2018-04-18 14:26:00

Furahini na kushangilia, utakatifu ni mchakato wa mapambano ya kiroho


Baba Mtakatifu Francisko ametoa Wosia wa Kitume “Gaudete et exsultate” yaani “Furahini na kushangilia, wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo” (Mt. 5:12) umezinduliwa, Jumatatu, tarehe 9 Aprili 2018, Kumbu kumbu ya Bikira Maria kupashwa habari kuwa atakuwa ni Mama wa Mungu. Kristo Yesu anawaalika wote wanaoteseka au kudhulumiwa kwa ajili yake, kufurahi na kushangilia, kwani yeye ni chemchemi ya maisha na furaha ya kweli. Anataka waja wake kuwa kweli ni watakatifu, mwaliko na changamoto inayojionesha katika sehemu mbali mbali za Maandiko Matakatifu.

Baba Mtakatifu anasema, lengo la wosia huu ni mwaliko wa kuwa watakatifu katika ulimwengu mamboleo; kwa kutambua vizingiti, changamoto na fursa ambazo zinaweza kutumiwa na waamini kufikia utakatifu wa maisha. Kristo Yesu anawaalika waja wake ili wawe watakatifu, watu wasiokuwa na hatia mbele zake katika upendo. (Rej. Ef. 1:4). Wosia huu wa kitume umegawanyika katika sura kuu tano: Sura ya kwanza ni Wito wa utakatifu; Sura ya Pili ni Adui wa utakatifu; Sura ya tatu: Mwanga katika maisha ya Mwalimu, Sura ya nne: Alama za Utakatifu wa maisha katika ulimwengu mamboleo na Sura ya tano: Mapambano ya maisha ya kiroho; kukesha na kufanya mang’amuzi!

Sura ya tano: Mapambano ya maisha ya kiroho; kukesha na kufanya mang’amuzi! Baba Mtakatifu Francisko anasema, maisha ya kikristo ni mapambano endelevu yanayohitaji nguvu na ujasiri, ili kumpatia nafasi Kristo aweze kushinda na hatimaye, waamini kufurahia maisha. Waamini watambue kwamba, shetani, Ibilisi yupo na wala si dhana ya kufikirika tu! Waamini wawe macho na waendelee kukesha na kusali kwa kutambua kwamba, ushindi wao unafumbatwa katika Msalaba wa Kristo. Utakatifu ni chemchemi ya furaha na amani ya ndani. Huu ni mwaliko wa kupambana na “giza la maisha ya kiroho” kwa kujikita katika mang’amuzi ya maisha ya kiroho kwa kutafakari kwa kina na mapana matamanio halali ya maisha, uchungu na fadhaa katika maisha yao; hofu na mashaka ili kutambua njia zinazowaelekeza katika uhuru wa kweli, daima wakijitahidi kusoma alama za nyakati kadiri ya mwanga wa Kristo Mfufuka. Mang’amuzi ya maisha ya kiroho, yawasaidie waamini kutambua Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Waamini wampatie nafasi Kristo Yesu ili aweze kuzungumza kutoka katika undani wa maisha yao! Furaha ya kweli anasema Mtakatifu Bonaventura imetundikwa kwenye mti wa Msalaba. Waamini wamwombe Roho Mtakatifu ili aweze kuwaondolea woga na hofu zisizokuwa na mashiko ili kuanza mchakato wa kutoka katika ubinafsi, tayari kuliendea Fumbo la maisha ya Mungu, anayewasaidia waja wake kutekeleza utume wao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya ndugu zao katika Kristo! Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha Wosia wa Kitume “Gaudete et exsultate” yaani “Furahini na kushangilia, wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo” kwa kumwangalia Bikira Maria aliyemwilisha Heri za Mlimani kuliko mtakatifu yoyote yule. Ni mwanamke aliyefurahia uwepo wa Mungu katika maisha yake na kuhifadhi yote katika sakafu ya moyo wake!

Bikira Maria ni Mtakatifu kuliko watakatifu wote. Ni kimbilio la waamini katika ulinzi na tunza ya kimama. Anawafundisha na kuwasindikiza waamini katika utakatifu wa maisha; anawalinda bila kuwahukumu; anawafariji, kuwaombea na kuwatakatifuza kwa uwepo wake, changamoto na mwaliko kwa waamini kumkimbilia katika sala. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Wosia huu wa kitume utawasaidia waamini kuambata hija ya utakatifu wa maisha, ili kweli waweze kuwa ni watakatifu kwa ajili ya utukufu wa Mungu kwa kusaidiana na kuhimizana katika mchakato wa utakatifu wa maisha, ili waamini wote waweze kushiriki furaha ya uzima wa milele.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.