2018-04-23 09:47:00

Malezi ya Kipadre yazingatie: Utu, tasaufi na huduma makini!


Mwongozo wa Malezi ya Kipadre  unaojulikana kama “Ratio Fundamentalisi Institutionis Sacerdotalis”  yaani “Zawadi ya wito wa Kipadre” ni muhtasari wa mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa katika malezi na majiundo ya kipadre ambayo yanapaswa kupyaishwa, kuendelezwa na kupewa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa Mama Kanisa kwa kusoma alama za nyakati. Mwongozo wa sasa unazingatia na kukidhi mahitaji msingi ya malezi na majiundo ya Kipadre ili kuweza kukabiliana na changamoto za ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Ni mwongozo unaotoa mwelekeo na uwiano sahihi wa malezi: kiutu, kiroho, kiakili na kichungaji kwa njia ya safari ya malezi na majiundo makini ya Kipadre, taratibu, lakini kila jandokasisi akiangaliwa kwa jicho la pekee.

Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo linakabiliana na changamoto nyingi kati yake ni Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na mabadiliko makubwa katika maendeleo ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano. Kutokana na changamoto zote hizi, Kanisa limeona kwamba, kuna busara ya kuanzisha, kupyaisha na kutoa kipaumbele cha kwanza kwa malezi na majiundo ya Kipadre katika maisha na utume wa Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko kwa njia ya maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, amekuwa ni changamoto kubwa ya kuangalia tena mchakato wa malezi na majiundo ya maisha, wito na utume wa Kipadre ndani ya Kanisa kwa kuendelea kusoma alama za nyakati, changamoto iliyotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Hii inatokana na ukweli kwamba, Mapadre si watu wa mshahara, bali ni wachungaji wa familia ya Mungu, wanaopaswa kwa namna ya pekee, kuwa ni watu wasikivu, wenye huruma na upendo kama ilivyokuwa kwa Kristo katika maisha na utume wake. Aliwaonea watu huruma, akawasikiliza kwa makini, akawaganga na kuwaponya, akawasamehe dhambi zao na kuwapatia tena furaha ya kuendelea kuishi kwa imani na matumaini, kwani walikuwa wameonja na kukutana na Uso wa huruma ya Mungu katika safari ya maisha yao!

Baba Mtakatifu Francisko amekuwa akiwaonya Wakleri kuhusu kishawishi cha kumezwa na malimwengu kwa kuwa na uchu wa mali na madaraka kwani matokeo yake ni hatari katika maisha na utume wa Kipadre. Kwa bahati mbaya, kumejitokeza katika maisha na utume wa Kipadre kwa baadhi yao kutafuta utukufu binafsi kwa kupenda kujikweza sana; kuwa na shingo ngumu katika shughuli za kichungaji kwa kukazia sheria peke yake bila kuonesha hata chembe ya huruma na mapendo kwa watu wanaotubu na kukimbilia huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao!

Kumbe, majiundo na malezi makini ya Kipadre ni kiini cha maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko kwa wakati huu, ili kweli Kanisa liweze kuwapata Mapadre wema, watakatifu na wachapakazi wanaoweza kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Maaskofu wanawajibika sana katika malezi na majiundo ya Majandokasisi pamoja na wakleri wao kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo! Hapa mkazo ni kuwa na muungano kamili na endelevu wa majiundo na malezi ya Kipadre: kiutu, kiroho, kiakili na katika shughuli za kichungaji.

Malezi ya kiutu yanamtaka Jandokasisi kuwa na ukomavu na uwiano mzuri kati ya maisha ya kiroho na kiutu; mahusiano kati ya watu yanayojikita katika heshima na nidhamu. Bila ya kuwa na jicho la kichungaji, matatizo na changamoto zinazoweza kujitokeza katika maisha ya majandokasisi, yanaweza kuwa ni mzigo mkubwa kwa siku za baadaye kwa Padre mwenyewe na kwa ajili ya familia ya Mungu inayomzunguka. Hapa kuna haja ya kuwa makini katika kuwachagua majandokasisi wanaoweza kuingia Seminarini tayari kuanza safari ya maisha na wito wa Kipadre, vijana hawa wanapaswa kuangaliwa kwa kina na mapana katika safari yao, ili waweze kusaidiwa kikamilifu bila ya kuwa na haraka wala kuchukua mambo kijuu juu tu!

Hapa hakuna njia ya mkato, kila hatua inapaswa kushughuliwa kikamilifu pasi na haraka wala upendeleo, ili kuhakikisha ukomavu wa jandokasisi. Lazima kuwepo na malezi endelevu yanayomsaidia mseminari kupata mambo msingi katika maisha na utume wake wa Kipadre hapo baadaye. Kumbe, majiundo ya falsafa, taalimungu na shughuli za kichungaji yameboreshwa kwa kuongezewa tena majiundo ya kitume, utambulisho wa wito na utume wa Kipadre, ili kuweza kuwa na mwelekeo mkamilifu wa Yesu Kristo mchungaji mwema.

Padre mwema, mtakatifu na mchapakazi hapatikani kwa kufaulu vyema masomo na mitihani yake, bali anahitaji kuwa na ukomavu wa kiutu, maisha ya kiroho na shughuli za kichungaji. Awe makini na lugha anayoitumia katika maisha na utume wake bila kusahau mbinu msingi za malezi na majiundo. Mambo makuu mawili yamepewa kipaumbele cha kwanza: Utu”, yaani, waseminari wanapaswa kusindikizwa ili waweze kuwa na ukomavu katika utu wa binadamu, ili kweli waweze kupenda na kupendwa katika hali ya ukomavu; watu huru kutoka katika sakafu ya maisha yao; watu wanaoweza kujenga na kudumisha mahusiano ya kijamii; watu wenye amani na utulivu wa ndani; wanaoweza kutoa na kupokea na kumwilisha Mashauri ya Kiinjili katika maisha yao bila shuruti, unafiki wala kutafuta njia ya mkato.

Pili ni “Tasaufi” neno lililopewa kipaumbele cha pekee katika malezi na majiundo ya kipadre kwa kufunda dhamiri nyofu mintarafu maisha na wito wa Kipadre. Ikumbukwe kwamba, Padre si mfanyakazi wa mshahara wala mfanyabiashara anayelitumia Kanisa kwa ajili ya mafao yake binafsi. Padre ni mfuasi wa Kristo Yesu anayejisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake, kwa kujenga na kudumisha uhusiano wa pekee na Kristo kwa njia ya Neno, Sakramenti, Matendo ya huruma: kiroho na kimwili pamoja na sadaka binafsi, kielelezo cha Kristo mchungaji mwema. Mapadre wanapaswa kuboresha maisha yao ya kiroho yanayofumbatwa katika tunu msingi za Kiinjili kwa kujisikia kuwa na Kanisa kwa ajili ya Kanisa kama alivyokuwa Kristo Yesu.

Mapadre wanapaswa kuwa ni watu wa “Huduma” yaani “Wasamaria wema”, watu wenye huruma, upendo na msamaha. Hawa ni watu wanaopaswa kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikiliza kwa makini, kwani katika maisha na utume wao, watakutana na watu wenye kiu ya kusikilizwa; watu wanaweza kuanzisha na kudumisha mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi pasi ya kuwa na jazba au kutaka kulipiza kisasi. Ikumbukwe kwamba, ndani ya familia ya Mungu kuna watu ambao wamejeruhiwa vibaya wanapaswa kugangwa na kuponywa na huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya Sakramenti za Kanisa, ushauri makini na ushuhuda wenye mvuto na mashiko.

Majandokasisi wanapaswa kuondokana na tabia ya kujifungia katika ubinafsi wao, tayari kujielekeza katika mwono mpana utakaowapatia mang’amuzi ya kina katika maisha na utume wao kwa siku za baadaye, kama Mapadre! Baadhi yao wanaishi na kufanya kazi katika mazingira magumu na hatarishi, kumbe, wanahitaji kusindikizwa kwa njia ya sala na sadaka ili kamwe wasikate tamaa, hata pale wanapoteleza na kuanguka katika udhaifu wa kibinadamu wawe na ujasiri wa kusimama na kusonga mbele kwa imani na matumaini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.