2018-04-14 16:07:00

Hati ya Maandalizi ya Sinodi ya Amazonia yapitishwa na Sekretarieti


Wajumbe washauri wa Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia itakayoadhimishwa mwezi Oktoba, 2019 na kuongozwa na kauli mbiu “Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ekolojia endelevu” wamehitimisha kikao chao cha kwanza kilichofunguliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 12-13 Aprili 2018 hapa mjini Vatican. Kardinali Lorenzo Baldiserri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu alitoa hotuba elekezi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia, kwa kumshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa uwepo na mchango wake katika mkutano huu wa awali. Baba Mtakatifu amewashukuru wataalam ambao wengi wao ni kutoka katika Mtandao wa Kanisa Amerika ya Kusini, (Pan-Amazon Ecclesial Network of the Latin American Church, REPAM).

Wajumbe wamepata nafasi ya kuchambua muswada wa hati ya maandalizi kwa ajili ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia. Wajumbe wameupongeza muswada huu ulioandaliwa na Sekretarieti kuu ya Sinodi ya Maaskofu kwa msaada wa wataalam mbali mbali! Wajumbe wakatoa maoni yao ni jinsi ya kuuboresha zaidi. Wajumbe wakati wa majadiliano yao, wameonesha umuhimu wa Ukanda wa Amazonia katika mustakabali wa utunzaji wa mazingira nyumba yote!

Wajumbe wamepembua kwa kina na mapana hali ya shughuli za kichungaji, umuhimu na hitaji la kuanzisha mchakato wa safari mpya ya uinjilishaji inayofumbatwa katika dhana ya utamadunisho kwa wananchi mahalia. Sehemu ya pili, imeangalia kwa namna ya pekee, changamoto na matatizo yanayotishia ekolojia katika Ukanda wa Amazonia na kuonesha umuhimu wa ekolojia endelevu kama inavyodadavuliwa na Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”. Baada ya majadiliano na tafakari ya kina, wajumbe kwa kauli moja, wamepitisha hati ya maandalizi ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia, itakayotumwa kwa wadau mbali mbali ili kuanza rasmi mchakato wa kupokea maoni na ushauri kwa ajili ya maadhimisho ya Sinodi hii. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru wajumbe wote kwa mchango wao, ari na moyo wa umoja na mshikamano ulioneshwa wakati wote wa mkutano huu wa maandalizi ya hati ya maandalizi ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 








All the contents on this site are copyrighted ©.