2018-04-24 09:34:00

Watu wanateseka kwa vita, njaa na umaskini huko Afrika ya Kati!


Madhara ya vita na mipasuko ya kijamii, kisiasa na kidini ni makubwa sana kwenye Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, kiasi hata cha kuonekana kana kwamba, vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini humo imesahauliwa na Jumuiya ya Kimataifa. Bado kuna mauaji ya watu wasiokuwa na hatia, uhuru wa kuabudu uko mashakani na kwamba, huduma ya elimu, afya, ustawi na maendeleo endelevu ya watu inasua sua kwa kiasi kikubwa! Katika hali na mazingira kama haya, Kanisa limeendelea kuwa kweli ni sauti ya kinabii, chombo cha huduma ya huruma na mapendo kwa waathirika wa vita huko Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati.

Watoto yatima, wagonjwa na wazee wameonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Katika shida na mahangaiko ya watu hawa wa Mungu, Baba Mtakatifu Francisko, ameendelea kuonesha uwepo wake wa karibu kwa hali na mali! Vita inayoendelea nchini humo kwa muda wa miaka mitano sasa, wala si kwa misingi ya kidini kama inavyoweza kuonekana kwa haraka haraka, bali ni njama za wajanja wachache wanaotaka kufaidika na rasilimali za nchi kwa manufaa yao binafsi. Wafanyakazi wengi wa Mashirika ya Kimataifa wameondoka nchini humo.

Haya yamesemwa hivi karibuni na Askofu Juan Josè Aguirre wa Jimbo Katoliki la Bangassou, katika mahojiano maalum na Vatican News, wakati alipokuwa anashiriki mkutano wa Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil. Utajiri wa madini na rasilimali mbali mbali zinazohitajika kama malighafi katika viwanda vya silaha na elektroniki, umekuwa ni balaa na janga kwa wananchi wa Afrika ya Kati. Vikundi vya Balaka na Seleka vinachezeshwa “Sindimba” wasiyoifahamu kwa kutumbukizwa katika vita na kinzani ambazo zimekuwa na madhara makubwa kwa maisha ya watu wengi!

Viongozi wa Kanisa na waamini katika ujumla wao, wanatembea na kifo mkononi, jambo la msingi ni kwa wananchi wote kutambua kwamba, wao ni ndugu wamoja, licha ya tofauti zao msingi ya kidini, kiimani na kiitikadi! Umoja, udugu na mshikamano ni kikolezo kikuu cha maendeleo, badala ya kung’ang’ania vita, kinzani na mipasuko ya kijamii ambayo kimsingi inawanufaisha watu wachache wenye uchu wa mali na madaraka! Askofu Juan Josè Aguirre anakaza kusema, wachochezi wa vita na vurugu wanaendelea “kula kuku kwa mrija” wakati wananchi wanaendelea kuteseka kwa umaskini, magonjwa na ujinga!

Umefika wakati wa kusimama kidete, kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kanisa litaendelea kutangaza na kushuhudia majadiliano ya kidini yanayofumbatwa katika huduma msingi kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Wapiganaji wa Seleka na Balaka, hawana budi kuweka silaha zao pembeni na kuanza mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Pili ni kuanza kujielekeza katika: uponyaji, msamaha na hatimaye, upatanisho wa kitaifa, ili kujenga umoja na mshikamano wa kitaifa, licha ya tofauti msingi zinazojitokeza kati yao. Wananchi wa Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, watambue kwamba, ulinzi na usalama wa raia na mali zao, uko pia mikononi mwao na kamwe wasiruhusu watu kutoka nje, kuja na kuwavuruga.

Wongofu wa shuruti na misimamo mikali ya kidini na kiitikadi ni mambo ambayo hayana mvuto wala mashiko kwa ustawi na maendeleo ya wengi. Askofu Juan Josè Aguirre anahitimisha mahojiano haya kwa kusema, umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu! Changamoto iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa kutembelea na hatimaye, kufungua Lango la Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu, iwe ni changamoto endelevu ya kujikita katika misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu nchini humo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.