2018-04-14 17:09:00

Tubuni na kuongoka, ili muweze kuwa ni mashuhuda wa Kristo Mfufuka


Furaha ya Pasaka ni furaha inayomwalika mwamini kuwa shahidi wa ufufuko wa Kristo; kutangaza kifo chake na kuutukuza ufufuko wake mpaka atakapokuja. Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika tafakari ya Neno la Mungu kwa dominika ya tatu ya Pasaka. Maandiko Matakatifu katika dominika hii yanatuangazia kuuona ufufuko wa Kristo kuwa si jambo la nadharia au jambo la kufikirika lililo nje ya mpango wa kawaida wa vitu bali ni tukio la kihistoria kwa maana kwamba ni jambo halisi lililotokea (Rej. KKK 643). Tena, ufufuko ni tukio linaloujulisha ulimwengu juu ya hatia yake na kualika wongofu ili kuingia katika mpango wa neema wa Mungu.

Masomo kwa ufupi: Somo la kwanza (Mdo. 3:13-15, 17-19). Somo hili ni sehemu ya hotuba ya Mtume Petro. Mazingira ya hotuba hii ni baada ya yeye Petro na Mtume Yohane kumponya kiwete aliyekuwa akikaa katika mlango wa Hekalu. Watu walipomwona yule kiwete ameponywa waliwakusanyikia Petro na Yohane wakishangaa juu ya kile kilichotokea. Ndipo hapo Petro anatumia nafasi hiyo kuwahutubia akianza kueleza kuwa si wao, yeye na Yohane, ambao wamemponya kiwete huyo bali ni kwa nguvu za Yesu Kristo. Huyu Yesu Kristo ndiye yule ambao wao, wayahudi, walimuua. Walimuua kwa sababu walimkataa, na hata mbele ya Pilato wakawa radhi kumruhusu muuaji aachiliwe ili Yesu auwawe. Wakamtetea mwangamizaji wa uhai na kumhukumu Mkuu wa uzima. Kwa kosa hili kubwa ambalo walilifanya bila kujua, Petro aliwaalika watubu wapate maondoleo ya dhambi na wayaanze maisha mapya na Kristo Mfufuka ambaye ndiye pia ndiye aliyetabiriwa na manabii tangu kale.

Somo la pili (1Yoh. 2:1-5a). Katika ujumla wake, Mtume Yohane aliandika waraka huu kwa jumuiya ya Makanisa ya Asia Ndogo. Huko walikuwa wameibuka watu walioanza kuwapotosha wengine kwa mafundisho yao na Yohane anawaandikia kurekebisha hali hiyo. Sehemu ya waraka huo ambao ni somo la pili dominika hii, Yohane anatoa katekesi kwa wakristo juu ya kuwa “waana wa Mungu” na aina ya maisha wanayopaswa kuishi kulingana na hali hiyo ya wana wa Mungu. Yohane anagusia kipengele cha dhambi. Anapozungumza juu ya dhambi na upatanisho kwa dhambi si kwamba anahalalisha watu kutenda dhambi kwa sababu msamaha na upatanisho upo, la hasha. Anawaasa waondokane na dhambi. Ni sawa kabisa kama kutangaziwa uwepo wa dawa ya kutibu malaria kusipohalalisha watu kutokujikinga na malaria! Mtume Yohane anawaasa waondokane na dhambi kwa kuzishika amri za Mungu na kuiishi amri ya mapendo.

Injili (Lk.24:35-49). Yesu anawatokea Mitume kumi na mmoja; anawathibitishia kuwa amefufuka na anawapa utume wa kuwa mashahidi wa ufufuko. Mitume waliopaswa kufundisha na kutoa ushuhuda wa ufufuko wa Kristo walihitaji wao kwanza kuondolewa kila chembe ya hofu na mashaka juu yake. Hivyo, kwanza anawaonesha mwili wake wauone na wamshikeshike ili wahakikishe kuwa sio mzimu bali ni yeye yule yule waliyemfahamu. Pili, aliwaomba chakula na anakula mbele yao. Jambo hili Mitume wanalitumia sana baadaye katika mafundisho yao juu ya ufufuko wa Kristo “...ndio sisi tuliokula na kunywa pamoja naye baada ya kufufuka kwake kutoka kwa wafu” (Rej. Mdo. 10:41). Tatu anafungua uelewa wao kuhusu Maandiko Matakatifu kwamba ufufuko wake ni utimilifu wa yote yaliyoandikwa katika Torati ya Musa, katika Manabii na Zaburi. Kisha kuwaondolea hofu na mashaka, anatuma kama mashahidi wa Habari Njema.

Tafakari: Maandiko Matakatifu yanatoa ushuhuda mkubwa sana juu ya tukio la ufufuko wa Kristo. Na ushuhuda huu umewahusisha Mitume kwa namna ya pekee zaidi. Wao kama masahidi wa ufufuko na mashahidi wa Kristo Mfufuka wanakuwa ni jiwe la Msingi la Kanisa alilokuja kulianzisha Kristo mwenyewe. Mitume wanakuwa msingi kwa sababu imani ya jumuiya ya kwanza ya waamini wa Kanisa hili ni imani iliyojengwa juu ya ushahidi wao thabiti juu ya ufufuko, ushahidi ambao walianza kuuhubiri kwa ulimwengu mzima wakianzia Yerusalem. Zaidi ya hao, Mtume Paulo anasema waziwazi kuu ya watu zaidi ya 500 ambao Yesu aliwatokea kwa pamoja (Rej 1Kor 15:4-8; Mdo 1:22).

Katika kipindi hicho cha Mitume haikuwa rahisi kiasi hicho kuamini juu ya ufufuko wa Kristo. Kwa Mitume, mateso ya Kristo waliyoyashuhudia yaliwapa mshtuko mkubwa sana ndiyo maana injili inaonesha wanapopata habari kuwa amefufuka badala ya kufurahi “wanakunja nyuso zao” wanakuwa na hofu na hata awali hawakuwasadiki akinamama waliokuwa wamerudi toka kaburini na wakaona maneno yao kuwa kama upuuzi tu. Hata baada ya mitume kuondolewa hofu na kuanza kuhubiri juu ya ufufuko, mafundisho juu ya ufufuko wa Kristo yaliendelea kukabiliwa na upinzani na hali ya kutokupoleka. Katika nyakati zetu leo kutokupoleka kwa mafundisho juu ya ufufuko wa Kristo huenda si zaidi sana kuwa Kristo amefufuka au hakufufuka bali ni kuwa ufufuko wake unadai mabadiliko katika maisha yetu ili tupokee mwaliko wa kuingia katika mpango wa neema wa Mungu. Huu ni mpango wa wokovu ambao Mungu anao kwa wanadamu, mpango ambao uliatabiriwa na Manabii katika Agano la Kale na unakamilishwa na Kristo mwenyewe. Kristo hakufa kwa dhambi za wayahudi tu bali kwa dhambi za ubinadamu mzima, kumbe kama vile Mtume Petro alivyowaalika wao kutubu kwa kumuua Kristo, anaualika ubinadamu mzima kutubu na kutambua kuwa  matendo yake ya dhambi ni kuendelea kumsulubisha tena Kristo.

Jambo la pili ni kwamba mwaliko huo wa kutubu ni mwaliko pia wa kutambua kuwa dhambi ipo. Kanisa alilolianzisha Kristo lina kati ya sifa zake utakatifu lakini utakatifu kamili wa washiriki wake ni lazima bado kuutafuta. Papa Francisko anasema Kanisa ni kama hospitali ya kutibu majeruhi walio na majeraha mengi yakiwemo makubwa kabisa ya dhambi. Ni mahala pa upatanisho, mahala pa msamaha na maondoleo ya dhambi kwa sakramenti ya Kitubio kama anavyousia pia Mtume Yohane katika somo la pili dominika ya leo.

Tunapoyaangalia maisha yetu katika nyakati hizi yanarudi maneno ya Papa Pius XII kuwa “dhambi kubwa tuliyonayo katika nyakati zetu ni kutokujua kwamba kuna dhambi”. Chini ya mwamvuli wa uhuru wa mwanadamu yote yanahalalishwa. Hatutendi tena kadiri ya hekima ya kimungu - “mema na mabaya” au kadiri ya kanuni ya kimaumbile - “ninachopaswa kufanya na nisichopaswa kufanya”. Ni kana kwamba kanuni ya kuishi na kufanya mambo tuliyonayo ni “kufanya ninachopenda, ninachokiona ni kizuri na ninachoona kinanipa manufaa”. Hata maisha kwa ujumla yanakuwa “ninaishi ninavyotaka katika namna ninayoipenda na ninayoona inanifaa”. Siajabu ndio maana wengi bado hawaoni umuhimu wa kupokea sakramenti ya kitubio kwa sababu tu hawaoni dhambi.

Mausia ya Mtume Yohane juu ya kutokutenda dhambi leo yatukumbushe kuwa binadamu si kipimo cha dhambi. Kama anavyoendelea kuusia, kipimo cha dhambi ni Mungu mwenyewe kama anavyofunua katika sheria zake na amri ya mapendo. Ni katika mwono huu anatualika kutambua nguvu ya mabadiliko ya maisha inayopatikana katika msamaha wa dhambi, huduma ya kanisa waliyokabidhiwa mitume kuiendeleza kama mwendelezo wa uwepo wa nguvu ya Kristo Mfufuka. Ushahidi wa ufufuko wa Kristo unaotualika kuanza maisha mapya pamoja naye utupe ujasiri wa kuhoji mustakabali wa maisha yetu juu ya uhalisia wa dhambi na nguvu ya kutoa ushuhuda wa wongovu kwa njia ya msamaha wa dhambi.

Bikira Maria malkia wa mashahidi, atuombee na atusaidie daima.

Na Padre William Bahitwa, VATICAN NEWS.

 

 

 
All the contents on this site are copyrighted ©.