2018-04-16 13:33:00

Padre Deogratias Matika ateuliwa kuwa "Mtawala wa Jimbo la Moshi"


Neema, furaha na amani ya Kristo Mfufuka viwe nanyi nyote.Wapendwa familia ya Mungu. Ninapoendelea kujifunza mazingira mapya ya kufanyia utume, nimeonelea kuwasalimu na kutoa shukrani za dhati kabisa, kwanza kwa Mwenyezi Mungu na pili kwa Wanajimbo Katoliki Moshi. Ninazungumzia Muda wa miaka kumi (10) ya utumishi wangu kama mchungaji Mkuu wa Jimbo Katoliki Moshi. Namshukuru Mungu kwa yote aliyotujalia tukaweza kupiga hatua kichungaji na kimaendeleo. Namshukuru zaidi kwa afya, ushirikiano na mabadiliko chanya ya kuendesha shughuli za kanisa kwa uwazi na ufasaha zaidi. Naomba muendelee na hayo tuliyoyafanikisha na kuyaboresha kwa sifa na utukufu wa Mungu, heshima ya Kanisa na kwa wokovu wa watu.

Aidha, nawashukuru wanajimbo kwa kuipokea kaulimbiu ya "Mwondoko - Kuwajibika na kushirikiana katika Kristo". Baada ya kutafsiri kwa matendo kaulimbiu hiyo, tumeshuhudia mwamko wa kufanikisha mipango ya Jimbo, Parokia, Parokia teule na Vigango. Kaulimbiu hiyo imehamasisha utekelezaji wa mpango Mkakati wa Jimbo letu. Nawapongeza wote waliowajibika na kushirikiana wakizingatia dira, utume na tunu msingi za mpango mkakati 2016 - 2020. Sasa tupo katikati ya kipindi hicho. Inafaa kufanya tathmini ili tuweze kujipanga vyema tukiangaziwa na malengo tuliojiwekea tulipouzindua Mkakati huo. Nawashukuru Mapadre na walei waliohamasisha utekelezaji wa mpango mkakati. Kiukweli maendeleo hayajileti yenyewe. Ni lazima yatafutwe, tena kwa gharama. Tunayo mifano hai ya kijimbo na kiparokia ya kutupa hamasa ya kushirikiana zaidi hasa kwa kushirikisha kila mdau ili aelewe na kutoa ushirikiano mkubwa. Naomba tumshukuru Mungu kwa kuimarisha hatua tunazozipiga na kuziboresha.

Kutokana na mimi kuhamishiwa Jimbo Kuu Katoliki Arusha, nawaomba wanamoshi mjitambue katika changamoto ya kipindi hiki cha mpito. Mchakato wa kumtafuta mchungaji mkuu umeshaanza. Wanamoshi salini kwa moyo na imani ili Mwenyezi Mungu atupatie mtumishi huyo. Baada ya muda mtapelekewa sala hiyo ya kuomba maongozi ya Mungu katika swala hilo. Tunapoendelea na sala, ni muhimu tuwe na utulivu, uwajibikaji na kulinda umoja. Sio ajabu watu wengine watatumia muda huu wa mpito kuvuruga watu kwa maneno yasiyo na faida. Natoa tahadhari tusiwape nafasi watu hao wasio na mapenzi mema. Kwa barua hii, Nawatangazieni rasmi kwamba tangu tarehe 11 Aprili 2018, Mheshimiwa Padre DEOGRATIAS MATIKA alichaguliwa na Baraza la Askofu Jimbo Katoliki Moshi chini ya Usimamizi wangu kuwa "MTAWALA WA JIMBO" mpaka tutakapompata Askofu. Kwahiyo atashughulikia mambo yote ya kiutawala kikamilifu kuendana na Mkusanyo wa Sheria Kanuni za Kanisa {Kan. 428 - 430}.

Mumpokee kwa moyo wa furaha kwakuwa analifahamu Jimbo na tumesafiri pamoja katika kulihudumia Jimbo akiwa Wakili wa Askofu. Nahitimisha nikiwashukuru watu binafsi, makundi ya watu kwa zawadi zote mlizonipa nilipotembelea Parokiani au mlipofika Kanisa Kuu. Aidha nashukuru kwa zawadi ya kuniaga nilipopangwa kwenda Arusha. Sikuweza kumwandikia kila mmoja binafsi ila natoa shukrani zangu za dhati kwa ukarimu wa aina yoyote mlionitendea. Mwenyezi Mungu awazidishie, na Kristo Mfalme atawale mioyo yenu kwa mapendo na amani yake, mzae matunda ya furaha katika familia na miito ichipue na kudumu.

Amani ya Bwana iwe nanyi daima.

Wenu katika Kristo,

Mha. Isaac Amani

ASKOFU MKUU JIMBO KUU KATOLIKI ARUSHA.








All the contents on this site are copyrighted ©.