2018-04-24 07:30:00

Mama Kanisa anapenda kuwahamasisha vijana kukimbilia huruma ya Mungu


Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Misericordia et misera” yaani “Huruma na amani” anawaalika waamini kuendelea kushuhudia na kumwilisha huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao, kwa njia ya Mafumbo ya Kanisa, hasa Liturujia na Sakramenti za Kanisa, Neno la Mungu, Matendo ya huruma kiroho na kimwili. Baba Mtakatifu anasema, Ekaristi Takatifu, Upatanisho na Mpako wa wagonjwa ni Sakramenti za huruma ya Mungu. Ni mahali pa kuonja upendo, toba, wongofu wa ndani na msamaha kwani huruma yake ni kuu na huvuka kila vikwazo na vizingiti katika maisha ya mwanadamu! Kwa njia ya huruma, waamini wataweza kumwilisha upendo katika maisha yao na hivyo kuwa ni sehemu ya vinasaba na utambulisho wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo!

Idara ya Toba ya Kitume, kwa kutambua umuhimu wa Sakramenti ya Upatanisho katika mchakato wa maisha ya vijana, imani na mang’amuzi ya miito, tema inayovaliwa njuga kwa sasa na Mama Kanisa katika maisha na utume kwa vijana, imeandaa kongamano la siku mbili, kuanzia tarehe 26-27 Aprili 2018. Kardinali Mauro Piacenza, Mhudumu mkuu wa Idara ya Toba ya Kitume atafungua kwa kutoa hotuba elekezi, kama sehemu ya mchakato wa maandalizi ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, itakayoadhimishwa, Mwezi Oktoba, 2018 hapa mjini Vatican.

Sakramenti ya Upatanisho ni muhimu sana katika safari ya maisha ya kiroho sanjari na mang’amuzi ya miito miongoni mwa vijana Wakristo. Ni katika Sakramenti ya Upatanisho, Mahakama ya huruma ya Mungu, mwamini anaonja huruma, upendo na msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu; ni mahali ambapo mwamini kutoka katika undani wake, anaguswa na kupyaishwa, huku akitiwa shime ya kusonga mbele katika hija ya maisha ya toba, wongofu na utakatifu. Watoa mada kutoka ndani na nje ya Kanisa, watajitahidi kupembua tema ya “Upatanisho” mintarafu mahusiano ya vijana katika nyanja mbali mbali za maisha. Hii itakuwa ni nafasi ya kudadavua hali kijamii na kitamaduni ambamo wanaishi vijana wa kizazi kipya. Wataoneshwa vishawishi vya maisha ya ujana, changamoto na vikwazo wanavyopaswa kuviepuka katika maisha ya kiroho na kimwili; tayari kupokea kwa imani na matumaini changamoto za maisha ili kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, Bwana na Mwalimu!

Hata leo hii, Kristo Yesu anaendelea kuzungumza na waja wake kwa njia ya Neno la Mungu pamoja na Kanisa. Vijana watapata fursa ya kusikiliza shuhuda ya watu waliotubu na kumwongokea Mungu katika hija ya maisha yao bila kusahau umuhimu wa Sakramenti ya Upatanisho katika hija ya maisha ya Kikristo! Vijana watashirikishwa pia mang’amuzi ya shughuli za kichungaji kama sehemu ya Mama Kanisa kuendelea kuwa ni shuhuda na chombo cha huruma ya Mungu kwa waja wake. Kanisa bado lina hamu ya kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma ya Mungu kwa waja wake. Hii ni mada itakayopembuliwa na Monsinyo Krzysztof Nykiel, Hakimu wa Idara ya Toba ya Kitume.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya 55 ya Kuombea Miito Duniani iliyoadhimishwa na Mama Kanisa, Jumapili ya Mchungaji mwema, tarehe 22 Aprili 2018 amasema, Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo, daima amekuwa akiwasindikiza waja wake hata katika njia ngumu za maisha yao, zinazosheheni mavumbi na matope. Anatambua fika kiu ya upendo iliyoko ndani mwao na hivyo anawaita kushiriki furaha yake. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kutafakari kwa kina mambo makuu matatu: kwanza kabisa: kusikiliza; pili, kufanya mang’amuzi ya miito na tatu ni kuishi upya wa maisha kama unavyopata utimilifu wake katika ufunuo wa Kristo Yesu. Mwenyezi Mungu, kamwe hachoki kuwaita vijana kufuata nyayo zake katika huduma kwa Mungu na jirani zao. Kwa bahati mbaya, vijana wanaishi katika dunia ambayo imegeuka kuwa kama tambara bovu!

Watu wamekosa dira na mwelekeo sahihi wa maisha; wamezeeka na kuchoka hata katika ujana wao kutokana na kubeba sana magumu ya maisha; watu wanageuziana kisogo na kupishana barabarani utadhani Merikebi baharini na kudhani kwamba, hii ni sehemu ya maisha ya kawaida tu kiasi hata cha kushindwa kuonja na kuwaonjesha wengine uzoefu wa ukarimu, kwani haya ni makovu na madhara ya dhambi! Katika mazingira kama haya, vijana wengine wamejikuta wakijutia maisha au kushikwa na woga; wamegubikwa na ubadiri wa maisha ya kiroho, kiasi kwamba Mwenyezi Mungu hana tena nafasi katika maisha na vipaumbele vyao. Idara ya Toba ya Kitume ni Mahakama ya huruma ya Mungu inayotaka kuwaonjesha vijana wa kizazi kipya umuhimu wa Sakramenti ya Upatanisho katika hija ya maisha yao ya kiroho ili kuwasaidia vijana hawa kupata huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.