2018-04-21 08:30:00

Siku ya Mama Dunia kwa Mwaka 2018: Sitisha uchafuzi wa mazingira!


Siku ya Kimataifa ya Mama Dunia ilianzishwa kunako mwaka 2009 na Umoja wa Mataifa, na inaadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 22 Aprili ili kutoa nafasi ya kutafakari kwa kina na mapana umuhimu wa kuitunza Mama Dunia kwa ajili ya mafao ya wengi. Kauli mbiu  kwa mwaka 2018 ni “Sitisha uchafuzi wa mazingira kwa plastiki”. Hii pia ni fursa muhimu ya kutanabaisha uhusiano tegemezi na mkamilishano uliopo kati ya viumbe hai mintarafu mwanga wa Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” kama unavyopembuliwa na Askofu mkuu Ivan Jurkovic, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Geneva.

Askofu mkuu Jurkovic anasema, Waraka wa Baba Mtakatifu Francisko “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” umesheheni utajiri mkubwa wa imani na mapokeo ya kidini pamoja na ushauri wa kisayansi unaoweza kufanyiwa kazi katika ngazi mbali mbali kuanzia kwa watu binafsi, vyama vya kiraia, serikali na mashirika ya kimataifa ili kukuza na kuimarisha mchakato wa maendeleo endelevu, usawa pamoja na kuzingatia haki msingi za binadamu. Utenzi wa huu wa Mtakatifu Francisko wa Assisi unafafanua mwingiliano uliopo kati ya maumbile, haki kwa ajili ya maskini na amani ya ndani.

Baba Mtakatifu anapenda kuuliza swali la msingi “Je, ni ulimwengu wa namna gani tunataka kuwachia watakaokuja baadaye? Hapa changamoto ni kuhakikisha kwamba, watu wanatambua maana na lengo la maisha, ili kuibua mbinu mkakati wa utunzaji bora wa mazingira kwa sasa na kwa siku za usoni! Maskini ndio waathirika wakuu wa athari za mabadiliko ya tabia nchi na kumbe, umefika wakati wa kusikiliza kwa makini kilio chao na kuanza kujikita katika mchakato wa wongofu wa kiekolojia sanjari na kuwajibika barabara katika utunzaji wa nyumba ya wote na kwamba, kuna uwezekano mkubwa wa kuanza upya kwa kujenga na kudumisha uhusiano mwema na Mwenyezi Mungu, jirani pamoja na mazingira.

Athari za uchafuzi mkubwa wa mazingira zinagusa medani mbali mbali za maisha ya binadamu hali inayohitaji sera na mikakati itakayosaidia kupambana na umaskini, kwa kurejesha utu na heshima ya binadamu pamoja na kuendelea kujizatiti katika utunzaji bora wa mazingira. Maendeleo ya sayansi na teknolojia hayana budi kusaidia mchakato wa kulinda, kutunza na kudumisha mazingira bora zaidi; kwa kuwa na ugavi na matumizi sahihi ya rasilimali za dunia, kwani kuna hatari kubwa kwamba, matumizi mabaya ya nishati za dunia yanaweza kupelekea kukauka kwa rasilimali hizi na hivyo madhara yake yatakuwa ni makubwa sana kwa familia ya binadamu!

Utandawazi wa mfumo wa teknokrasia unaotoa kipaumbele cha kwanza kwa teknolojia inayotafuta faida kubwa zaidi kiasi hata cha kuhatarisha ustawi, maendeleo na haki msingi za binadamu. Kwa kawaida, teknokrasia ina mwelekeo tenge kuhusu maisha, utu, heshima na haki msingi za binadamu! Baba Mtakatifu anasema, uhakiki wa fikra potofu ya mwanadamu haupaswi kupuuza umuhimu wa mahusiano kati ya watu na kwamba, kinzani na migogoro ya kiekolojia ni dalili za kumong’onyoka kwa tunu msingi za kitamaduni, kimaadili na maisha ya kiroho.

Huu ndio mwelekeo wa baadhi ya watu katika jamii kuwatumia wenzao kama vyombo kwa ajili ya faida binafsi, kwani hapa watu wanataka kuuona ukweli kwa mtazamo binafsi. Mwenyezi Mungu, binadamu na mazingira ni mambo yanayotegemeana na kukamilishana. Ni katika mwelekeo huu, utu wa binadamu unaweza kulindwa, kukuzwa na kudumishwa mintarafu ekolojia endelevu inayofumbatwa katika: haki, sheria kanuni msingi ya maadili jamii na utu wema. Yote haya yanapania kukuza na kudumisha mafao ya wengi mintarafu mshikamano unaoongozwa na kanuni auni na maadili, ili kulinda utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, ili aweze kufikia utimilifu wake! Familia inapaswa kuwa ni kini cha jamii. Mafao ya wengi yanadai amani, utulivu na usalama kwa kuzingatia haki mgawanyo.

Kutokana na utajiri wote huu unaofumbatwa kwenye Waraka wa Kitume wa “Laudato si” Askofu mkuu Ivan Jurkovič anasema, Baba Mtakatifu Francisko, analiangalia suala zima la utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote katika mwanga wa kanuni maadili jamii, ili kuwasaidia watu kubadili mtindo, kanuni na taratibu za maisha zinazowatumbukiza katika ubinafsi na uchoyo, kwa kujikita zaidi katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu ni mambo yanayopewa msukumo wa pekee katika Waraka huu unaotoa changamoto pia ya wongofu wa kiekolojia, kama njia ya kudumisha mahusiano ambayo yanategemeana na kukamilishana. Binadamu na mahitaji yake msingi awe ni kipimo cha maamuzi ya kimaadili kuliko kuegemea zaidi maamuzi ya kiuchumi yenye kutafuta mafao binafsi, ili kulinda na kudumisha haki msingi za binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.