2018-04-16 10:16:00

Vyuo vikuu vina dhamana ya malezi na majiundo makini ya vijana


Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni alipokutana na wajumbe wa Baraza pamoja na Bodi ya Wakurugenzi wa Chuo Kikuu cha “Villanova” kutoka Philadelphia nchini Marekani, alisema, hitaji msingi kwa wakati huu ni mchakato wa ujenzi wa dira yenye mwelekeo wa kikatoliki, umoja wa familia ya binadamu na ujenzi wa mshikamano unaotekelezeka kama njia ya kupambana na ukosefu wa usawa na haki, mambo ambayo yanaendelea kujitokeza katika ulimwengu mamboleo. Vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu kwa asili yake, vinapaswa kuwa ni maabara ya majadiliano, mahali pa watu kukutana katika huduma ya ukweli, haki, ulinzi na tunza makini ya utu na heshima ya binadamu katika kila hatua!

Jumapili, tarehe 15 Aprili 2018 Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Moyo Mtakatifu wa Yesu, “Sacro Cuore” kilichoanzishwa na Padre Agostino Gemelli, huko Milano, nchini Italia, kimeadhimisha Siku ya 94 ya Kitaifa kama sehemu ya mchakato endelevu wa taasisi hii muhimu ya Kanisa katika kujizatiti kwenye huduma kwa vijana wa kizazi kipya, kwa kutoa elimu na majiundo makini: kiutu, kitamaduni na kitaaluma mintarafu tunu msingi za maisha ya Kikristo! Taasisi hii ikishirikisha na vitivo mbali mbali imeendelea kuwa ni tumaini kwa vijana wa kizazi kipya.

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, katika barua aliyomwandikia Askofu mkuu Mario Delpini, wa Jimbo kuu la Milano, ambaye pia ni Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Juu ya Giuseppe Toniolo, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko anasema, licha ya changamoto na matatizo ya ukosefu wa fursa za ajira kutokana na kuchechemea kwa uchumi, hali inayopelekea vijana kushindwa kufanya maamuzi magumu katika maisha yao, hasa katika mchakato wa ujenzi wa familia makini, wanapaswa bado kuendelea kujikita katika kukuza na kudumisha mafao ya wengi, haki na amani. Tema iliyoongoza maadhimisho kwa mwaka 2018 ni “Warithi na wagunduzi. Vijana ni wadau wa historia.

Hii ni changamoto kwa taasisi ya elimu kama hii, kuhakikisha kwamba, inakuwa ni dira na mwongozo kwa vijana wa kizazi kipya ili kuweza kufikia malengo, kwani wakati mwingine, licha ya kuwa wameunganika kwa pamoja, lakini, wanaweza kutumbukia katika ombwe! Vijana kwa njia ya matumizi ya mitandao ya kijamii, wanaweza kujisikia kuwa ni raia wa ulimwengu, lakini kwa bahati mbaya, bado wanajisikia wapweke na watu wasioridhika katika maisha.

Vijana wana uwezo wa kuwasiliana na watu wengi, wakiwa na malengo makubwa kwa siku za usoni, lakini dhamana na wajibu mkubwa wa chuo kikuu ni kuwajengea vijana hawa uwezo wa kielimu na kitamaduni, daima wakitumia amana na urithi mkubwa wa ujuzi na maarifa waliyorithi katika historia. Kwa njia hii, vijana wanaweza kuwa ni wagunduzi na watu wanaoweza kutumia maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Kardinali Parolin anakaza kusema, Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha “Sacro Cuore”, kinawajibika kuwajengea vijana uwezo wa ugunduzi kwa kuzingatia urithi na amana ya kiutu na maisha ya kiroho yanayofumbatwa katika hekima na busara ya maisha ya Kikristo kwa kuzingatia misingi mikuu minne ambayo ni: utafutaji wa ukweli, tafakari ya kina kuhusu uzuri; hamu na kiu ya dhati kabisa katika kukuza na kudumisha majadiliano pamoja na kukubali kupokea mema na mazuri kutoka kwa wengine ili kujenga na kudumisha: utulivu, mshikamano na amani. Ili kuweza kutekeleza ndoto hii, watu kama Mwenyeheri Giuseppe Toniolo na Padre Agostino Gemelli, Armida Barelli, Lodovico Necchi pamoja na Monsinyo Francesco Olgiati, waliweza kuanzisha Taasisi ya Elimu Katoliki, inayoendelea kuwasha moto katika nyoyo na akili za vijana wengi ndani na nje ya Italia.

Kardinali Parolin anaendelea kufafanua kwamba, Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake, anaendelea kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utume wa vijana wa kizazi kipya, ili waweze kutekeleza ndoto katika maisha yao, wakiwa wanaongozwa na kusimamiwa na Moyo Mtakatifu wa Yesu. Vijana hawa wanapaswa kusimamiwa kikamilifu, ili waweze kutekeleza malengo yao ya muda mfupi na mrefu, kwa kujikita katika malezi na majiundo makini ya kiutu na yanayofumbata tunu msingi za maisha ya Kikristo. Baba Mtakatifu anapenda kuwahakikishia vijana uwepo wake kwa karibu kwa njia ya sala na sadaka yake, anawaomba vijana pia kumkumbuka na kumsindikiza katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Anawatakia wanajumuia wote heri na baraka katika maadhimisho haya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.