2018-04-14 15:24:00

Chuo kikuu ni maabara ya majadiliano, huduma, ukweli, haki na utu!


Hija mbali mbali zinazofanywa na waamini mjini Roma zinalenga kuimarisha maisha ya kiroho. Ni maneno yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 14 Aprili 2018 alipokutana na Baraza pamoja na Bodi ya Wakurugenzi wa Chuo Kikuu cha “Villanova” kutoka Philadelphia nchini Marekani, kinachochota hekima na utajiri wake katika tafiti kutoka katika “Shule ya Mtakatifu Agostino.” Lengo ni kukuza na kurithisha Mapokeo ya Kanisa Katoliki kwa wanafunzi wa kizazi kipya, kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Agostino, katika ujana wake.

Uaminifu katika dira kama Jumuiya inayojikita katika tafiti na masomo, haina budi kujipima kwa kuangalia changamoto changamani zinazofumbatwa katika kanuni maadili na tamaduni zinazoibuka kila kukicha katika ulimwengu mamboleo. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba kila sehemu ya maisha na utume wake, Chuo kikuu cha Villanova kitaendelea kujizatiti katika kutekeleza dhamana yake ya kurithisha tunu msingi za kiakili, kiroho na kimaadili, ili kuwaandaa vijana wa kizazi kipya kuweza kushiriki kwa hekima na busara katika majadiliano yanayolenga ujenzi wa jamii kwa siku za usoni!

Baba Mtakatifu anasema, hitaji msingi kwa wakati huu ni mchakato wa ujenzi wa dira yenye mwelekeo wa kikatoliki, umoja wa familia ya binadamu na ujenzi wa mshikamano unaotekelezeka kama njia ya kupambana na ukosefu wa usawa na haki, mambo ambayo yanaendelea kujitokeza katika ulimwengu mamboleo. Vyuo vikuu kwa asili yake, vinapaswa kuwa ni maabara ya majadiliano, mahali pa watu kukutana katika huduma ya ukweli, haki, ulinzi na tunza makini ya utu na heshima ya binadamu katika kila hatua!

Dhamana hii ni muhimu sana kwa taasisi inayosimamiwa na kuongozwa na Kanisa Katoliki kama kilivyo Chuo Kikuu cha Villanova, kwani kinachangia katika maisha na utume wa Kanisa, ili kusaidia ukuaji na ukomavu wa kweli na endelevu wa familia ya binadamu, ili hatimaye, kuweza kufikia utimilifu wake katika Mwenyezi Mungu! Baba Mtakatifu anakiri kwa kusema, hakuna mtu awaye yote aliyefahamu mahangaiko ya moyo wa mwanadamu ambao haukufanikiwa kupata pumziko lake katika Mwenyezi Mungu ambaye kwa njia ya Kristo Yesu anawafunulia waja wake undani wa ukweli na hatima ya maisha yao kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Agostino.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, muda huu wa kutafakari, kujadiliana na kukutana utasaidia kuimarisha dhamana na utume wa Chuo Kikuu kwa ajili ya huduma ya ukweli unaowaweka watu huru. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewaweka wajumbe wa Baraza na Bodi ya Wakurugenzi wa Chuo Kikuu cha Villanuova chini ya sala na maombezi ya Mtakatifu Agostino na ya Mtakatifu Monica na hatimaye, akawapatia Baraka zake za kitume, wakati huu, Mama Kanisa anapoendelea kuadhimisha ushindi wa Kristo Mfufuka!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.