2018-04-23 09:21:00

Papa Francisko: Mapadre iweni wenye huruma kama Kristo Mchungaji mwema


Baba Mtakatifu Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya 55 ya Kuombea Miito Duniani iliyoadhimishwa na Mama Kanisa, Jumapili ya Kristo Yesu Mchungaji mwema, tarehe 22 Aprili 2018, amependa kuwaalika waamini kutafakari kwa kina na mapana mambo makuu matatu: kusikiliza;kung’amua na kuishi upya wa maisha kama unavyopata utimilifu wake katika ufunuo wa Kristo Yesu, Mchungaji mwema. Ujumbe huu ni mwendelezo wa tafakari kwa ajili ya maandalizi ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana itakayotimua vumbi Mwezi Oktoba, 2018 hapa mjini Vatican, kwa kuongozwa na kauli mbiu: “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya Miito”. Mwenyezi Mungu daima anapenda kukutana, kutembea na kuambatana na waja wake ili kuzima kiu ya upendo inayowaka ndani mwao.

Baba Mtakatifu katika maadhimisho ya Jumapili ya Kristo Yesu mchungaji mwema, akiwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, ameongoza Ibada ya Misa Takatifu sanjari na kutoa Daraja takatifu ya Upadre kwa Mashemasi wa mpito 16 na kati yao 11 ni kwa ajili ya Jimbo kuu la Roma. Katika mahubiri yake, ametafakari kwa kina kuhusu Daraja Takatifu ya Upadre inayopata chimbuko lake kutoka katika Agano la Kale na hatimaye, kufikia utimilifu wake kwa Kristo Yesu, Kuhani mkuu na wa milele.

Yesu aliwateua Mitume kutoka miongoni mwa wafuasi wake, ili kuendeleza utume wake ndani ya Kanisa kama: Bwana, Mwalimu na Mchungaji mwema, aliyetumwa na Baba wa milele naye akawatuma Mitume na waandamizi wao, ambao wanaendelea kushirikiana, kushikamana na kufungamana katika huduma ya kikuhani kwa watu wa Mungu. Mapadre wapya waliowekwa wakfu, wanaendeleza dhamana na utume huu, ili kujenga na kuimarisha Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa na kwamba, watu wa Mungu ni Hekalu la Roho Mtakatifu. Mapadre wapya waliowekwa wakfu mintarafu Agano Jipya, wanatumwa na Mama Kanisa: kutangaza na kushuhudia Injili; kuwaongoza watu wa Mungu kama wachungaji wema na kwamba katika maisha na utume wao, wataadhimisha Mafumbo ya Kanisa na hasa zaidi, Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa.

Baba Mtakatifu amewakumbusha Mapadre wapya kwamba, wanapotekeleza dhamana na wajibu wao, watambue daima kwamba, wanashiriki katika utume wa Kristo, Bwana na Mwalimu. Wawe ni watangazaji na mashuhuda wa Injili ya furaha ambayo wao wenyewe wameipokea; wajitahidi kusoma na kulitafakari Neno la Mungu; ili kufundisha kile ambacho wamekisoma na kukitafakari; wafundishe na kushuhudia katika matendo imani wanayofundisha, ili harufu ya furaha ya maisha iweze kuwafikia wafuasi wa Kristo, ili kwa njia ya maneno na matendo yao adili waweze kuijenga na kuidumisha nyumba ya Mungu, ambalo ni Kanisa.

Mapadre waliowekwa wakfu, wataendeleza utume wa kuwatakatifuza watu wa Mungu, kwa kuadhimisha Sadaka ya Kristo pamoja na Mafumbo ya Kanisa. Baba Mtakatifu anawataka Mapadre wapya kutambua na kuiga kile wanachoadhimisha, kwani kwa njia ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, wanashiriki kifo na ufufuko wa Kristo; ambao wanapaswa kuwashirikisha na  kuwamegea ndugu zao katika Kristo, ili waweze kushiriki katika upya wa maisha na Kristo Yesu! Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, wataliwezesha Kanisa kupata watoto wapya wanaozaliwa kwa maji na Roho Mtakatifu. Kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho, watawaondolea waamini dhambi zao kwa niaba ya Mama Kanisa.

Hapa Baba Mtakatifu anawataka Mapadre wapya, kuwa ni wachungaji wenye huruma, kwa kutambua kwamba, hata wao katika maisha na utume wao, wanaweza kuogelea katika dimbwi la dhambi, lakini, Kristo Yesu, anawaganga na kuwaponya pale wanapomkimbilia kwa moyo wa toba na wongofu wa ndani. Kwa njia ya Mafuta ya Wagonjwa, Mapadre wapya watawafariji wagonjwa katika mahangaiko yao ya ndani. Maisha ya Mapadre, yapambwe kila siku kwa maadhimisho ya Mafumbo na Sala ya Kanisa, kama sauti ya watu wa Mungu na binadamu katika ujumla wake. Mapadre watambue kwamba, wametwaliwa kati ya watu kwa ajili ya watu mintarafu mambo matakatifu, changamoto mbele yao ni kuhakikisha kwamba, wanatekeleza dhamana na utume huu kwa furaha na upendo, daima wakipania kumpendeza Mungu kwa njia ya Kristo na wala si kwa ajili ya kujitafutia umaarufu au kutaka kuonekana mbele ya watu.

Mapadre wapya wajisadake bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa Mungu, ustawi na mafao ya watu wa Mungu. Kwa kushiriki katika utume wa Kristo, daima wajitahidi kujenga na kudumisha umoja na mshikamano na Askofu mahalia; kwa kuwaunganisha waamini, ili hatimaye, kuwapeleka kwenye Fumbo la Utatu Mtakatifu. Mbele yao, wamwone daima Kristo Yesu, mchungaji mwema, aliyekuja si kwa ajili ya kuhudumiwa, bali kuhudumia na kutoa maisha yake, ili kutafuta na kuokoa kile kilichopotea!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.