2018-04-20 15:15:00

Jumapili ya Kuombea Miito Mbali mbali ndani ya Kanisa!


Utangulizi: “Mimi ndimi mchungaji mwema, nao walio wangu nawajua; nao walio wangu wanijua mimi” karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika tafakari ya Neno la Mungu kwa dominika ya nne ya Pasaka. Dominika hii ambayo Kristo anajitambulisha kuwa ndiye mchungaji mwema imekuwa ni dominika ambayo Kanisa linaadhimisha siku ya Miito Duniani. Kiini cha siku hii ni kuitikia agizo la Kristo mwenyewe aliposema “mwombeni Bwana wa mavuno apeleke watendakazi shambani mwake” (Mt.9:38, Lk 10:2). Siku hii Kanisa huiombea kwa namna ya pekee miito ya Upadre na Utawa wa aina zote na kumwomba mwenyezi Mungu aendelee kuwaita wengi, awasindikize aliowaita na awaimarishe aliowapokea katika miito hii kwa ajili ya kueneza ufalme wake na kwa ajili ya sifa na utukufu wa Jina lake.

Masomo kwa ufupi: Somo la kwanza (Mdo. 4:8-12) Mitume Petro na Yohane wanaitwa mbele ya Baraza la Wayahudi na kuhojiwa kwa nini wanahubiri juu ya Yesu na juu ya ufufuo wa wafu. Wakiwa katika Baraza hilo, ambalo ndilo lilikuwa baraza la juu kabisa lililokuwa na mamlaka katika masuala ya kidini, kisiasa na kijamii kama mahakama, Petro anazidi kuongea juu ya Yesu na mojakwamoja analiambia baraza kuwa lilimsulubisha mtu asiye na hatia ambaye sasa amefufuka na ndiye anawapa nguvu za kutenda maajabu. Ndiye “jiwe lililokataliwa na waashi ambalo sasa limekuwa jiwe kuu la pembeni”. Zaidi ya hayo anawaalika nao kulikiri Jina la Yesu kwani “hakuna jina lingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu kwa ajili ya wokovu isipokuwa jina la Yesu”. Somo hili linatoa picha ya upinzani ambao Kanisa tangu mwanzo kabisa limekutana nao. Hapo hapo somo linatoa pia picha ya ujasiri na uthabiti wa wale wanaosimama kwa jina la kanisa ili kuendeleza utume wake; ndio mitume na waandamizi wao katika ngazi mbalimbali za huduma.

Somo la pili (1Yoh. 3:1-2). Mojawapo ya matunda ya Tukio la Kipasaka (Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo) ni kufanyika wana wa Mungu kwa wote wanaomwamini Kristo. Mtume Yohane, katika somo hili, anafafanua juu ya huko “kuwa mwana wa Mungu”. Kwanza anatofautisha hatua mbili: hatua ya mwanzo - ya hapa duniani -  ambapo mtu anapokea imani ya kikristo na hatua ya mwisho - ya mbinguni - ambapo mwamini anapokea ukamilifu wa kuwa “mwana wa Mungu”. Ni hatua hiyo ya ukamilifu ambayo anasema tutafanana na Mungu na tutamwona kama alivyo.

Mtume Yohane anaeleza pia kuwa hadhi ya “kuwa mwana wa Mungu” ni upendo mkubwa sana anaotupa Baba. Na ni kitu ambacho ulimwengu - wasiomwamini - hautambui. Somo hili pia kama lile la kwanza linaonesha ukinzani uliopo kati ya “wana wa Mungu” na “ulimwengu”. Ulimwengu unaelezwa kuwa hauelewi thamani ya upendo mkuu wa Mungu na haulewi hadhi ya waamini iliyo hadhi ya “wana wa Mungu”. Somo la Injili (Yoh. 10:11-18) Yesu anatoa mafundisho kwa njia ya “mfano” ambapo anajieleza mwenyewe kuwa ndiye mchungaji mwema. Ni mfano ambao anaujenga katika mazingira ya kiyahudi ya ufugaji yanayoeleza mahusiano ya mchungaji na kundi la mifugo analolichunga.  Ambapo ni kawaida kukuta mmiliki wa mifugo anaajiri mtu wa mshahara kuchunga mifugo yake na ni kawaida pia mmiliki mwenyewe wa mifugo kuichunga mifugo yake.

Yesu analizungumzia kundi la watu wa Mungu kama kondoo; watu wanaomtegemea Mungu na wanaojiweka daima chini ya maongozi yake. Katika kundi hilo, Kristo anajipambanua kuwa ndiye mchungaji mwema ambaye anawachunga vema kondoo wake. Kwanza, anawajua: anawaangalia kwa macho ya huruma, yuko karibu nao na kila mmoja wao kadiri ya mahitaji yake ya pekee. Pili, anawapa uhai kondoo: anawakinga dhidi ya maadui mbalimbali wanaowazunguka na Tatu yuko tayari kuutoa uhai wake kwa ajili yao. Na hili amefanya kwa kifo chake Msalabani.

Katika mfano huu, kwanza Yesu anawazungumzia Viongozi wa dini ya kiyahudi ambao walikabidhiwa kundi la waana wa Mungu ili waliandae kumpokea Masiha mkombozi wao. Wao badala ya kuliandaa kundi, kuliandalia malisho, walichukua tabia kama ya watu wa mshahara ya kutanguliza maslahi yao na kulinda nafasi zao kiasi kwamba Masiha alipokuja hawakumpokea na hivi wakalinyima kundi walilokabidhiwa nafasi ya kumpokea Masiha. Aidha Yesu katika mfano huu pia anajitambulisha kuwa ndio mfano sasa wa wote wanaokabidhiwa kundi la waana wa Mungu kama viongozi wa Kiroho. Wawe wachungaji kweli kwa mfano wake Yeye Mchungaji mwema.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, Kanisa linapomtafakari Kristo anayejipambanua leo kama mchungaji mwema, linapata nafasi ya kuadhimisha siku ya miito, kwa namna ya pekee wito wa upadre na wito wa maisha ya wakfu. Hii ni miito ambayo vijana - wake kwa waume huitikia ili kumfuata Kristo kwa karibu zaidi na kumtumikia wakifuata ukamilifu wa mapendo. Wanaoitikia na kupokea upadre huunganishwa na Kristo mwenyewe na kushirikishwa hadhi na kazi zake za kikuhani, kinabii na kifalme, ndio uchungaji kwa kundi analowakabidhi.

Awali ya yote tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya miito hii. Kwa namna ya pekee sisi Kanisa la Tanzania tunaoadhimisha Jubilei ya Miaka 150 ya Kanisa Katoliki Tanzania bara, tunatambua kuwa kuwepo, kusambaa na kushamiri kwa imani Katoliki Tanzania bara ni kwa sababu ya uwepo wa miito hii nchini kwetu na kwa sababu ya ushuhuda wa miito hii ambayo ndugu zetu mapadre na watawa wameutoa katika kipindi hicho chote.  Kama walivyotukumbusa Maaskofu wetu katika Ujumbe wa Kwaresima mwaka huu wa 2018 juu ya “uinjilishaji mpya... na juu ya kujenga roho ya umisionari katika kumshuhudia Kristo kwa maneno na matendo yetu popote tulipo” yatupasa kukiri kuwa ushuhuda wa miito ya upadre na utawa unaoakisi sura ya Kristo Mchungaji mwema hauwezi kutengwa na azma hiyo. Ndiyo maana siku ya leo tunaalikwa kuwaombea wanaoitikia miito hii ili katika utume na maisha yao yote wamtangulize Kristo na Yeye aendele kuwatumia japo ni vyombo dhaifu kwa ajili ya huduma na wokovu kwa watu wake.

Baba Mtakatifu Francisko katika kuadhimisha siku ya leo anatupatia ujumbe unaokazia mambo matatu kwenye safari nzima ya miito hii mitakatifu. Mambo hayo ni Kusikia, Kung’amua na Kuishi. Mungu ndiye mmiliki wa miito yote naye huwaita kadiri ya mapenzi yake wale aliowakusudia kwa huduma yake. Lakini si mara zote walioitwa huitikia. Ndiyo maana Papa Francisko anatualika kujifunza kusikiliza sauti ya Mungu anayeita. Anaeleza kuwa katika mazingira tuliyomo kuna hatari ya kutokuisikia sauti ya Mungu anayeita kwa sababu zipo “kelele” nyingi zinazoweza kuharibu usikivu. Hizi zinaweza kutokana na mageuzi ya mitandao ya mawasiliano lakini hata mfumo wa maisha usiochochea utulivu wa ndani. Kisha kusikiliza, hatua inayofuata ni kung’amua, yaani kufanya maamuzi sahihi juu ya wito. Hatua hii muhimu inahitaji msaada na mwanga wa Roho Mtakatifu kwa njia ya sala. Na ni muhimu kujifunza kuyatafsiri mazingira tuliyomo na kujiuliza “Mungu anataka nifanye nini hapa, wakati huu na katika mazingira haya? Papa anasema wito anaokuitia Mungu daima una utume wa kinabii kumwilishwa katika mazingira ya wakati. Kisha kung’amua hufuata kuuishi wito wenyewe.

Akitukumbusha maneno ya Kristo mwenyewe aliposema “leo maneno haya yametimia masikioni mwenu” (Lk. 4:21) anatualika kutokusubiri mpaka mashaka au giza la mang’amuzi ya wito liishe bali kuanza kuuishi wito tulioupokea mara moja. Anaendelea kusema kuwa “Tusisubiri na kungoja hadi tutakapokuwa wakamilifu ili tuanze kuitikia wito wake na kusema “ndiyo” kwa umkarimu bali tuifunue mioyo yetu tukiuitikia mwaliko wa Bwana. Tuiitikea sauti yake, tuufanye utume wake binafsi katika Kanisa la ulimwengu na mwisho tuiishi siku ya leo ambayo Mungu ametujalia”.

Bikira Maria Malkia wa Mitume, atuombee.

Padre William Bahitwa.

VATICAN NEWS.








All the contents on this site are copyrighted ©.