2018-04-23 14:51:00

Changamoto za malezi na majiundo ya kikasisi nchini Tanzania!


Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi wa Jimbo kuu la Mwanza, Tanzania, katika mahojiano maalum na Vatican News anasema, maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania Bara yamekuwa yakienda sanjari na Jubilei ya Miaka 100 ya Upadre nchini Tanzania, iliyoadhimishwa mwaka 2017. Hii ilikuwa ni fursa kwa familia ya Mungu nchini Tanzania kuweza kutafakari kuhusu: wito, maisha, utume, changamoto, vikwazo, ukuu na utakatifu wa Daraja ya Upadre katika maisha na utume wa Kanisa. Mapadre wanashiriki katika utume wa Kristo kwa ajili ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu.

Itakumbukwa kwamba, Mapadre wa kwanza walipadrishwa kunako tarehe 15 Agosti 1917, ndiyo maana kilele cha maadhimisho haya kilifanyika Jimbo kuu la Dodoma, kunako mwaka 2017. Jimbo kuu la Mwanza, lilifunga Jubilei ya Mwaka wa Padre hapo tarehe 17 Desemba 2017 kwa tendo la shukrani kwa Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo kwa waja wake. Ilikuwa ni nafasi ya kuwakumbuka na kuwaombea mapadre wao neema, Baraka, afya njema ya roho ya mwili, sanjari na kuwaombea ari, mwamko na furaha katika wito na maisha yao ya kipadre. Jimbo kuu la Mwanza lilitoa pia Daraja ya Ushemasi wa mpito kwa majandokasisi watatu ambao bado wanaendelea kusikikiliza kwa makini kuhusu wito wao, kuupambananua, ili hatimaye, waweze kuuishi kadiri ya upya unaoletwa na Kristo Yesu. Mashemasi hawa ni zawadi ya Mungu kwa Kanisa linaloendelea kuhitaji watenda kazi: wema, watakatifu na wachamungu, kwa maneno mengine, mashuhuda wenye mvuto na mashiko kama sehemu muhimu sana ya mchakato wa uinjilishaji mpya.

Itakumbukwa kwamba, Seminari kuu ya Mtakatifu Agostino, Peramiho, Jimbo kuu la Songea, kunako mwaka 2017 imeadhimisha pia Jubilei ya Miaka 75 tangu ilipoanzishwa. Hiki kimekuwa ni kitalu cha kulelea na kukuzia miito kwa Kanisa la Tanzania. Familia ya Mungu nchini Tanzania inaendelea kuio mbea heri na baraka Seminari kuuu ya Peramiho ili iweze kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa Kanisa ndani na nje ya Tanzania. Hii ndiyo sala pia inayoelekezwa kwenye seminari na nyumba za mashirika ya kitawa na kazi za kitume huko Njiro, Jimbo kuu la Arusha, Chuo Kikuu cha Yordan, Jimbo Katoliki la Morogoro, Seminari kuu ya Wasalesiani wa Don Bosco, Njiro, Jimbo kuu la Arusha.

Jukumu la Seminari ni kulea mapadre kwa ajili ya Kanisa, moja, takatifu katoliki na la mitume! Hii inatokana na ukweli kwamba, Mapadre wote wanashiriki Ukuhani mmoja wa Kristo Yesu, kila mmoja kadiri ya karama na tunu alizokirimiwa na Mwenyezi Mungu. Askofu mkuu Ruwaichi anasema, Mapadre wanapaswa kutumia vyema tunu na karama hizi kwa ajili ya kulihudumia Kanisa kwa tija, weledi, ari na moyo mkuu, ili hatimaye, kumfanya Padre mwenyewe aaminike na kufurahia utume wake katika Kanisa. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linatambua changamoto, matatizo na fursa zilizopo katika malezi ya awali na endelevu kwa wakleri wake na kwa ajili ya mahitaji ya Kanisa la kiulimwengu. Kanisa la Tanzania limeanza kujielekeza zaidi katika kutengeneza Mwongozo wa Malezi ya Kipadre Kitaifa; kwanza kabisa kwa kuwekeza katika malezi na majiundo makini ya walezi; kwa kuhakikisha kwamba, Kanisa la Tanzania linakidhi walau mahitaji ya walezi seminarini! Hawa ni watu wanaofaa, wenye ujuzi, maarifa, weledi na ukarimu katika kukuza na kupalilia miito ndani ya Kanisa. Ni watu ambao wako tayari kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Baraza la Maaskofu linaendelea kuandaa programu zitakazokidhi: hali na changamoto mamboleo ndani na nje ya Tanzania mintarafu malezi na majiundo ya kipadre.

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linaendelea kuhimiza malezi makini na endelevu ya majandokasisi kuanzia kwenye ngazi ya familia, taasisi za elimu, Kanisa na jamii katika ujumla wake. Dhamana hii inapaswa kutekelezwa kwa uthibiti na ustawi ili kumwezesha kijana kukua huku akiwa na uwiano mzuri wa tabia, nafsi, imani, maadili na utu wema unaodaiwa kwa watu wanaojisikia kuwa na wito wa kuwa Mapadre wa Kristo katika Kanisa lake. Uwiano huu unapaswa kuwa ni vigezo muhimu katika maisha ya kiroho, ili kufanyiwa kazi kwa kuzingatia sera na mikakati inayomwezesha kijana kupambanua wito wake, kwa uangalifu, uchaji, weledi na pia kwa kulijali Kanisa na ukuaji wa mtu mzima: kiroho na kimwili.

Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi anakaza kusema, viongozi wa Kanisa nchini Tanzania wanatambua changamoto nyingi zilizoko kwenye malezi, wito na maisha ya kipadre. Lakini, hata walezi wanao wajibu mkubwa wa kutambua vipaji na kuwekeza katika stadi maalum, kwani yote haya ni sehemu ya mchakato wa toba na wongofu wa ndani kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Malezi makini, yalenge kumjenga na kumwimarisha padre anayekuwani “Kristo mwingine” ili kijana anapohitimu masomo na kuonekana walau anafaa kupewa Daraja Takatifu ya Upadre, awe ni faraja, shuhuda na nabii wa Kristo Yesu, ambaye ndiye Kuhani halisi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.