2018-04-18 13:54:00

Umuhimu wa majadiliano ya kidini katika vyuo vikuu!


Majadiliano ya kidini yanapaswa kuwa ni mpango mkakati unaomwilishwa katika ngazi mbali mbali za maisha ya waamini, kuanzia kwenye familia, masuala ya kidiplomasia pamoja na mwingiliano wa tamaduni kati ya watu, ili kujenga msingi wa maridhiano, umoja na udugu, kwa kutambua kwamba wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kuwa tofauti zao msingi ni utajiri unaopaswa kuendelezwa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kamwe dini zisiwe ni chanzo cha vita, kinzani na mipasuko ya kijamii kwani kwa kufanya hivi, ni kwenda kinyume kabisa cha asili na uwepo wa Mungu ambaye ni chemchemi ya: furaha, wema, haki, amani na upendo mkamilifu!

Majadiliano ya kidini kati ya waamini wa dini mbali mbali ni nyenzo msingi ya kupambana na tabia ya ubinafsi na hali ya kudhaniana vibaya ili kujenga na kudumisha umoja, upendo, mshikamano na maridhiano kati ya watu, kila mtu akipewa nafasi ya kushuhudia imani yake kama kielelezo cha uhuru wa kidini na kuabudu ambao ni msingi wa haki zote za binadamu. Waamini wa dini mbali mbali duniani, wanapaswa kukita maisha yao katika sala na majadiliano ya kidini yanayosimikwa katika ukweli na uwazi; kwa kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu wamoja; kwa kushikamana katika huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni!

Hii ndiyo changamoto ambayo imetolewa hivi karibuni na Askofu Miguel Angel Ayuso Guixot, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini katika ziara yake ya kikazi, nchini Kenya, ambako ameshiriki katika kongamano la majadiliano ya kidini lililokuwa limeandaliwa na Chuo Kikuu cha Tangaza kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Kiislam cha Umma nchini Kenya. Katika hotuba yake elekezi, Askofu Guixot amekazia umuhimu wa taasisi za elimu ya juu pamoja na vyuo vikuu kushirikiana na kushikamana katika mchakato wa majadiliano ya kidini kati ya Wakristo na Waislam ili kuleta mabadiliko chanya Barani Afrika.

Amewashirikisha wajumbe wa kongamano hili katika maisha na utume wake kama Mmisionari wa Shirika la Wacomboni aliyebahatika kufundisha katika taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu nchini Sudan na Misri, akateuliwa kuwa ni Rais wa Taasisi ya Masomo ya Kiarabu na Dini ya Kiislam, (PISAI) mjini Roma na kwa sasa ni Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini. Anasema, katika maisha na utume wake, majadiliano ya kidini yamekuwa ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kwani kwa njia hii, amepata fursa ya kukutana, kushirikiana na kushikamana na waamini wa dini ya Kiislam sehemu mbali mbali za dunia, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!

Ametambua na kuthamini tofauti msingi kati ya waamini wa dini ya Kiislam na Kikristo, akazitumia kama utajiri wa kujenga na kudumisha mshikamano na mafungamano ya kijamii, katika utekelezaji wa miradi ya huduma kwa maskini na wahitaji zaidi kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa dunia inayomsikwa katika haki, umoja, udugu, amani na upendo katika huduma. Lengo kuu ni kukuza na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Katika imani na Mapokeo ya dini hizi mbili, kuna tofauti msingi, lakini pia kuna mambo ambayo yanaweza kuwaunganisha kwa pamoja. Kumbe, jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, waamini wa dini hizi mbili wanajielekeza zaidi kukuza na kudumisha mambo yanayowaunganisha na kuwawajibisha na kuachana na yale yanayotaka kuwachongamisha na kuwagawa.

Viongozi na waamini wa dini mbali mbali wawe ni vyombo na mashuhuda wa misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu na washindane katika kutenda mema kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Vita na kinzani za kijamii, hazina macho wala pazia, hazichagui wala hazibagui. Umoja, upendo, mshikamano na amani ni mambo yanayojengeka siku kwa siku! Kumbe, mchakato wa majadiliano ya kidini unapaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu kwani hii ni sehemu ya vinasaba na utambulisho wao kama waamini.

Kuna haja ya kujenga na kudumisha mtandao wa taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu, ili kushiriki kikamilifu katika majadiliano ya kidini, kwa kujikita katika masomo ya maisha ya kiroho, ili kuwarithisha waamini wa dini mbali mbali utajiri na amana za maisha ya kiroho, kiutu na kimaadili zinazobubujika kutoka katika dini mbali mbali duniani.  Kama anavyosema baba Mtakatifu Francisko, vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu kwa asili yake, vinapaswa kuwa ni maabara ya majadiliano, mahali pa watu kukutana katika huduma ya ukweli, haki, ulinzi na tunza makini ya utu na heshima ya binadamu katika kila hatua ya maisha. Taasisi hizi ziwe ni maabara ya kufanya upembuzi yakinifu katika shida, magumu, fursa na changamoto zinazomwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo na kuzipatia ufumbuzi wa kudumu katika mwanga wa imani, matumaini na mapendo. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika Tamko la “Nostra aetate” yaani uhusiano wa Kanisa na dini zisizo za Kikristo linakazia: majadiliano, ushirikiano na ushuhuda kutoka kwa waamini wa dini mbali mbali ili kukuza na kudumisha: haki jamii, tunu msingi za maisha ya kiroho na kimaadili, amani, uhuru, ustawi na maendeleo ya wengi!

Chuo Kikuu cha Tangaza na Chuo Kikuu cha Kiislam cha Umma nchini Kenya vinaweza kushirikiana kwa karibu zaidi katika masomo na tafiti za kisayansi; kwa kuibua kanuni na mbinu za ushirikiano ili kujibu maswali tete katika maisha ya binadamu. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume nchini Misri, kunako mwezi April, 2017 kwa kutembelea Chuo Kikuu cha Al Azhar kilichoko Cairo, alisikika akisema kwamba, viongozi wa kidini wanayo dhamana ya kuhakikisha kwamba, wanasaidia kujenga na kudumisha utamaduni wa amani duniani unaojikita katika mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kudumisha usalama wa watu na mali zao. Viongozi wa kidini wawe mstari wa mbele kutangaza na kushuhudia utakatifu wa maisha ya mwanadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu ili kuondokana na utamaduni wa kifo unaosimikwa hasa zaidi katika misimamo mikali ya kidini na kiimani, ambayo imepekea watu wengi kupoteza maisha  na mali zao kutokana na mashambulizi ya kigaidi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.