2018-04-24 08:46:00

Askofu mkuu Jurkovic: Watu wana haki ya kupata maendeleo endelevu!


Askofu mkuu Ivan Jurkovič, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Geneva, hivi karibuni, katika hotuba yake kwenye mkutano kuhusu haki ya maendeleo ya watu anasema, kuna pengo kubwa la maendeleo kati ya maskini na matajiri duniani, ingawa kuna dalili za matumaini katika sera na mikakati ya utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030. Jambo la msingi kwa Jumuiya ya Kimataifa ni kuhakikisha kwamba, inayavalia njuga mambo yote yanayokwamisha mchakato wa maendeleo endelevu, ikiwa ni pamoja na kubadili miundo mbinu sanjari na kujikita katika kukuza na kudumisha haki msingi za binadamu.

Ili kufanikisha malengo haya, kuna haja kwa serikali mbali mbali kushirikiana kwa karibu zaidi, daima utu, heshima na haki msingi za binadamu zikipewa kipaumbele cha kwanza, ili kukuza na kudumisha: uhuru wa kweli na amani ya kudumu! Saratani ya rushwa ambayo ni kikwazo kikubwa cha maendeleo endelevu sehemu mbali mbali za dunia, haina budi kuvaliwa njuga kwa kudumisha haki za kiraia, kisiasa, kiuchumi, kijami na kitamaduni sanjari na kuhakikisha kwamba, rasilimali fedha inatolewa ili kuharakisha mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu!

Askofu mkuu Ivan Jurkovič anaendelea kufafanua kwamba, maendeleo endelevu yanapania kuboresha maisha ya mtu mzima: kiroho na kimwili; kwa kuwapatia watu fursa za maisha bora zaidi ili kukuza na kudumisha utu, karama na vipaji vyao, kadiri ya ujuzi na wito katika maisha. Usalama wa raia na mali zao ni jambo la msingi katika mchakato mzima wa maendeleo endelevu ya binadamu. Jumuiya ya Kimataifa haina budi pia kutekeleza dhamana na wajibu wake wa kuchangia maendeleo endelevu: kiuchumi na kijamii. Ili kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu, umaskini wa hali na kipato hauna budi kushughulikiwa kikamilifu na kamwe binadamu hasigeuzwe kuwa ni chombo cha uzalishaji mali na hutoaji wa huduma, bali mdau katika mchakato wa maendeleo endelevu.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, ili kuondokana na ubinafsi na uchoyo, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujikita katika mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa kulinda na kudumisha kanuni maadili na sheria; udugu na mshikamano, daima maskini na “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi” wakipewa msukumo wa pekee! Ni matumaini ya ujumbe wa Vatican kwamba, itifaki ya makubaliano ya Malengo ya Maendeleo Endelevu iliyofikiwa kunako mwaka 2015 itakuwa ni chachu ya kuendeleza ustawi na mafao ya wengi kama sehemu ya maboresho ya maisha ya binadamu katika medani mbali mbali. Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030 yanaweza kufanikiwa ikiwa kama sera na malengo haya yatatekelezwa kwa kuzingatia ukweli na usawa. Binadamu anakabiliwa na changamoto pevu za maendeleo endelevu, kiasi kwamba, anahitaji sera makini zinazoweza kujadiliwa na kutekelezwa na Jumuiya ya Kimataifa, kwa kutambua kwamba, changamoto za kujisadaka na utekelezaji wake ni kubwa, kuliko hata inavyofikiriwa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 

 
All the contents on this site are copyrighted ©.