2018-04-14 15:46:00

Kardinali Rai: futilieni mbali vita; jengeni utamaduni wa amani!


Kardinali Bechara Boutros Rai, Patriaki wa Kanisa la Wamaroniti Wakatoliki nchini Lebanon anasikitika kusema kwamba, wakati huu ambapo “Mataifa Makubwa” yanaendelea kupiga ngoma ya vita huko Syria, hakuna hata chembe ya lugha ya amani inayosikika kiasi cha kusahau mateso na mahangaiko ya mamilioni ya wananchi wa Syria kutokana na vita inayoendelea huko kwa takribani miaka saba sasa! Hawa ni watu wanaoteseka kutokana na ukame wa kutisha, uhalifu wa kitaifa na kimataifa; uharibifu mkubwa wa miundo mbinu na makazi ya watu; ni wananchi wanaoendelea kuteseka kutokana na vitendo vya kigaidi na vita inayopukutisha maisha ya watu wasiokuwa na hatia!

Kardinali Bechara Boutros Rai katika ujumbe wake kwa Jumuiya ya Kimataifa anakaza kusema, kuna wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum milioni moja na laki saba kutoka Syria wanaopatiwa hifadhi nchini Lebanon. Hawa ni watu ambao wamefugiwa mipaka na nchi za Ulaya! Hizi ni nchi zile zile ambazo leo hii zinaendelea kushabikia mashambulizi ya kijeshi yanayopania kwa mataifa makubwa kupimana nguvu za kijeshi mateso na mahangaiko ya wananchi wa Siria huko Lebanon.

Kardinali Bechara Boutros Rai anapenda kuchukua fursa hii kuitaka Jumuiya ya Kimataifa kumaliza vita na hatimaye, kuanzisha mchakato wa kubainisha malengo ili kujenga na kudumisha misingi ya haki na amani ya kudumu inayofumbatwa katika majadiliano na juhudi za kidiplomasia na wala si kwa mtutu wa bunduki. Wananchi wa Mashariki ya Kati wanayo haki ya kuishi katika amani na utulivu. Jumuiya ya Kimataifa kwa kutaka kujikita kwenye vita ni kuonesha udhaifu wake kwani ujenzi wa amani ni ushuhuda wa nguvu na wenye mvuto! Viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa watambue kwamba, watu wanafahamu siku ya kuanza vita, lakini hawatambui hata kidogo siku ya kumalizika kwa vita hii. Viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa wajenge hofu ya Mungu na kusikiliza kilio cha watu wanaoteseka kutokana na vita huko Mashariki ya kati. Umefika wakati wa kufutilia mbali vita na kuanza kujenga utamaduni wa amani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.