2018-04-25 07:16:00

Utandawazi wa mshikamano katika maisha na utume wa Kanisa!


Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanasema uchungu na fadhaa ya wanadamu wa nyakati hizi hasa za wale maskini na wale wanaoteseka ni furaha na matumaini, uchungu na fadhaa ya wafuasi wa Kristo pia! Kanisa linapenda kusoma alama za nyakati na kuzifafanua mintarafu mwanga wa Injili, ili kujibu changamoto hizi na kuzipatia maana mpya kadiri ya tunu msingi za Kiinjili. Hizi ndizo changamoto ambazo zimevaliwa njuga na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM pamoja na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya, CCEE katika mkutano wa ushirikiano baina ya Mabaraza haya mawili kuanzia tarehe 12-15 Aprili 2018, huko Fatima, nchini Ureno.

Kati ya mada zilizopembuliwa ni: athari za utandawazi katika maisha na utume wa vijana wa kizazi kipya; changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta: usalama, hifadhi na maisha bora zaidi ughaibuni; utu na heshima ya binadamu sanjari na ekolojia ya mazingira, kama sehemu ya utunzaji bora wa kazi ya uumbaji ambayo binadamu amekabidhiwa ili kuiendeleza kwa ajili ya mafao ya kizazi cha sasa na kile kijacho! 

Utandawazi ni mchakato unaogusa maisha ya mtu mzima: kiroho na kimwili; unagusa na kutikisa maisha ya mtu binafsi, familia na jamii katika ujumla wake. Utandawazi una tabia ya kujielekeza zaidi katika masuala ya kitamaduni, kiuchumi, kisiasa na hata kidini. Kimsingi, utandawazi unagusa medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu. Kwa upande mwingine, jamii ikijenga na kukuza utandawazi wa umoja, udugu na upendo, kunakuwepo na mafungamano ya watu wa familia ya Mungu duniani; watu wanaweza kujizatiti na kusimama kidete: kulinda, kutetea na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu kwa kujikita katika mchakato wa haki, amani na maridhiano kati ya watu!

Utandawazi wenye mvuto na mashiko, unawawezesha watu kushirikishana na kugawana amana na utajiri wa maisha ya kiroho; kwa kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni, urithi mkubwa kwa vijana wa kizazi kipya! Utandawazi unapotea na kuogelea katika dhambi na ubinafsi kama inavyojionesha sehemu nyingi za dunia, unakuwa ni “jamvi” la uchu wa mali na madaraka; uchoyo na ubinafsi; mapambano kati ya nchi maskini na tajiri; kati ya wenye nacho na “akina yakhe pangu pakavu tafadhali tia mchuzi”.

Utandawazi katika mwelekeo huu, unakuwa ni “kichaka” cha kutaka kuchuma rasilimali na utajiri asilia kwa mafao binafsi; kwa kujikita katika raha, starehe na kupenda mno anasa kiasi cha kutoguswa na shida wala mahangaiko ya maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Utandawazi wa namna hii unabomoa na kuvuruga misingi ya utamaduni, maisha ya kiroho, utu na heshima ya binadamu na matokeo yake ni kukumbatia utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika sera za utoaji mimba, kifo laini na ndoa za watu wa jinsia moja.

Askofu mkuu Charles Palmer-Buckel wa Jimbo kuu la Accra, Ghana ambaye pia ni Mtunza hazina wa SECAM anasikitika kusema kwamba, utandawazi wa kiuchumi umepelekea matatizo na changamoto nyingi katika sekta ya kiuchumi kiasi cha kuwa ni chanzo cha umaskini na tabia ya kuwageuzia maskini kisogo na hivyo kusahamu kwamba, maskini ni amana na utajiri wa Kanisa, hawa ni walengwa wa kwanza wa Habari Njema ya Wokovu! Katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, maskini hana chake ni sawa na soli ya kiatu!

Utandawazi umewajengea watu tamaa na uchu wa mali na madaraka na matokeo yake ni vita, kinzani na mipasuko ya kijamii, kifamilia, kitaifa na kimataifa, kwani hapa kinachopewa kipaumbele cha kwanza ni fedha na utajiri na wala si utu na heshima ya binadamu! Haya ni mambo ambayo pia yanagusa hata maisha ya wanandoa, kwani falsafa ya mtindo wa sasa wa maisha ni “pochi kwanza, ndoa baadaye” hatari kubwa katika kukuza na kudumisha Injili ya familia inayosimikwa katika Injili ya uhai.

Mashirika na Makampuni ya uzalishaji na huduma kitaifa na kimataifa yanaendelea kufaidika na faida kubwa wanayozalisha, lakini maskini wanaendelea kutumbukiza katika ombwe la umaskini wa hali na kipato! Kumekuwepo na uporaji wa maeneo makubwa ya ardhi ambayo yamepelekea watu kuhamishwa kutoka makazi yao ili kupisha kilimo cha mashamba makubwa bila hata kupata fidia ya kutosha kuanza tena mchakato wa maisha mapya!

Ni makampuni ambayo yamejikita katika uzalishaji wa nishati uoto wakati watu wanaendelea kupoteza maisha kutokana na baa la njaa na utapiamlo wa kutisha bila kusahau uchafuzi na uharibifu mkubwa wa mazingira nyumba ya wote! Viongozi wa serikali, wanasiasa, wachumi na wapanga sera kutoka Barani Afrika wanapaswa kusimama kidete: kulinda, kutetea na kudumisha ustawi, maendeleo, mafao ya wengi na haki msingi za familia ya Mungu kutoka Barani Afrika. SECAM Barani Afrika iendelee kuwa ni shuhuda, chombo na sauti ya kinabii kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kuna wimbi kubwa sana la biashara ya binadamu na utumwa mamboleo.

Haya ni matukio yanayonyanyasa utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu! Haya ni madhara ya utandawazi kama yalivyojadiliwa na wajumbe wa SECAM pamoja na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya katika mkutano wake huko kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Fatima, ulioandaliwa kwa hisani ya Kardinali Manuel Clemente, Patriaki wa Ureno kwa kushirikiana na Askofu Antonio Marto wa Jimbo Katoliki la Leiria-Fatima nchini Ureno.

Askofu mkuu Charles Palmer-Buckel anaendelea kudadavua kwa kusema kwamba, kumekuwepo na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia kiasi kwamba, leo hii, habari na matukio mbali mbali ya kitaifa na kimataifa yanapatikana katika viganja vya watu! Maajabu makubwa ya Mungu! Matumizi sahihi ya tovuti na wavuti yamewapatia vijana wa kizazi kipya ujuzi, maarifa na weledi katika medani mbali mbali za maisha, lakini kwa bahati mbaya, wengi wa watumiaji wa mitandao hii hawana elimu ya kutosha kuhusu athari za njia za mawasiliano ya kijamii katika utu na heshima ya binadamu! Matokeo yake ni kuvunjika kwa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika mchakato wa kujenga na kudumisha haki jamii, utu na heshima ya binadamu, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, ili kweli utandawazi uweze kuwa na mvuto na mashiko kwa watu wengi zaidi.

Askofu mkuu Gabriel Mbilingi, Rais wa SECAM, katika hotuba yake elekezi amegusia faida, hasara na changamoto za utandawazi wenye mvuto na mashiko kama kielelezo cha ushuhuda wa umoja, mshikamano na upendo kwa Kristo na Kanisa lake. Anakiri kwamba, kuna sababu msingi zinazowafanya baadhi ya watu kutoka katika Nchi za Kiafrika kuzikimbia nchi zao ili kutafuta: hifadhi, usalama na maisha bora zaidi. Lakini, kuna baadhi ya watu wanaliona Bara la Ulaya kuwa ni “Jahazi” la maendeleo, uhuru, ustawi na mafanikio katika maisha kiasi cha kuhatarisha maisha kwa kufanya safari katika mazingira tete na hatarishi.

Ni watu wanaothubutu kupambana na utupu jangwani na hata wakati mwingine kumezwa kwenye “tumbo la Bahari ya Mediterrania” ambako hata makaburi yao hayana alama na matumaini yao huyeyuka kama ndoto ya mchana! Haya ni madhara ya utandawazi usiokuwa na mashiko. Kanisa katika maisha na utume wake, linapaswa kukuza na kudumisha utandawazi unaofumbatwa katika Mafundisho Jamii ya Kanisa yaani: utu, heshima, haki msingi za binadamu, ustawi, mafao na maendeleo ya wengi!

Kardinali Angelo Bagnasco, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya katika hotuba yake elekezi amekazia: utume wa Kanisa Barani Ulaya unaopaswa kuwa ni kioo cha upendo wa Mungu kwa waja wake, uliofunuliwa na Kristo Yesu unaopaswa kuwaambata na kuwafumbata watu wote! Lakini, tabia ya ukanimungu, maamuzi mbele ni mambo yanayoendelea kushika kasi kiasi cha kuingilia medani mbali mbali za maisha ya watu Barani Ulaya. Utume wa Kanisa katika mazingira na changamoto kama hizi ni kuendelea kujikita katika: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kwa kuzingatia ukweli na uzuri wa mambo.

Anasema, kuna maendeleo makubwa katika uelewa wa “dhana ya utamaduni” ambayo inaonekana kutokuwa na vifungo vya tunu za jumla kwa wananchi wa Bara la Ulaya, lakini, Kanisa linatangaza na kushuhudia kwamba, Kristo Yesu ni: njia, ukweli na uzima, aliteswa, akafa na kufufuka kwa wafu ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Kristo Yesu ni ufunuo wa Uso wa Baba wa milele, chemchemi na kipimo cha utu wa kweli, maendeleo na matarajio ya utu wa binadamu! Hapa kuna haja ya kuhakikisha kwamba, maendeleo ya utamaduni yanasaidia pia kuleta ukombozi kwa wananchi wa Bara la Ulaya kwa kudumisha utamaduni unaofumbatwa katika historia, mapokeo, mahali na dini pamoja na mafungamano yanayomwandama mtu katika ujumla wake.

Kardinali Angelo Bagnasco, anaendelea kufafanua kwamba, Ibada na Utamaduni ni sawa na chanda na pete ni mambo yanayoshibana na kukamilishana, kwa kutambua kwamba, mwanadamu hapa duniani ni hujaji kuelekea maisha ya uzima wa milele! Hija hii ya maisha ya mwanadamu inafumbatwa kwa namna ya pekee katika historia, tamaduni na kanuni sheria. Kanisa linatumwa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Kristo ni kiini cha Habari Njema ya Wokovu, changamoto kubwa katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Upya wa maisha unaopaswa kuendelezwa ni kwa kutambua kwamba, kiini cha imani ya Kanisa ni Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai. Fumbo la Umwilisho linatoa maana na heshima ya binadamu kadiri ya mpango wa Mungu. Kumbe, imani kwa Kristo na Kanisa lake, ni kiini cha umoja, upendo na mshikamano unaojenga Jumuiya ya waamini inayosimikwa katika misingi ya ukweli, urafiki, uaminifu na udumifu. Yote haya yanalenga kukuza na kudumisha utu na heshima ya binadamu mahali popote pale alipo! Hata katika shida na changamoto za maisha, hakuna sababu ya waamini kukata wala kujikatia tamaa katika maisha yao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.