2018-04-17 10:21:00

Wanawake wanapaswa kushirikishwa kikamilifu katika mchakato wa amani


Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuendelea kusimama kidete kupinga ukatili na nyanyaso za kijinsia dhidi ya wanawake, ili kuwajengea uwezo wa kushiriki kikamilifu katika kukuza na kudumisha amani na usalama. Kuna mafanikio makubwa ambayo yamekwisha kupatikana kukuza na kudumisha haki msingi za wanawake, lakini bado kuna changamoto katika masuala ya ulinzi na usalama zinazopaswa kuvaliwa njuga. Uhalifu wa kijinsia bado unaendelea kusikika katika maeneo ya vita, kumbe, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inasikiliza na kujibu kilio cha wanawake, ili kuwajengea uwezo utakaowashirikisha katika mchakato mzima wa kutafuta, kulinda na kudumisha amani duniani!

Jambo la pili ni kwa Jumuiya ya Kimataifa kujizatiti katika kudumisha haki msingi, utu na heshima ya wanawake katika maeneo ya vita na mipasuko ya kijamii. Wanawake washirikishwe kikamilifu katika masuala ya ulinzi na usalama. Hii ni changamoto ambayo imetolewa hivi karibuni na Askofu mkuu Bernardito Auza, Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa, wakati akichangia mada kwenye mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Anasema, hata baada ya kumalizika kwa vita na kinzani, kuna haja ya kuendelea kuwajengea uwezo wanawake kisheria, ili wale wote waliohusika katika nyanyaso za kijinsia wanafikishwa kwenye mkondo wa sheria na haki inatendeka! Lakini, lengo la kwanza liwe ni kuzuia vita, kinzani na mipasuko ya kijamii kwa kujenga utamaduni wa haki, amani na maridhiano kati ya watu! Wanawake wawezeshwe pia kielimu na kiuchumi ili matunda ya amani ya kudumu yazidi kuendelezwa kwa ajili ya wengi.

Askofu mkuu Auza anakiri kwa kusema, Kanisa katika maisha na utume wake, limekuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu makini na endelevu kwa wasichana na wanawake bila ubaguzi wa kidini, kikabila, kiitikadi au mahali anapotoka mtu! Wanawake kutoka Chuo kikuu cha Kikatoliki cha Bethlehemu wamekuwa mstari wa mbele katika kujenga na kudumisha: haki, amani na maridhiano huko nchini Palestina: Wahusika wa mauaji katika ngazi mbali mbali wanapaswa kufikishwa mbele ya sheria. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume nchini PerĂ¹ hivi karibuni, alisikika akilaani dhuluma na nyanyaso dhidi ya wanawake na wasichana kwamba, hivi ni vitendo ambavyo havikubaliki kwa jamii kwani vinakwenda kinyume cha utu na heshima ya wanawake. Vatican inapenda kuhakikisha kwamba, wanawake na wasichana wanashiriki kikamilifu katika mchakato wa kutafuta, kujenga na kudumisha haki, amani na maridhiano kati ya watu. Wanawake wakishirikishwa kikamilifu, amani ya kweli inaweza kupatikana.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.