2018-04-17 11:44:00

Jumapili ya Kristo Mchungaji mwema, Siku ya Kuombea Miito Duniani!


Maisha ya wafugaji wa kabila la Wabedui yaweza kutusaidia katika kuelewa neno la Mungu leo. Wao wanaishi jangwani na wao ni wafugaji tena wahamaji. Hukaa muda wote na kondoo na huwepo uhusiano mkubwa kati ya mchungaji na kondoo na uhusiano huo huwa wa karibu mno katika maisha hayo ya jangwani kiasi kwamba mchungaji na kondoo wanafahamiana kabisa. Kondoo hufahamu vizuri sauti ya mchungani na mchungaji huwafahamu kondoo wake hata kwa tabia zao. Mchungaji na kondoo huwa marafiki, hupendana. Katika mazingira yetu tunaweza kuelewa mfano huu tukiangalia maisha ya makabila ya wafugaji. Upo uhusiano mkubwa kati ya mfugaji na mifugo kiasi kwamba hata kwa alama ng’ombe anaweza kuelewa alama za ishara zinazofanywa na mfugaji na kutii alama au sauti ( kwa mfano mluzi) inayoashiria jambo fulani.

Katika Maandiko Matakatifu Zab. 23 tunasoma habari ya mchungaji mwema; Bwana, mchungaji wa watu. Tunaambiwa kuwa sala hii ni ya matumaini na inatumia picha mbili kuelezea upendo wa Mungu kwa watu wake. Aidha picha ya Mungu kama Mchungaji wa taifa la Israeli – Zab. 80:2 ni ya kawaida  katika Agano la Kale, hasa miongoni mwa manabii (Isa. 40:11; Ezek.34:11-16). Katika Agano Jipya, Yesu alitumia jina hili la cheo kwa ajili yake mwenyewe kama ilivyo katika injili ya leo na pia anapewa cheo hiki na waandisi wa baadaye wa Agano Jipya – Ebr. 13:20; 1Pt. 2:25; Ufu. 7:17. Cheo cha mchungaji kwa upana wake humtambulisha yule anayeongoza ulimwenguni katika nafasi ya Mungu – kama wafalme, makuhani na viongozi kwa ujumla wake. Pamoja na mfano huu wa mchungaji mwema upo pia uwezekano wa mchungaji mwovu – nabii Ezek. 34:1 – analaani hili. Nabii anaagizwa na Mungu kuwafukuza wachungaji wake, wale ambao wanajichunga wenyewe.

Katika injili ya leo, Yesu anajiita mchungaji mwema lakini kwa mtazamo mpya, ila zaidi ya kuwa mchungaji, yuko tayari kutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo. Huu ni mtazamo mpya na aina mpya ya uhuru kama iliyo katika somo la pili la leo – 2Kor. 3:17 – Bwana ni Roho, na penye Roho wa Bwana, ndipo penye uhuru. Kadiri ya mwinjili Yohana, upendo wa Mungu ni juu ya yote na ni kitu cha thamani kuliko vitu vyote. Mwinjili Yohana anauliza upendo ni nini? Katika 1 Yoh. 4:10 – anasema ‘huu ndio upendo; si kwamba sisi tulimpenda Mungu, bali kwamba yeye alitupenda sisi, akamtuma Mwana wake awe malipizi ya dhambi zetu’. Na hitimisho la mwinjili Yohana kuhusu upendo ni hili ‘Mungu ni upendo na mwenye kuishi katika pendo, anaishi ndani ya Mungu na Mungu anaishi ndani yake’ – 1 Yoh. 4:16. Ufahamu huu wa aina ya upendo tunauona pia katika kitabu cha Nabii Hosea anapoongea juu ya upendo wa kimungu na ukuu wake. Katika sura ya 11 anaongea juu ya upendo wa Mungu wakati Israeli alipokuwa mtoto – kwamba alimwita alipokuwa mtoto, akamwita toka Misri. Pamoja na kwamba hawakumsikia, yeye alizidi kuwapenda na kuwaokoa.

Katika Injili, Yesu anaendelea kusema kuwa anawafahamu kondoo. Katika Biblia kufahamu maana yake inahusisha akili na moyo. Ni namna nyingine ya kusema kupenda. Na alipotoa uhai wake kwa ajili yetu, basi ufunuo wa upendo wake ulikamilika. Tukumbuke kuwa mwonekano wa upendo kati yetu huoneshwa katika uhusiano wetu na Mungu. Huonekana kwetu sisi kwa kuitwa wana wa Mungu. Ni kujazwa na hilo pendo la Mungu. Pendo la Mungu latufanya sisi kuwa wanae na latubidisha katika kuishi pendo hilo. Sisi ni watu tuliojazwa na pendo lake. Dhana hii ya mchungaji mwema inaendana na pendo la dhati lililodhihirishwa na Mungu Baba. Kwa njia hii sisi tumepata wokovu kwa njia ya Kristo. Yule aliyelifahamu pendo hili anaalikwa kuishi huu wito mtakatifu. Kuishi pendo hilo.

Nimalizie tafakari hii kwa kushirikisha mfano wa ushuhuda wa Kardinali Heenan. Kardinali Heenan alielekezwa na daktari wake kupumzika sababu ya udhaifu wa afya na alihamia katika nyumba iliyokuwa sehemu za mashambani huko Hertfordshire. Kabla hajafika huko, alipokea barua toka kwa mkristo wake akilalamikia mabadiliko yaliyojitokeza baada ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican akiweka wazi kuwa ameamua kuachana na Kanisa Katoliki. Katika barua yake, huyu mkristo aliandika wazi kuwa anaamini kwamba Mwadhama Kardinali hatajali sana na kuipa uzito barua iliyotoka kwa mkristo wake, tena asiyejulikana na anayesema kuwa anaachana na Kanisa Katoliki. Kumbe, Kardinali Heenan akamjibu kwa upole, mimi ni mchungaji na wewe ni mmoja wa kondoo wangu. Ninarudi London mara moja kukutana nawe ili kwa pamoja tupate ufumbuzi wa tatizo lako. Tunaambiwa kuwa alimpata huyu kondoo aliyepotea.

Ndugu zangu, hii ndiyo maana ya kuwa mchungani mwema. Wote ni kondoo wake Mungu awe mkubwa au mdogo. Maelezo ya mchungaji mwema anayeutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo wake yanamdokeza mtumishi anayeutoa uhai wake kama sadaka kadiri ya Isa. 53:10 – ‘Bwana ametaka kumponda mtumishi wake kwa mateso, amemhuzunisha, amefanya maisha yake kuwa sadaka ya malipo ya dhambi. Naye ataona uzao wake, atazidisha siku zake, nayo mapenzi ya Bwana yatatimia kwa mikono yake’.

Tumsifu Yesu Kristo.

Padre Reginald Mrosso, C.PP.S.
All the contents on this site are copyrighted ©.