2018-04-25 15:02:00

Papa Francisko: Maisha yote ya Mkristo ni mapambano dhidi ya dhambi


Baba Mtakatifu Francisko katika kipindi hiki cha Pasaka anaendelea na Katekesi kuhusu maisha ya Kikristo kwa kuchambua maadhimisho ya Sakramenti ya Ubatizo ambayo ni msingi wa maisha yote ya Kikristo na lango la kuingilia uzima katika Roho na hivyo kumruhusu Kristo Yesu kufanya makazi kwa waja wake. Ishara ya Msalaba na Tangazo la Neno la Mungu ni mafundisho muhimu sana kwa waamini wanaopokea Sakramenti ya Ubatizo.

Baba Mtakatifu wakati wa Katekesi yake, Siku ya Jumatano, tarehe 25 Aprili 2018 anasema, tangazo la Neno la Mungu huwaangazia waamini ukweli mfunuliwa na huamsha jibu la imani lisilotengana na Sakramenti ya Ubatizo ambayo kimsingi, ni Sakramenti ya imani inayomwingiza mtu kisakramenti katika maisha ya imani na hivyo, inayomwondolea mtu dhambi. Kristo Yesu aliwapatia wafuasi wake imani kwa kujipambua kuwa ni chemchemi inayobubujikia uzima wa milele, nuru ya ulimwengu, ufufuo na uzima wa milele. Haya ni mambo msingi wanayofundishwa wakatekumeni wanapojiandaa kupokea Sakramenti ya Ubatizo. Wanahimizwa kuwa wasikivu wa Neno la Mungu, Mafundisho na Matendo yake makuu!

Kwa njia hii, wakatekumeni wanaonja uzoefu na mang’amuzi aliyopata yule mwanamke Msamaria pale kisimani! Kristo Yesu akazima kiu yake kwa kumpatia maji yanayobubujikia uzima wa milele! Kama ilivyokuwa kwa yule mtu aliyezaliwa kipofu, akapata kuona tena na Lazaro aliyekuwa amekufa, akatoka kaburini mzima! Injili inayotangazwa inabeba ndani mwake nguvu inayoleta mabadiliko kwa mwamini anayelipokea Neno la Mungu kwa imani na hivyo kuokolewa kutoka katika mitego ya Ibilisi, shetani, ili kujifunza kumtumikia Mwenyezi Mungu kwa furaha na upya wa maisha!

Baba Mtakatifu anasema, waamini wanasindikizwa kwa Sala ya Kanisa, Litania ya Watakatifu, Sala ya Kupunga Pepo pamoja na kupakwa Mafuta ya wakatekumeni, waamini wanapoelekea kwenye Kisima cha Ubatizo. Haya ni Mapokeo ya Kanisa tangu mwanzo kabisa yanayoonesha mapambano dhidi ya dhambi na ubaya wa moyo. Lengo ni kuwaonesha waamini wanaozaliwa upya kwa maji na Roho Mtakatifu njia inayoelekea kwenye wema, kwa kujimanua kutoka kwenye dhambi ili hatimaye, kuingia katika Ufalme wa neema ya Mungu.

Mama Kanisa anasali kwa ajili ya watu wote wa Mungu, ili waweze kuunganika naye kutoka katika undani wa mioyo yao. Hata watoto wachanga wanaombewa kwa Mwenyezi Mungu ili aweze kuwaondolea dhambi ya asili na hatimaye, kuwaweka wakfu kama Mahekalu ya Roho Mtakatifu. Sala kwa watoto wachanga inapania kuwalinda na maadui wa kiroho na kimwili, dhamana na wajibu uliotekelezwa na Kristo Yesu katika maisha yake, ili kujenga Ufalme wa Mungu hapa duniani. Ushindi wake dhidi ya Shetani unatoa mwanya wa furaha ya ukuu wa Mungu kuonekana na hivyo kuupatanisha na maisha. Sakramenti ya Ubatizo ni zawadi ya Roho Mtakatifu inayomwezesha mwamini kupambana na Ibilisi, shetani, kwani uzoefu wa maisha ya Kikristo unaonesha kwamba, vishawishi ni chanzo kikuu kinachomwondoa mwamini kutoka usoni pa Mwenyezi Mungu. Sakramenti ya Ubatizo inawaandaa waamini kupambana na shetani kila siku ya maisha yao, kwani daima anazunguka zunguka akitafuta watu wa kuwapigisha magoti katika utawala wake.

Licha ya sala, katika madhehebu ya Ubatizo kuna kupakwa mafuta ya wakatekumeni, anamkataa shetani na mambo yake yote, anaandaliwa vyema ili kukiri imani ili hatimaye, aweze kuzaliwa upya kwa maji na Roho Mtakatifu. Mafuta matakatifu yanaingia mwilini kama alama ya wokovu inayotolewa na Kristo Yesu ili kumwimarisha Mkristo katika mapambano dhidi ya dhambi na hatimaye, aweze kushinda. Baba Mtakatifu anakiri kwamba, si rahisi sana kupambana na dhambi pamoja na vishawishi vya dunia hii, lakini jambo la msingi ni kutambua kwamba, maisha yote ya Mkristo ni mapambano dhidi ya dhambi. Katika mapambano haya, waamini wanasindikizana na Mama Kanisa katika sala na kuwapatia maisha mapya yanayobubujika kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo, ili kwa nguvu ya Fumbo la Pasaka, waweze kumshinda shetani. Baba Mtakatifu anakaza kusema, yote wanayaweza katika yeye anayewatia nguvu, yaani Mwenyezi Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.