2018-04-18 13:24:00

Changamoto ya uwajibikaji wa pamoja katika utunzaji wa mazingira


Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume Laudato si  yaani ”Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” anatoa mwelekeo wa ustaarabu mpya wa maisha unaojikita katika Mafundisho Jamii ya Kanisa kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa: Mwenyezi Mungu muumba wa mbingu na nchi; binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; mazingira na kazi ya uumbaji ambayo mwanadamu amekabidhiwa ili kuilinda, kuitunza na kuiendeleza. Baba Mtakatifu anapembua kwa kina na mapana kuhusu ekolojia ya binadamu na ekolojia ya mazingira; mambo ambayo ni sawa na chanda na pete, waswahili wangesema ni sawa na “uji kwa mgonjwa” kwani yanakwenda pamoja, yanategemeana na kukamilishana. Huu ni mwaliko wa kuitafakari dunia mintarafu jicho la Mungu, ili kuitunza dunia, iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi; kwa kupyaisha mahusiano kati ya mfumo wa maisha ya binadamu na mazingira.

Inasikitisha kuona kwamba, shughuli nyingi zinazofanywa na binadamu zimechangia kwa kiasi kikubwa uharibifu wa mazingira, kumbe, hapa kuna haja ya kuwa na uwiano bora zaidi, ili kazi ya uumbaji iweze kuleta mafao, ustawi na maendeleo kwa binadamu, kwa leo na kwa jili ya vijana wa kizazi kipya. Kwa mwamini mazingira ni jambo takatifu linalonesha mahusiano makubwa kati ya Mungu na viumbe wake. Kumbe, maendeleo ya sayansi na teknolojia yasaidie kuboresha mazingira na kamwe yasiwe ni chanzo cha uharibifu wa mazingira na matokeo yake ni athari za mabadiliko ya tabianchi yanayosababisha umaskini na majanga kwa watu na mali zao sehemu mbali mbali za dunia.

Hapa kuna umuhimu wa kuwa na mwelekeo mpya katika kufikiri, kutenda na kuishi ili kupambana na kinzani za kimazingira na kijamii zinazoendelea kumwandama mwanadamu kiasi cha kutopea katika majanga asilia na kudhani kwamba hii ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya binadamu! Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican hivi karibuni, ameshiriki katika mkutano wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Oceania:Federation of Catholic Bishops' Conferences of Oceania (F.C.B.C.O.) huko Port Moresby, Papua New Guinea kwa kukazia sana umuhimu wa uwajibikaji wa pamoja katika kulinda, kutunza na kuendeleza mazingira nyumba ya wote. Huu ni wajibu fungamanishi kwa wanasiasa na wananchi wa kawaida wanaopaswa kubadili mtindo na mfumo wa maisha yao, ili uweze kuleta tija zaidi.

Mkutano huo ulikuwa unaongozwa na kauli mbiu “Utunzaji wa nyumba ya wote Oceania: kuna bahari ya fursa”. Nchi za Oceania zimekuwa ziliathirika sana na athari za mabadiliko ya tabianchi kiasi cha kuwa ni kati ya vyanzo vikuu vinavyowatumbukiza watu katika dimbwi la umaskini wa hali na kipato! Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, ni mchakato unaokwenda sanjari na usimamiaji makini wa: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kardinali Parolin anakaza kusema, hii inatokana na ukweli kwamba, uchafuzi na uharibu mkubwa wa mazingira unaoendelea kufanywa na binadamu una madhara makubwa si tu kwa nchi za Oceania, bali kwa ulimwengu mzima. Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji; watu wasiokuwa na makazi kutokana na mafuriko na ukame wa muda mrefu; changamoto ya ukosefu wa fursa za kazi na ajira ni mambo ambayo yanaleta mtikisiko mkubwa katika ustawi, maendeleo na mafungamano ya kijamii katika Jumuiya ya Kimataifa.

Kwa upande wake Padre Victor Roche, Katibu mkuu wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Oceania anasema, mkutano huu uliofunguliwa tarehe 11-18 Aprili 2018 umelenga zaidi katika kuibua mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji, utakaoweza kujibu changamoto za athari za mabadiliko ya tabianchi zinazoendelea kuleta maafa makubwa kwa watu: kijamii, kisiasa na kiuchumi. Maaskofu kwa kuangalia changamoto zote hizi, wameamua kuzipembua katika mwanga wa Injili, kanuni maadili na utu wema, daima mwanadamu akipewa kipaumbele cha kwanza.

Umefika wakati kwa watu kutumia vyema rasilimali za dunia kwa kuwajibika badala ya mwelekeo wa sasa unaowatumbukiza katika ubinafsi, uchoyo, rushwa na ufisadi wa mali ya umma. Kuna wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta: usalama, hifadhi na maisha bora zaidi! Hii ni changamoto pevu na endelevu kwa wakati huu kutokana na ukweli kwamba, kila kukicha watu wanalalama kutoka na athari za mabadiliko ya tabianchi! Kwa sasa hata ukarimu kwa waathirika imekuwa ni changamoto kubwa kutokana na umaskini wa watu na hali mbaya ya uchumi kwa familia nyingi!

Kardinali Parolin, akiwa nchini Papua New Guinea, amefurahia ukarimu wa familia ya Mungu Jimbo kuu la Port Moresby linaloongozwa na Kardinali John Ribat aliyekuwa ameandamana na Askofu mkuu Kurian Mathewe Vayalunkal, Balozi wa Vatican kwenye Visiwa vya Oceania. Kardinali Parolin, kwa nyakati mbali mbali ameihakikishia familia ya Mungu nchini humo, sala na sadaka ya Baba Mtakatifu Francisko na kwamba, uwepo wake miongoni mwao, ulilenga kwa namna ya pekee kabisa, kushirikishana furaha na upendo unaobujika kutoka kwa Kristo Mfufuka. Kardinali Parolin amepata nafasi pia ya kukutana na kuzungumza na familia ya Mungu pamoja na viongozi wakuu wa Serikali ya Papua New Guinea.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.