2018-04-17 09:31:00

Waamini wanapaswa kuwa ni mashuhuda vyombo na manabii wa huruma!


Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume “Misericordia et misera” yaani “Huruma na haki” anasema, huruma ya Mungu inapaswa kuendelezwa katika medani mbali mbali za maisha ya watu kama utimilifu wa huruma, upendo na msamaha wa Mungu unaobubujika kutoka katika Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo kutoka kwa wafu! Huruma ya Mungu inajionesha katika maadhimisho ya Sakramenti mbali mbali za Kanisa, lakini kwa namna ya pekee kabisa, Sakrameti ya Ekaristi Takatifu, Upatanisho na Mpako wa Wagonjwa.

Huruma ya Mungu inaendelea kujifunua katika historia na maisha ya watu kwa njia ya Neno la Mungu, ikikumbukwa kwamba,  Biblia ni muhtasari wa ufunuo wa huruma ya Mungu kwa binadamu! Changamoto anasema Baba Mtakatifu ni kwa Jumuiya za Kikristo kuhakikisha kwamba, zinaendelea kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu, kama kielelezo makini cha imani tendaji. Kwa njia hii, Kanisa litaendelea kuwa kweli ni shuhuda wa huruma ya Mungu na kama sehemu ya utambulisho wa Kanisa.

Hivi karibuni, Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Uinjilishaji mpya limehitimisha mkutano wa Wamisionari wa huruma ya Mungu, waliobahatika kuadhimisha Jumapili ya huruma ya Mungu, wakakutana na kuzungumza na hatimaye, kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu pamoja na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Wamisionari wa huruma ya Mungu wamejinoa kwa mara nyingine tena kuhusu: “Upatanisho: Ni Sakramenti ya huruma ya Mungu! Dhambi na huruma ya Mungu katika maisha na utume wa Padre: Wamisionari wa huruma ya Mungu kadiri ya mtazamo wa Papa Francisko pamoja na ushauri wa kichungaji kuhusu Sakramenti ya Upatanisho! Ikumbukwe kwamba, huruma ya Mungu ni kati ya vipaumbele vya pekee katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko.

Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Uinjilishaji mpya amehitimisha mkutano huu kwa kufafanua kuhusu Wamisionari wa huruma ya Mungu kadiri ya mtazamo wa Papa Francisko. Anasema, huruma ya Mungu ni muhtasari wa upendo unaomwambata mtu mzima: kiroho na kimwili. Huruma hii kadiri ya Baba Mtakatifu Francisko inamwilishwa kwa namna ya pekee katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama yalivyofafanuliwa na kumwilishwa wakati wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Ni huruma inayoshuhudiwa katika maisha ya kila siku kama chachu ya utakatifu wa maisha na wala si dhana inayoelea katika ombwe! Huruma ya Mungu ni kielelezo cha imani tendaji inayomwezesha mwamini kusimama kidete: kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Huruma ya Mungu inabubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, kiini na utilimifu wa upendo wenyewe! Wale wote wanaojibidisha katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, wanaonja na kuwaonjesha jirani zao, upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka! Askofu mkuu Fisichella anawataka waamini katika ujumla wao, kuwa kweli ni mashuhuda, vyombo na manabii wa huruma ya Mungu katika ulimwengu mamboleo.

Huu ni utume unaovaliwa njuga na Baba Mtakatifu Francisko kwa wakati huu, kinyume kabisa na wazushi waliojitokeza kwenye Kanisa la mwanzo, wakachafua na kuvuruga dhana ya unabii wa huruma ya Mungu kwa waja wake. Hata leo hii kuna watu wanaoendelea kuogelea katika uzushi kutokana na ukali wa mawazo kiasi cha kusahau: haki na huruma ya Mungu kwa waja wake. Huruma ya Mungu ni unabii endelevu katika maisha na utume wa Kanisa! Ni changamoto ya kutubu na kumwongokea Mungu; kwa kuendelea kumwilisha huruma yake katika uhalisia wa maisha ya watu, kama kielelezo makini cha imani tendaji!

Kwa upande wake, Monsinyo Octavio Ruiz Arenas, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Uinjilishaji mpya ametoa ushauri wa shughuli za kichungaji mintarafu Sakramenti ya Upatanisho kadiri ya maelekezo na ushauri unaotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa Mapadre waungamishaji. Injili ya Baba mwenye huruma; iwasaidie Mapadre waungamishaji kuwa na mwelekeo wa huruma kwa wadhambi wanaotubu na kumwongokea Mungu; watu wanaotaka kuanza kuandika tena kurasa za historia na maisha yao kwa kuambata huruma, upendo na msamaha wa Mungu.

Mapadre watambue na kuthamini utu na heshima ya wale wanaotubu, wawapatie nafasi ya kujuta na kujiwekea malengo ya kusonga mbele, licha ya udhaifu na mapungufu yao ya kibinadamu. Wamisionari wa huruma ya Mungu, wawapokee, wawasikilize na kuwashauri vyema wale wote wanakimbilia huruma na upendo wa Mungu katika hija yao ya maisha. Mapadre watambue kwanza kabisa wanapaswa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu unaomwilishwa katika maadhimisho ya Sakramenti za huruma ya Mungu na huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.