuga na waamini wa dini mbali mbali duniani. Huu ni mchango uliotolewa hivi karibuni na Askofu Miguel Angel Ayuso Guixoit, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini alipokuwa anatoa hotuba elekezi kwenye kongamano kati ya Wakristo na Waislam lililokuwa limeandaliwa na Chama cha Kitume cha Wafokolari, katika Kituo cha Mariapoli, huko Castelgandolfo, nje kidogo ya mji wa Roma.

Kongamano hili liliongozwa na kauli mbiu “Kwa pamoja ili kutoa matumaini: Wakristo na Waislam katika hija ya karama ya umoja.” Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na mabadiliko makubwa ya kijamii, ambamo kuna mwingiliano mkubwa wa watu, tamaduni, imani na mapokeo mbali mbali. Kutokana na changamoto hii, kuna haja kwa waamini wa dini mbali mbali kujibidisha ili kufahamiana, kuheshimiana na kuthaminiana hata katika tofauti zao msingi ambazo ni utajiri mkubwa unaopaswa kudumishwa.

Ujinga na maamuzi mbele, yamekuwa ni chanzo kikuu cha kinzani na migogoro ya kidini na kiimani sehemu mbali mbali za dunia. Kumbe, majadiliano ya kidini kati ya Wakristo na Waislam yanalenga kutoa nafasi kwa waamini wa dini hizi mbili: kwanza kabisa kukutana, kufahamiana na kuanza mchakato wa kusaidiana kwa hali na mali. Ili kuweza kujikita katika majadiliano ya kidini yanayopania ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, kwanza kabisa kuna haja kwa waamini kufahamu utambulisho wao unaowajengea uwezo wa kuwathamini waamini wa dini nyingine.

Askofu Miguel Angel Ayuso Guixoit, anakaza kusema, huu ndio mwanzo wa utamaduni wa kusikilizana katika ukweli na uwazi; kwa kuheshimu na kuthamani amana na utajiri wa utu na maisha ya kiroho kutoka kwa waamini wa dini nyingine. Majadiliano ya kidini pamoja na jitihada za kutaka kufahamiana ni msingi wa ujenzi wa madaraja ya urafiki ambao una mafao makubwa kwa familia ya binadamu katika ujumla wake. Kwa njia hii, waamini wa dini mbali mbali watajitahidi kubomoa kuta na viambaza vinavyowatenga kutokana na hofu, wasi wasi na ujinga. Hii ni safari ndefu na ngumu, inayowahitaji waamini wa dini mbali mbali kuambatana na kushikamana, ili kwa pamoja waweze kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa matumaini. Kumbe, hata Chama cha Kitume cha Wafokolari kina wajibu na dhamana ya kujenga umoja na matumaini miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali.

Kardinali Jean Louis Tauran, hivi karibuni akizungumza na viongozi wa chama hiki cha kitume, alikazia umuhimu wa elimu kwa vijana wa kizazi kipya katika mchakato mzima wa majadiliano ya kidini. Hii inatokana na ukweli kwamba, vijana katika ulimwengu mamboleo wanaendelea kukutana na bahari ya matukio yanayowakatisha tamaa na kuwaondolea imani!

Ni wajibu wa waamini wa dini mbali mbali duniani kuhakikisha kwamba elimu ya majadiliano ya kidini kwa vijana wa kizazi kipya inavaliwa njuga, kwa kuwekeza miongoni mwa vijana, ili kuwapatia matumaini ambayo yatawasaidia kutambua kwamba, kwa hakika wanapendwa, wanaheshimiwa na kuthaminiwa. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake kitume nchini Misri kunako mwaka 2017, akizungumza na wajumbe wa mkutano wa dini kimataifa kwenye Chuo Kikuu cha Al-Azhar, kilichoko mjini Cairo, alikazia umuhimu wa utambulisho wa waamini; ujasiri wa kuthamini tofauti msingi kati ya waamini, ujasiri wa kuweza kukabiliana na changamoto katika ukweli na uwazi pamoja na kuwa na nia njema!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.