2018-04-19 07:49:00

Ujumbe wa Papa Francisko kwa Siku ya 55 ya Kuombea Miito Duniani 2018


Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo, daima amekuwa akiwasindikiza waja wake hata katika njia ngumu za maisha yao, zinazosheheni mavumbi na matope. Anatambua fika kiu ya upendo iliyoko ndani mwao na hivyo anawaita kushiriki furaha yake. Hiki ndicho kiini cha ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Siku ya 55 ya Kuombea Miito Duniani inayoadhimishwa na Mama Kanisa, Jumapili ya Mchungaji mwema, tarehe 22 Aprili 2018. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kutafakari kwa kina mambo makuu matatu: kwanza kabisa kujenga utamaduni na sanaa ya kusikiliza; pili, kufanya mang’amuzi ya miito na tatu ni kuishi upya wa maisha kama unavyopata utimilifu wake katika ufunuo wa Kristo Yesu.

Baba Mtakatifu anasema, ujumbe huu ni mwendelezo wa tafakari kwa ajili ya maandalizi ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana itakayoadhimishwa Mwezi Oktoba, 2018 hapa mjini Vatican, kwa kuongozwa na kauli mbiu: “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya Miito”. Hii itakuwa ni nafasi ya kutafakari kwa kina mwaliko wa furaha kama kiini cha maisha kwa watu wa marika mbali mbali. Maisha na uwepo wa watu hapa duniani ni kadiri ya mpango wa Mungu na wala si kwa nasibu tu! Mwenyezi Mungu daima anapenda kukutana, kutembea na kuambatana na waja wake ili kuzima kiu ya upendo inayowaka ndani mwao.

Katika umoja na utofauti wa miito ndani ya Kanisa, kuna haja ya kujikita katika mchakato wa: kusikiliza, kung’amua na kuishi kama alivyofanya Kristo Yesu kabla ya kuanza utume wake wa hadhara. Alipata nafasi ya kujitenga na malimwengu, akaenda kusali Jangwani kwa muda wa siku arobaini, akatembelea Sinagogi la Nazareti, akasikiliza kwa makini na hatimaye, akawaambia watu wote waliokuwemo humo “leo Maandiko haya yametimia masikioni mwenu” (Lk. 4:16-21).

Mosi: Kusikiliza kwa makini: Baba Mtakatifu anasema, Mwenyezi Mungu anazo njia mbali mbali ambazo anazitumia kumwita mja wake kadiri ya mazingira na uzoefu wa kila siku bila kuathiri uhuru wa mtu binafsi. Wakati mwingine, sauti yake inafifishwa na malimwengu pamoja na makando kando yanayowazunguka watu katika mawazo na nyoyo zao. Kumbe, kuna haja ya kujifunza sanaa ya kusikiliza kwa umakini zaidi ili kupima mambo kadiri ya mwanga wa imani na kujiachilia wazi mikononi mwa Roho Mtakatifu ili kuona maajabu yake katika maisha yao! Ili kupata mang’amuzi haya, kuna haja ya kuwa wazi mbele ya Mungu, ili kuweza kuota ndoto kubwa zaidi na hivyo kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa mpango wa Mungu anayetaka kuandika historia pamoja nao!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, hata Yesu katika maisha yake, alitwa na kutumwa, akajiandaa katika sala na upweke wa ndani, akasoma na kutafakari Maandiko Matakatifu na kwa mwanga na nguvu ya Roho Mtakatifu akawafunulia watu maana ya Maandiko haya, huku akifanya rejea katika maisha yake binafsi na historia ya Waisraeli katika ujumla wao. Kusikiliza kwa makini ni changamoto kubwa katika ulimwengu mamboleo ambao umesheheni kelele za kila aina na taarifa za habari kila upande kiasi kwamba, wakati mwingine, watu wanachanganyikiwa na kukosa mwelekeo katika maisha. Hali kama hii inawanyima waamini fursa ya kusimama kidogo na kufurahia tafakari ya matukio mbali mbali katika maisha na hivyo kujiaminisha mbele ya mpango wa Mwenyezi Mungu katika maisha ya waja wake kwa kufanya mang’amuzi yenye kuzaa matunda!

Pili: Kung’amua: Yesu alipokuwa kwenye sinagogi la Nazareti, aliwafafanulia Maandiko Matakatifu, kutoka chuo cha Nabii Isaya na kusema “Roho wa Bwana yu juu yangu, kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini Habari Njema, amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, na vipofu kupata kuona tena, kuwaacha huru waliosetwa, na kutangaza mwaka wa Bwana” (Lk. 4:18-19). Katika mwelekeo kama huu wa mang’amuzi ya maisha ya kiroho, kila mwamini anaweza kutambua wito wake. Huu ni mchakato unaomwezesha kila mwamini kufanya maamuzi msingi, kwa kujadiliana na Mwenyezi Mungu pamoja na kusikiliza sauti ya Roho Mtakatifu, kwa kuanzia na uchaguzi wa maisha ya kila mwamini.

Baba Mtakatifu anaendelea kudadavua kwa kusema, wito wa Kikristo daima una mwelekeo wa kinabii, kwani hata katika Maandiko Matakatifu, inaonekana kwamba, manabii walitumwa katika: hali na mazingira tete: kwa watu waliotopea katika mmong’onyoko wa maisha ya kiroho, maadili na utu wema. Manabii walikuwa ni wajumbe wa Mungu waliotumwa kutangaza na kushuhudia wongofu wa ndani, matumaini na faraja; wakawasaidia watu kutafsiri matukio mbali mbali ya maisha yao mintarafu mwanga wa Mungu uliofukuzia mbali vivuli vya historia yao!

Hata leo hii, kuna haja ya kufanya mang’amuzi na kuendelea kujikita katika unabii, kwa kukataa kishawishi cha sera potofu na mabaya katika maisha, ili kugundua ndani mwao uhusiano wao na Mwenyezi Mungu, mazingira, njia na hali mbali mbali ambazo Mwenyezi Mungu anatumia ili kuwaita waja wake katika furaha ya maisha. Kila Mkristo anapaswa kukuza uwezo wa kusoma ndani mwake maisha yake na kuelewa wapi na kwa jinsi gani anaitwa na Mwenyezi Mungu, ili kutekeleza utume wake!

Tatu: Kuishi: Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kristo Yesu alitangaza upya wa maisha unaoibua furaha katika baadhi ya nyoyo za watu na ukakasi kwa baadhi ya watu. Yesu ni utimilifu wa nyakati, ni Masiha aliyetiwa mafuta kuwahubiri maskini Habari Njema, aliyetumwa kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, na vipofu kupata kuona tena, kuwaacha huru waliosetwa, na kutangaza upendo wa huruma ya Mungu kwa kila kiumbe na Maandiko haya Matakatifu yanapata utimilifu wake kwa wale wanaomsikiliza.

Furaha inayobubujika kutoka katika Injili ndiyo inayowawezesha waamini kufunua maisha yao, tayari kukutana na Mwenyezi Mungu pamoja na jirani zao, kwa haraka na moyo mkuu, tayari kufanya maamuzi magumu katika maisha! Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuchangamka na kuondokana na tabia ya kukaa kitako huku wakichungulia madirishani, kwani huko watajikuta wanaambulia patupu pasi na kufanya maamuzi ya maisha. Utume wa Kikristo ni sasa na wala hakuna muda wa kupoteza! Kila mwamini anaitwa katika wito maalum ndani ya Kanisa kama mama: waamini walei katika maisha ya ndoa na familia; mapadre katika maisha na utume wa Daraja Takatifu au katika maisha ya kitawa, ili kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa Kristo Yesu, kwa wakati huu!

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya 55 ya Kuombea Miito Duniani kwa Mwaka 2018 anaendelea kudadavua kwa kusema, Leo iliyotangazwa na Kristo Yesu inaendelea kushuka hapa duniani ili kuikoa familia ya binadamu, ili hatimaye, kuwashirikisha waamini katika utume wake. Kristo Yesu anaendelea kuwaita watu kuishi pamoja naye na kumfuasa kwa ukaribu zaidi, tayari kumhudumia moja kwa moja. Kwa wale wote wanaosikia kutoka katika undani wao kwamba, wanaitwa kujisadaka kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu, hawana sababu ya kuogopa! Inapendeza sana, na hii ni neema kubwa kuwekwa wakfu kwa ajili ya Mungu na huduma makini kwa jirani! Hata leo hii, Mwenyezi Mungu anaendelea kuita na kuwatuma watu, wasisubiri hadi pale watakapokuwa wakamilifu ili kuweza kujibu kwa kusema “Mimi hapa Bwana”.

Baba Mtakatifu Francisko mwishoni mwa ujumbe wake, anawataka waamini wasiogope uwepo wa dhambi na mapungufu katika maisha yao, bali waweze kuwa na ujasiri wa kufungua “hazina” ya nyoyo zao, tayari kusikiliza kwa makini sauti ya Mungu, ili kufanya mang’amuzi ya kina kuhusu wito wa kila mmoja wao mintarafu utume wa Kanisa na ulimwengu katika ujumla wake, ili hatimaye, kuweza kuishi leo ambayo Mwenyezi Mungu katika wema na ukarimu wake, anawakirimia. Bikira Maria Mtakatifu, ambaye katika ujana wake aliweza kusikiliza, akakubali na kupata mang’amuzi ya Neno wa Mungu aliyetwaa Mwili na kukaa kati ya watu wake, awalinde na kuwasindikiza waamini katika hija ya maisha yao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.