2018-04-16 11:03:00

Ujumbe wa Vatican: Silaha za sumu zina madhara makubwa kwa binadamu!


Askofu mkuu Ivan Jurkovič, Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa na Mashirika ya Kimataifa yaliyoko mjini Geneva, nchini Uswiss, hivi karibuni akizungumza na kikundi cha wataalam wa serikali kuhusu Uhuru wa Mfumo wa Silaha za Sumu, Lethal Autonomous Weapons Systems (LAWS) anakiri kwamba, Jumuiya ya Kimataifa kwa muda wa miaka mitano imekuwa ikijita katika mjadala huu, kwa matumaini kwamba, hatimaye, Jumuiya ya Kimataifa itapata muafaka wa kisheria na kimaadili utakaosaidia kuratibu na kudhibiti silaha za sumu! Hii inatokana na ukweli kwamba, matumizi ya silaha za sumu ni kitendo kinachokwenda kinyume kabisa cha utu na heshima ya binadamu, changamoto na mwaliko kwa Serikali mbali mbali kuangalia tena upya uwezo wao wa kijeshi.

Askofu mkuu Ivan Jurkovič anasema, matumizi ya nguvu za kijeshi hayana budi kufanyiwa tathmini kubwa mintarafu uhalali wake, nia na madhumuni yake; kwa kuzingatia sheria kanuni maadili. Changamoto kubwa iliyoko mbele ya Jumuiya ya Kimataifa ni matumizi ya mashine zinazojiendesha zenyewe katika mapambano ya kivita, hali ambayo inaleta mkanganyo mkubwa katika masuala ya kimaadili. Sheria kanuni inayozingatia utu na heshima ya mwanadamu inapaswa kuwa sheria rejea katika matumizi ya silaha!

Lakini, ili kuweza kufikia maamuzi haya kuna haja ya kuwa na uelewa wa kina kuhusu utu na heshima ya binadamu! Mosi, matumizi ya mashine zinazojiendesha zenyewe haziwezi kuwajibishwa kimaadili na kwamba, zinakwenda kinyume kabisa cha dhamiri nyofu na utu wema! Pili, matumizi ya mashine zinazojiendesha zenyewe yanaweza kupangwa na kuratibiwa na wanasiasa au viongozi wa kijeshi kwa ajili ya kuwashambulia raia ili kujiimarisha kijeshi, jambo ambalo linakwenda kinyume kabisa cha uamuzi unaoweza kutolewa na mtu mwenye dhamiri nyofu. Kumbe, mauaji ya raia yanapotokea katika mazingira kama haya, hakuna mtu anayeweza kuwajibishwa kwa kuvunja sheria ya kimataifa kuhusu haki msingi za binadamu na sheria za kiutu! Tatu, matumizi ya mashine zinazojiendesha zenyewe ni ushuhuda wa kukosa imani kwa binadamu kwa kukataa kuwajibika kadiri ya utashi ambao Mwenyezi Mungu amemkirimia mwanadamu.

Hapa Askofu mkuu Ivan Jurkovič anasema mwanadamu anapokonywa uwezo wake wa kufikiri na kutenda. Amani na usalama wa Jumuiya ya Kimataifa unaweza kupatikana kwa kujizatiti zaidi na zaidi katika utamaduni wa majadiliano na ushirikiano na wala si katika mashindano ya kutengeneza, kuhifadhi na kutumia silaha. Ujumbe wa Vatican unapenda kutoa changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inasitisha mashindano ya silaha na kuanza mchakato wa Serikali kuaminiana ili kumwilisha matumaini ya watu wengi wanaotaka kuishi katika mazingira ya amani na utulivu. Katika ulimwengu ambamo silaha zinazojiendesha zenyewe zinaruhusiwa kufanya kazi bila ya kuratibiwa na akili pamoja na utashi wa binadamu, kutasababisha majanga makubwa kwa maisha ya watu na mali zao, hali ambayo itadhohofisha umoja na udugu katika familia ya binadamu!

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” anasema, binadamu anao uhuru unaohitajika wa kudhibiti na kusimamia teknolojia; kwa kutumia teknolojia hii kwa ajili ya kuleta aina nyingine ya maendeleo, ambayo ni maridhawa, yenye utu zaidi yanayosimikwa katika jamii na yenye utimilifu zaidi. Maneno haya yanaweza kumwilishwa katika majadiliano ya kuhusu “Uhuru wa Mfumo wa Silaha za Sumu”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.