2018-04-22 15:05:00

Papa:Kwa mara nyingine tena Injili inatualika kufuata Yesu Mchungaji mwema!


Liturujia ya Domenika ya nne ya Pasaka inaendelea na lengo la kutusaidia kugundua utambulisho wetu wa kuwa mitume wa Bwana Mfufuka. Katika somo la Matendo ya Mitume, Petro anawatangazia wazi kwamba, uponyeshaji wa kiwete aliofanya huko Yerusalem umetokea kwa jina la Yesu, kwasababu hakuna wokovu uletwao na mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.(4,12). Katika undani wa yule mtu aliye ponywa, tupo hata sisi yaani kila mmoja wetu na jumuiya zetu; na kila mmoja anaweza kuponyesha kila aina ya magonjwa ya kiroho, hanasa, uvivu, kiburi, lakini akikubali kuweka matumaini yake katika mikono ya Bwana Mfufuka. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, anasisitiza Petro, yupo mbele yenu aliyeponywa. Lakini  Kristo anayeponyesha ni nani? Ni jambo gani la kuponyeshwa na Yeye? Na kwa namna gani?

Huo ni utangulizi wa Mahubiri ya Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu, kwa mahujaji na waamini waliofika katika viwanja vya Mtakatifu Petro Mjini Vatican tarehe 22 Aprili 2018, ikiwa ni Jumapili ya Kristo Mchungaji mwema na ambayo inakwenda sambamba na Siku ya Kuombea Miito Duniani. Baba Mtakatifu akiendelea na mahubiri anasema: Jibu la maswali yote hayo yanapatikana katika Injili ya leo, mahali ambapo Yesu anasema: “Mimi ni mchungaji mwema”. Mchungaji mwema ajua maisha ya kondoo wake “(Yh 10,11) Kujitangaza kwake Yesu namna hiyo, hauwezi kupunguzwa kwa hisia tu, bila kuwa na matokeo ya dhati! Yesu anaponya kutokana na kwamba ni mchungaji anayetoa maisha, kwa ajili ya watu na ambaye anamwambia kila mtu kwamba “maisha yako yana thamani kubwa kwangu na ili kuyaokoa, ninajitoa mimi  mimi mwenyewe kwa ajili yako”.

Ndiyo maana tendo la kujitoa maisha yake, linamfanya awe kweli Mchungaji mwema kabisa, ambaye anaponya na kukufanya uweze kuishi maisha mema na kuzaa matunda.  Sehemu ya pili katika Injili inaonesha hali ambayo Yesu anaweza kuponyesha na kufanya maisha yawe ya furaha na kutoa matunda. Sehemu hiyo ni “mimi ni mchungaji mwema, ninajua kondoo wangu na kondoo wangu wanijua, kama vile Baba anijuavyo, nami nimjuavyo Baba” (Yh 10,14-15).

Yesu hazungumzii juu ya ufahamu wa kiakili, bali ni kuhusu mahusiano binafsi ya , uchaguzi, ya ukarimu na upamoja, unaoangaza uhusiano wa ndani ya upendo kati yake na Baba. Hiyo ndiyo tabia ambayo inakamilisha mahusiano hai,  binafsi ya Yesu, yaani kujiachia utambuliwe na yeye. Yeye ni makini kwa kila mtu, anafahamu kwa kina mioyo yetu. Anatambua uwezo,  hata makosa yetu, mipango yetu tuliyoitenda na matumaini ambayo hayakamiliki. Lakini anatukubali jinsi tulivyo na kutuongoza kwa upendo, kwasababu tunaweza kupitia njia hata iliyo ngumu lakini bila kuipoteza.

Baba Mtakatifu amehitimisha akisema kuwa: ni kwa mara nyingine tena  tunaalikwa kumjua Yesu. Na hiyo inalazimisha kukutana naye na kuwa na shauku ya kuacha yote ili kumfuasa na kutembea katika njia mpya, zilizo elekezwa na yeye mwenyewe na  zilizofunguliwa katika upeo mkubwa.  Iwapo katika jumuiya zetu kuna ubaridi wa shauku ya kuishi na uhusiano na Yesu, kusikiliza sauti yake na kumfuata kwa uaminifu, ni wazi pakatokea mambo mengi ya kufikiria na kuishi bila udhati wa Injili! 

Sr Angela Rwezaula 
Vatican News








All the contents on this site are copyrighted ©.