2018-04-14 08:30:00

Tafakari ya Fumbo la Kifo, Jimbo la Same katika Mwanga wa Pasaka


Sakramenti zote, na hasa zile za kuingizwa katika Ukristo, zina kama lengo, Pasaka ya mwisho ya mtoto wa Mungu, ile ambayo kwa kifo inamwingiza katika uzima wa Ufalme wa mungu. Sasa kinatimilizika kile alichokisadiki katika imani na matumaini: “Nangojea ufufko wa wafu na uzima wa ulimwengu ujao”. Maana ya Kikristo ya kifo imefunuliwa katika mwanga wa Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu, ambaye ndani mwake, waamini wanachota tumaini lao moja, yaani kwa kutoka katika maisha ya hapa duniani ili kukaa pamoja na Mwenyezi Mungu, milele yote!

Kanisa linafundisha kwamba, kwa Mkristo siku ya kifo huanzisha, mwishoni mwa maisha yake ya Kisakramenti, utimilifu wa kuzaliwa kwake upya kulikoanzishwa na Sakramenti ya Ubatizo kwa kufanana kamili na “sura ya Mwana” kulikotolewa kwa mpako wa Roho Mtakatifu na ushirika katika karamu ya Ufalme wa Mungu, uliotangulizwa katika Fumbo la Ekaristi Takatifu, hata kama analazima bado kutakaswa zaidi ili kuvikwa vazi la arusi! Familia ya Mungu nchini Tanzania, lakini kwa namna ya pekee kabisa, Jimbo Katoliki Same, inajiuliza swali gumu ambalo pengine halina majibu ya haraka haraka kutokana na vifo vya mapadre watatu katika muda wa siku mbili!

Hawa ni Marehemu Padre Michael Kiragheja, kilichotokea Maua, Jimbo Katoliki la Moshi, tarehe 11 Aprili 2018 wakati akiwa usingizini, alikokuwa anahudhuria mafungo ya kiroho kwa Mapadre wa Jimbo Katoliki la Same, akiwepo pia Askofu Rogath Kimaryo wa Jimbo Katoliki la Same! Wakati bado, wanaendelea kutafakari juu ya Fumbo la kifo, taarifa nyingine ikatolewa kwamba, Padre Arbogasti Mndeme, aliyekuwa anapatiwa matibabu kwenye Hospitali ya KCMC, naye amefariki dunia! Familia ya Mungu Jimbo Katoliki Same, ikapigwa butwaa! Maziko ya Mapadre hawa wawili, walioshiriki katika huduma ya kutangaza na kushuhudia Mafumbo ya Kanisa, ilipangwa kufanyika Jumanne, tarehe 17 Aprili 2018 kwenye Seminari Ndogo ya Chanjale, Jimbo Katoliki la Same!

Katika maandalizi haya, Padre Raymond Saba, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, akatangaza tena kifo cha Padre Ubaldus Kidavuri wa Jimbo Katoliki la Same, aliyekuwa Katibu mtendaji wa Idara ya Utume wa Walei, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania amefariki dunia, akiwa usingizini. Padre Kidavuri anakumbukwa na wengi kutokana na huduma yake Radio Vatican alipokuwa anaandaa Kipindi cha Liturujia ya Neno la Mungu. Amewahi pia kuwa ni Mhariri mkuu wa Gazeti la Kiongozi linalomilikiwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Familia ya Mungu nchini Tanzania na kwa namna ya pekee kabisa Jimbo Katoliki la Same, tunaiombea iendelee kulitafakari Fumbo la Kifo katika mwanga wa Fumbo la Pasaka! Taarifa kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania zinasema kwamba,  Ibada ya kuaga rasmi mwili wa Padre Ubaldus Kidavuri itafanyika Kurasini, kuanzia saa 5:00 na baadaye mwili wake kusafirishwa kwenda Jimboni Same kwa mazishi yanayotarajiwa kuongozwa na Askofu Rogath Kimaryo. Roho za marehemu mapadre hawa pamoja na waamini wote zipate rehema kwa Mungu na wapumzike kwa amani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.