2018-04-24 14:31:00

Papa Francisko: Waamini jiwekeni wazi kwa maongozi ya Roho Mtakatifu


Mateso na hatimaye kifodini cha Stefano Shahidi, lilikuwa kana kwamba, ni kosa lenye heri, kwa sababu Wakristo walitoka kifua mbele kwenda kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Habari Njema ya Wokovu ikawafikia watu wa Foinike, Kipro na Antiokia na hapo ndipo mahali ambapo kwa mara ya kwanza waamini waliitwa “Wakristo” yaani “Watu wa Kristo” kutokana na ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Jumanne, 24 Aprili 2018 amekazia umuhimu wa waamini kuwa huru mbele ya Roho Mtakatifu; kufikiri na kutenda kama watoto wa Mungu na kwamba, kwa njia ya sala na mang’amuzi katika maisha, waamini wanaweza kuona njia na upya wa maisha unaoletwa kwa njia ya Roho Mtakatifu.

Baba Mtakatifu amewataka waamini kuwa huru na wazi mbele ya Roho Mtakatifu na kamwe wasikubali kuwa ni wafungwa wa maneno yao! Wakristo wawe daima watu wanaomwachia nafasi Roho Mtakatifu ili aweze kuwafunda na kuwaongoza kadiri ya mapenzi yake, kwani, daima mwanadamu katika historia ya maisha yake ameonesha tabia ya kutaka kumpinga Roho Mtakatifu kwa kuwa na shingo ngumu, kwa kutokubali mageuzi. Waamini wakumbuke kwamba, Roho Mtakatifu anaendelea kutenda kazi katika Kanisa, kumbe, wawe tayari kukubali mageuzi yanayoletwa na Roho Mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwa kusema, watoto wa Mungu wanapaswa kuwa na tabia tofauti kabisa, inayowawezesha kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Roho Mtakatifu katika maisha na utume wao. Wakristo wa Kanisa la Mwanzo walikuwa wanyenyekevu mbele ya Roho Mtakatifu, wakakubali kubeba dhamana ya kwenda kutangaza na kushuhudia Neno la Mungu nje ya mapokeo yao, kiasi cha kuwa ni mvuto na mashiko kwa watu wengi waliosikia Habari Njema ya Wokovu ikitangazwa na kushuhudiwa mbele yao! Wakristo hawa waliweza kufanikisha dhamana hii kwa vile tu walikuwa ni wanyenyekevu mbele ya Roho Mtakatifu aliyewawezesha kutenda makuu. Hapa Baba Mtakatifu anasema, Kanisa lilikuwa liko katika harakati za kutoka katika undani wake, ili kutekeleza dhamana na utume wa kimisionari, daima likiendelea kuwa aminifu kwa maongozi ya Roho Mtakatifu. Kanisa linapaswa “kuchanja mbuga”, ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, ili kufanikisha azma hii, kuna haja kwa Wakristo kujiweka wazi mbele ya Roho Mtakatifu na kamwe wasikubali kupoteza dira na mwelekeo wa maisha. Daima wajitahidi kusali na kufanya mang’amuzi katika maisha yao na kwa njia ya Roho Mtakatifu, watafanikiwa kuona njia sahihi. Kwa kawaida kuna tabia ya binadamu kutaka kumwekea Roho Mtakatifu pingamizi katika maisha! Katika mazingira kama haya, waamini watambue kwamba, hapa kuna “mchezo mchafu” unaofanywa na shetani, Ibilisi, anayetaka kuwapokonya watoto wa Mungu, uhuru wa kweli unaowafungulia njia na maisha mapya. Nguvu na neema ya Roho Mtakatifu inawawezesha waamini kufanya mang’amuzi kwa kusoma alama za nyakati, ili hatimaye, kufanya maamuzi magumu katika maisha! Waamini wawe tayari kujiachilia chini ya maongozi ya Roho Mtakatifu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 
All the contents on this site are copyrighted ©.