2018-04-20 07:00:00

Kristo Yesu ni kielelezo cha mchungaji mwema anayesadaka maisha yake!


Mpendwa msikilizaji wa Vatican News! Leo ni Dominika ya Kristo Mchungaji Mwema ambapo mama Kanisa anatualika kuiombea miito mitakatifu. Kristo Mchungaji Mwema anajidhihirisha katika uhai wa kundi analoliongoza. Hii inamaanisha kwamba Mchungaji mwema ameungana na kondoo zake na kondoo hawa ni sehemu muhimu ya maisha yake. Kuondoa mmoja wa kondoo zake ni sawa na kuitoa sehemu ya muhimu ya uhai wake lazima atahangaika hadi kumrudisha. Ni kama vile mmoja anavyopambana katika matibabu kwa ajili kurudisha utimamu anapokuwa mgonjwa. Ndivyo nasi tunavyoalikwa katika miito miito yetu mbalimbali kujifananisha na Kristo Mchungaji Mwema na hivyo huduma zetu kwa ndugu zetu zidhihirishe uwepo wake kati ya jamii ya mwanadamu.

Katika somo la kwanza Mchungaji Mwema amejionesha kama jiwe kuu la pembeni. Hii inamaanisha kwamba ni yeye anayeshikilia uimara wa kundi lake; kwa mafundisho yake, kwa uponyaji wake na kwa kuwamiminia neema kutoka mbinguni. Hivyo daima yupo na kundi lake na kukosekana kwake ni sawa na maangamizi kwa kundi. Ingawa alidharaulika na watu wa ulimwengu, wakiwakilishwa na Wayahudi lakini yeye ambaye ni “Jiwe walilolikataa waashi, Limekuwa jiwe kuu la pembeni”. Yupo tofauti na mchungaji wa kuajiriwa ambaye “kondoo si mali yake…huwaacha kondoo na kukimbia; na mbwa-mwitu huwakamata na kuwatawanya”. Kondoo ni mali ya mchungaji mwema, daima anakaa nao kama Jiwe kuu la pembeni na msingi wake thabiti!

Huduma na utumishi wetu kwa wenzetu inapata ufanisi pale tunapoona kuwa tukifanyacho ni sehemu muhimu si kwa uwepo wangu au ni sehemu muhimu kwa si uhai wangu tu bali hata kwa wale ninaowahudumia; pale tutakapoweza kubadili mawazo ya kutumia nafasi mbalimbali tulizonazo kwa ajili ya kujinufaisha binafsi na hivyo kutafuta kujinufaisha wote. Ni hali ya kuwa tayari kujifunua na kuwaangalia wengine walio pembeni yangu; hali ya kuona kuwajibika kwa mwenzangu kwa sababu yu sehemu muhimu na anayeleta maana ya uwepo wangu. Ni hatua muhimu kuelekea undugu wa kikristo ambao Kristo anakuwa kwetu ndugu yetu wa kwanza na katika yeye sote tunafanywa kuwa ndugu.

Mchungaji mwema hufungua mlango wa moyo wake kuangalia watu wote. Si wale wa kundi lake tu: “Na kondoo wengine ninao, ambao si wa zizi hili; na hao nao imenipasa kuwaleta; na sauti yangu wataisikia; kisha kutakuwako kundi moja na mchungaji mmoja”. Kabla ya mstari huu Kristo alianza kwa kusema kwamba anawajua kondoo zake nao wanamjua. Hii inathibitisha umoja kati ya mchungaji na kondoo. Lakini hiki anachoongezea kinaonesha kwamba hata walio nje ya kundi lake wanaisikia sauti yake na kwa namna hiyo kunakuwa na umoja kati ya kondoo wote. Sauti yake mchungaji mwema inawaunganisha wote kuwa kitu kimoja. Hakika huyu mchungaji ni sababu ya umoja kwa wanadamu wote.

Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican umezungumzia namna ambavyo wasio wakristo nao wanavyopewa nafasi ya kushiriki wokovu ulioletwa kwa njia ya Kristo. Pamoja na kwamba Kanisa kimuundo na kiutendaji linaonekana kukasimiwa katika Kanisa Katoliki chini ya Halifa wa Petro na maaskofu wanapokuwa katika umoja naye, “viashiria vya utakatifu na ukweli vinapatikana hata nje ya mipaka yake” (Lumen Gentium, 8) Ni maelezo mazuri ya kuimarisha juhudi mbalimbali za kikanisa za kukuza mazungumzano baina ya dini mbalimbali na mazungumzano ya kiekumene. Ukuu wa Ukombozi uletwao na Kristo unaenea kwa watu wote. Kwa imani inayodhihirika sisi tulio wakristo tunaonesha kuisikia na kuifuata sauti ya Kristo. Ila kwa upande mwingine wapo wanaoisikia kwa kutenda yale aliyokusudia kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu. Hii ni ishara muhimu ya umoja kati ya wanadamu uletwao na Kristo Mchungaji Mwema.

Mtume Yohane katika somo la pili anatupeleka hatua moja mbele. Kristo Mchungaji Mwema aliutwaa ubinadamu wetu na hivyo kwa fumbo la Umwilisho nasi tunafanyika kuwa wana wa Mungu. Ni tendo la upendo mkubwa wa Mungu kwetu. Hivyo nasi tunafanywa kwa namna fulani kuwa kama Yeye Mchungaji Mwema au jiwe Kuu la pembeni. Hapa ndipo tunapoona wito wetu ambao unajikita katika fumbo zima la Kristo Mfufuka. Kwa namna nyingine hapa tunaona muunganiko wa Dominika hii na jukumu la kuiombea miito. Zawadi hii ya kufanyika kuwa wana wa Mungu kimantiki inaathiri pia utendaji wetu. Bila shaka utajimithilisha na Yeye ambaye kwa njia yake tunafanyika kuwa wana wa Mungu, yaani Kristo Mchungaji mwema. Hivyo, ni vema kujitafakari vyema katika sauti ya Mungu inayoita na kuitikia vema kusudi kuleta matunda yanayotarajiwa na Yeye anayetuita.

Katika ujumbe wake wa Siku ya 55 ya Kuombea Miito Duniani kwa Mwaka 2018 Baba Mtakatifu Francisko anatutia moyo katika kuitikia miito yetu mbalimbali kama mtu mmoja mmoja na kama Kanisa kwa ujumla bila kuhofu kufunikwa na vurugu au “sintofahamu” za jamii mamboleo. Baba Mtakatifu ametukumbusha kwamba maisha yetu ni matunda ya wito wa Mungu. Fumbo la umwilisho limemleta Kristo kati yetu wanadamu na yeye aliye Mchungaji Mwema anaufanya hai kila siku ukaribu kati yetu na Baba na hivyo tunakutana naye mara kwa mara. Hivyo “katika tofauti na upekee wa kila mwito, kwa mtu binafsi na kama Kanisa, kuna haja ya kusikiliza, kutambua na kuishi neno hili ambalo linatuita kutoka juu na huku kutuwezesha kuendeleza vipaji vyetu, hutufanya vyombo vya wokovu ulimwenguni na kutuongoza kwa furaha kamili”. Matendo hayo matatu ya kusikiliza, kutambua na kuishi ni muhimu katika kuutimiza wito wa Mungu.

Kristo Mchungaji Mwema aliuanza utume wake wa hadhara kwa kuyatimiza vema matendo hayo na kuwa kielelezo kwetu tulio kundi lake. Baada ya tukio la kufunga na kusali kwa siku arobaini, Baba Mtakatifu Francisko anatukumbusha jinsi alivyoingia hekaluni na kuanza kwa kusikiliza Neno la Mungu kisha akatafakari ni nini ambacho Mungu amemtuma na baada ya kutambua ndiposa akaanza kuishi yaani kuitangaza habari njema ya wokovu ambayo imetufikia hata sisi hadi leo (Rej Lk 4:16 – 21). Katika jamii mambo leo iliyogubikwa na makelele mengi kiasi cha kutotoa fursa kuisikiliza sauti ya Mungu inayoita kwa njia ya Roho Mtakatifu, Baba Mtakatifu anatuasa kujitafutia fursa za tafakari na kuisikia sauti ya Mungu; katika ulimwengu ambao umejaa mawazo yenye tabia hasi na yanayopingana na ukweli Baba Mtakatifu anatualika katika utambuzi wa kiroho ili kuutambua wito wetu wa kikristo wenye haiba ya kinabii, unabii ambao unaoifunua sauti ya Mungu iliyojaa ukweli; na mwisho utambuzi wa wito huo utatutuma kwenda kuuishi kwa kazi za uinjilishaji kwa kuutangaza na kuuishi ukweli wa Injili katika ulimwengu mamboleo.

Kristo Mchungaji Mwema ni kielelezo, chanzo na uhai wa wito huo. Yeye aliye Njia, ukweli na uzima (Rej Yoh 14:6) anatuonesha jinsi nasi tunavyopaswa kuwa kama Yeye katika kutekeleza majukumu yetu mbalimbali tuliyokasimiwa kadiri ya wito wa Mungu. Kwanza kwa kuwa tayari kujitoa kwa ajili ya unaowahudumia. Ni wito kwa viongozi wa kada zote kuiga mfano wake; zaidi anaonesha kwa kuwajua watu wake, yaani, mahitaji yao, vipaji vyao, udhaifu wao na hivyo kila mmoja atawaongoza kwa namna yake mahsusi. Yeye pia ni chanzo kwani ni ufunuo wa Mungu kwetu; tunapoitikia wito wetu tunapaswa kuchota kutoka kwake yale tunayopaswa kuyatekeleza; tunapaswa kuisikiliza sauti yake. Lakini pia Yeye ni uhai wa kondoo wake. Anakuwa ni nguvu ya kuwaongoza wengine kufikia ukamilifu. Hivyo Yeye aliye Mchungaji mwema anatuita sisi kuitikia miito yetu mbalimbali, kila mmoja kwa kadiri yake na kumwakilisha Yeye kwa kujimithilisha katika haiba yake ya Mchungaji Mwema. Kwa njia hiyo tutashiriki nasi katika kuuokoa ubinadamu.

Mimi ni Padre Joseph Peter Mosha

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.